Wednesday, July 31, 2013

Man City yaifumua AC Milan 5-3
Mabao ya Man City yakitiwa kambani na wakali wao David Silva, Aleksandar Kolarov, Micah Richards na Edin Dzeko, Huku mabao ya kufutia machozi kwa upande wa AC Milan yakifungwa na mchezaji wao machachari Stephan El Shaarawy na lengine likifungwa na Andrea Petagna.
Angalia video ya mabao hapa chini

Beckham kumiliki timu Marekani
Beckham (kulia) akiwa pamoja na Ronaldo walipokutana jijini, Los Angeles, Marekani
NYOTA wa zamani wa Los Angeles Galaxy ya Ligi Kuu ya Marekani, David Beckham, anakaribia kutangazwa kuwa mmiliki na bosi mpya wa klabu jijini Miami.
Becks, 38, ana chaguo linalomruhusu kununua hisa katika timu ya Ligi Kuu ya Marekani ‘Major League Soccer – MLS’ baada ya kuichezea LA Galaxy na sasa yuko katika nafasi ya kutumia nafasi hiyo.
Mkataba wa Beckham na Galaxy ulikuwa na kipengele kinachomuwezesha nyota huyo kuanzisha ama kumiliki klabu katika Ligi Kuu kwa dau linaloanzia dola za Marekani milioni 25.
Beckham ameripotiwa mara kadhaa kukutana na bilionea raia wa Bolivia, Marcelo Claure, ambaye amedhamiria kuamua na nyota huyo wa zamani wa Man United na Real Madrid, kuhusu uanzishwaji wa timu mpya na uwanja mpya.
Mkuu wa MLS, Don Garber, alisema: “Sisi tunadhani itakuwa kali David Beckham kushiriki katika ligi yetu. Tutaendelea kujadiliana naye kwa uhakika kuhusu hilo.”
Beckham alistaafu kuichezea LA Galaxy baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, alioiwezesha kuipa klabu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu.
Simba yanasa mshambuliaji, 
Joseph Owino amwaga wino
Mshambuliaji Mpya wa Simba, Betram Mombeki (kulia) akimwaga wino
KATIKA kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza Agosti 24, klabu ya Simba imemsajili rasmi beki wa kati, Joseph Owino na mshambuliaji wa zamani wa Pamba FC ya Mwanza, Betram Mombeki.
Mombeki aliyekuwa akiishi na kucheza soka nchini Marekani, alisaini jana mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Msimbazi.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya uongozi wa Simba, wameamua kumsajili Mombeki baada ya kuridhishwa na kiwango alichokionesha wakati wa majaribio yake.
Kiongozi huyo alisema wanaamini hawajafanya makosa kumsajili wingi huyo ambaye ameonesha kiwango cha juu kipindi chote tangu ajiunge na klabu hiyo kwa majaribio hivyo atawasaidia katika michuano mbalimbali.
Kusajiliwa kwa Mombeki kunafanya idadi ya wachezaji wazawa waliosajiliwa Simba kufikia watano ambapo awali iliwanyakua mshambuliaji Zahor Iddi Pazi aliyekuwa akicheza kwa mkopo JKY Ruvu kutoka Azam, kipa Andrew Ntala kutoka Kagera Sugar na beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutoka Mtibwa Sugar na Twaha Shekuwe ‘Messi’ wa Coastal Union.
Luiz kuing'arimu Bayern pauni mil. 60
MABINGWA wa Europa League, Chelsea, wamewatunishia misuli mabingwa wa Ulaya Bayern Munich na kuwaambia kuwa kiungo Mbrazil inayemuwinda, David Luiz, atawagharimu pauni milioni 60.
Kocha mpya wa Bayern, Pep Guardiola, amebainisha nia ya kumuwania Luiz, 26, ili kukipa nguvu kikosi chake, huku akitenga kitita cha pauni milioni 40 kumng’oa nyota huyo Stamford Bridge na kumpeleka Allianz Arena.
Lakini Chelsea chini ya Kocha mpya, Jose Mourinho, imesisitiza kuwa haiko tayari kumuuza Luiz na The Bavarians aidha ikubali kutoa pauni milioni 60 au iachane na jaribio la kumsajili nyota huyo.
Bayern ilijiona iko katika njia sahihi kufikia utimilifu wa uhamisho wa Luiz, ambaye aliigharimu Chelsea kitita cha pauni milioni 21.3 ilipomsajili akitokea Benfica ya Ureno, Januari 2011 kabla ya dili lao kupingwa na The Blues.
Nguvu ya Bayern pia ilitokana na madai yaliyofunika ujio wa Mourinho, ambaye alidaiwa kutokuwa na mipango ya muda mrefu na Mbrazil huyo, ambaye alikuwa mhimili wa Chelsea kutwaa mataji mawili ya Mabingwa Ulaya na Europa League.
Zidane aingili kati usajili wa Bale
NGULI wa klabu ya Real Madrid, Mfaransa, Zinedine Zidane, ameingilia kati mchakato wa usajili tata unaobaniwa na Tottenham na kuiambia klabu hiyo: Mwacheni Gareth Bale azungumze nasi, vinginevyo hatapata tena nafasi nyingine ya kufanya hivyo.
Zidane, mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ufaransa, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Michezo klabuni Bernabeu, alisema: “Kama yeye ameonesha kuvutiwa kujiunga Madrid, basi Tottenham inapaswa kumruhusu kuzungumza nasi.
“Nafasi ya kuichezea klabu ya Real Madrid inakuja mara moja tu katika mzunguko wa maisha ya mchezaji yeyote yule. Na inaeleweka wazi kuwa Bale hataki kuipoteza nafasi hiyo ya kushindwa kujiunga nasi,” alisema Zidane maaarufu kama Zizzou.
Bale, 24, winga wa kimataifa wa Wales, amebaki kuwa chaguo pekee linaloongoza klabuni Bernabeu, ambapo Madrid iko tayari sasa kuvunja rekodi ya dunia iliyoweka yenyewe kwa kukubali kulipa pauni milioni 95 kumng’oa Spurs.
Licha ya harakati hizo za Madrid kupandisha kila uchao dau la Bale, Tottenham chini ya Mwenyekiti wake, Daniel Levy, imeendelea kukataa kumruhusu nyota huyo kuhama, huku ikisisitiza kuwa winga huyo hauzwi kwa dau lolote.
Zidane, nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, ameongeza presha kwa Spurs kwa kumwambia Bale anapaswa kulazimisha kuvua jezi nyeupe za kikosi chake tayari kuvaa nyeupe zilizo maarufu zaidi za Madrid – mabingwa mara tisa wa soka Ulaya.
Zizzou aliongeza kuwa: “Inakuwa hali isiyo ya kawaida moyoni mwa mchezaji yeyote anapotambua kuwa anahitajiwa Real Madrid, ni kwamba lazima apate msisimko na hamasa kubwa kutokana na hilo.
“Hakuna kitu cha fahari zaidi kwa mchezaji kama kuvaa jezi nyeupe za Real Madrid,” alisisitiza Zidane ambaye kwa sasa yuko na kikosi cha Madrid nchini hapa, kwa ajili ya mechi dhidi ya LA Galaxy.
Klabu 10 zasusia uchaguzi SLFA
KLABU 10 miongoni mwa 14 za Ligi Kuu ya soka ya nchini hapa, zimegomea ligi hiyo kupinga kitendo cha Mohamed Kallon na wengine wanne kuchujwa kwenye mbio za uchaguzi wa Chama cha Soka (SLFA).
Tayari klabu hizo zimeandika barua ya kutoshiriki ligi hiyo na kuikabidhi kwa Bodi ya Ligi Kuu kutohusishwa kwenye ratiba ya ligi hiyo iliyokuwa itolewe hivi karibuni kwamba Kallon na wenzake wamechujwa kimizengwe.
Kalabu hizo zilizogomea ligi hiyo ni Diamond Stars, Gem Stars, Kambui Eagles, Old Edwardians FC, FC Kallon, Bo Rangers, Ports Authority FC, Mighty Blackpool, Central Parade FC na Freetown City FC.
Wakati hizo zikigoma, nyingine nne zilikuwa tayari kuendelea na ligi hiyo iliyokuwa ianze Jumatatu ijayo kwa mechi kati ya Bo Rangers na Mighty Blackpool.
Kallon, nyota wa zamani wa Inter Milan ya Italia na AS Monaco ya Ufaransa, alichujwa kwenye mbio hizo kwa kile kilichoelezwa kutokidhi vigezo kwa mujibu wa Ibara ya 32 (4) ya Katiba ya SLFA.
Kipengele hicho kinataka mgombea katika uchaguzi huo awe ni mkazi wa Sierra Leone si chini ya miaka mitano, kigezo ambacho kinamtupa nje Kallon ambaye anasema ni siasa za soka.
Wagombea wengine waliochujwa kwa nafasi ya rais wa chama hicho ni Rodney Michael na Foday Turay ambao ni kutokana na kutokidhi matakwa ya katiba hiyo ibara ya 25, inayohusu maadili kwa upande wa shughuli za kamari.
Hata hivyo, wagombea hao wamepinga kuchujwa kwao kwa hoja kuwa imetafsiriwa isivyo na kamati iliyowachuja, hivyo wanataka majina yao yarejeshwe kwenye kipute hicho.
Mashabiki wa Kallon na Michael wameitisha maandamano ya amani kuelekea Ikulu mjini hapa Jumatatu kutaka wagombea hao warejeshwe katika uchaguzi huo wa Agosti 3.
Rais wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma, amekutana na  Kallon na wafuasi wake na kuahidi kulishughulikia suala hilo kwa masilahi ya soka ya nchini hapa.
Kallon, nahodha wa zamani wa timu ya taifa, Leone Stars, ameiambia BBC kuwa anaamini Rais Koroma atamaliza mgogoro huo.
Wengine waliochujwa katika uchaguzi huo katika nafasi nyingine ni Idrissa Taralley na John Dissa kutokana na kuhusika kwao na shughuli za uendeshaji wa kamari.
Uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Jumamosi chini ya Kamati ya Maridhiaano, ni baada ya kuahirishwa mara kadhaa kabla ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kuingilia kati Desemba mwaka jana.
Kuchujwa kwa Kallon na wengine kunatoa nafasi kwa mgombea, Isha Johansen, kushinda kirahisi nafasi ya urais kutokana na kukosa mpinzani.
Azam Tv yawachanganya Yanga
SAKATA la Klabu ya Yanga kugomea udhamini wa Azam Tv katika Ligi Kuu Tanzania bara, limezidi kupata nguvu baada ya viongozi wa matawi ya klabu hiyo kubariki msimamo huo wa uongozi.
Msimamo huo ulitolewa jana na viongozi wa matawi ya klabu hiyo jijini Dar es Salaam ambao walikutana kujadili suala hilo na kusema wanaunga mkono.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bakili Makele alisema viongozi wao (Yanga) wapo sahihi kujitoa kwenye udhamini huo na kusema wanapata shaka na uharaka ya Kamati ya Ligi katika suala hilo.
Bakili alisema licha ya kutowekwa kwa tenda ya suala hili ili kushindaniwa katika mazingira ya wazi, pia jambo hilo lingeachwa lishughulikiwe baada ya uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la soka la Tanzania (TFF).
Kutokana na dosari hizo, wanachama hao wamemsihi Rais wa TFF, Leodegar Chilla Tenga kuingilia kati na kusema wanahofia jambo hilo limeharakishwa kwa maslahi binafsi.
“Jamani tamko letu ni kwamba, tunaungana na viongozi wetu, kwani Yanga ndio kila kitu hapa nchini, Na Azam Tv, inataka kutuchanganya,” alisema Bakili.
Hata hiyo Makele alionekama kutoa kauli zenye mwelekeo wa wivu wa maendeleo kwa kusema kitendo cha Azam Tv kumiliki haki za Ligi Kuu, kutainufaisha klabu ya Azam.
“Jamani, kitendo cha Azam TV kumiliki haki za Ligi Kuu, kutaifanya timu yao izidi kupata kipato, hivyo ving’amuzi vyao tusinunue,” alisema Makele na kuikiwa na viongozi wenzake wa matawi ….Yanga Oyeeeee.
Mwandishi Wetu ilipomtafuta Katibu Mkuu wa klabu hiyo Laurance Mwalusako  ni kwanini walikubali jambo likiwa kwenye mchakato, alisema walijaribu bila mafanikio.
“Ni kweli kwenye vikao tulikuwepo, lakini hatukuafiki kabisa na ndio maana nikasubiri tulifikishe kwa kamati ya utendaji ili wafanye,” alisema Mwalusako.
Kauli hiyo ya Mwalusako imekuja kutokana na wadau kuhoji mantiki ya klabu hiyo kupinga suala hilo wakati Yanga iliwakislishwa na yeye Mwalusako na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga.
“Sisi tuliomba kuona mkataba kwanza, ili tujue haki na mambo katika mkataba huo,  lakini TFF ilikagoma kwa kusema yatosha kusomewa.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia kuhusu msimamo huo wa wanachama, alisema hawana muda kuzozana wanasubiri kufanyia kazi taarifa rasmi itakayofika kwao.
“Yanga ilikuwa na wajumbe wake katika mchakato mzima wa jambo hili, hivyo hatuoni tija kurumbana nao katika kipindi hiki. Kama kweli wamegomea, watuarifu rasmi kwa maandishi.
Uchaguzi Mkuu TFF utata mtupu
UWEZEKANO wa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufanyika ndani ya kipindi kilichotakiwa na Shirikisho la soka Tanzania (Fifa), ni mdogo, Tanzania Daima imebaini.
Wakati Fifa wakiagiza uchaguzi huo uwe umefanyika ifikapo Oktoba 30, lakini marekebisho ya katiba yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa Dharura Julai 13, yamekwama katika
Ofisi ya Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo.
Japo TFF imepanga uchaguzi huo ufanyika Septemba 29, lakini suala la Katiba hiyo kukwama kwa Msajili, kunatia shaka kama uchaguzi huo utafanyika kwa ulitakiwa na Fifa
Wakati kukiwa na ukimya huo, habari zilizoifikia Tanzania Daima, zinasema kukwama kwa Katiba hiyo katika ofisi ya Msajili, ni kutokana na dosari mbili kubwa zilizofanywa.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa, dosari ya kwanza ambayo imeifanya ofisi ya Msajili kusita kupitisha marekebisho hayo, ni staili iliyotumiwa na Mkutano Mkuu kuipitisha Katiba hiyo.
Kwamba, wakati Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Shirikisho hilo ikitaka marekebisho yapigiwe kura, kuna habari kuwa jambo hilo halikufanywa na wajumbe wa mkutano Mkuu.
Kwa mujibu wa kipengere hicho, ili marekebisho yawe halali, yapaswa kupata baraka ya zaidi ya asilimia 50 ya idadi ya Wajumbe katika mkutano huo.
“Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya TFF inatamka wazi ili marekebisho yaweze kuwa halali, yanapaswa kupata baraka ya asilimia 50 + 1 ya wajumbe walipo ukumbini. Katika uchaguzi ule wa Julai 13, hili halikufanyika, ilipitishwa kijumla tu,” kilidokeza chanzo chetu.
Habari zinasema, kwa vile jambo hilo halikufanyika katika upitishaji wa marekebisho hayo, Ofisi ya Msajili imejikuta kwenye wakati mgumu kuipitisha hadi kufikia jana, akihoji ilipitishwa kwa staili ipi kwani utaratibu ni wajumbe kupiga kura.
“Ili marekebisho yaweze kuwa halali, yanapaswa kuuungwa mkono na asilimia 50+ 1 ya idadi ya wajumbe waliohudhuria mkutano husika,” kinasomeka kifungu hicho cha tatu cha Ibara ya 30 ya Katiba ya shirikishi hilo.
Habari zinasema, japo Ofisi ya Msajili ingependa kuona mchakato wa uchaguzi huo unafanyika ndani ya kipindi kinachotakiwa na Fifa, lakini dosari hiyo imeifanya isite kuipitisha katiba hiyo haraka kama ilivyokuwa imetarajiwa.
Kinachotishia zaidi uchaguzi huo kufanyika kwa wakati, ni mchakato mzima kuhitaji muda wa siku zisizopungua 60 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, hivyo kama si rasimu hiyo kukwama kwa Msajili, mchakato huo ungepaswa uwe umeanza walau kuanzia leo.
Aidha, kitendo cha Kamati ya Utendaji kufanya uteuzi wa Kamati mbalimbali kwa mujibu wa marekebisho yaliyomo kwenye rasimu inayosubiri baraka za Msajili, ni dosari nyingine ambayo
pia imehojiwa na Ofisi ya Msajili.
“Ofisi ya Msajili imehoji pia uundwaji wa Kamati za Maadili umefanywa kwa katiba ipi? Inajiuliza hivi kwa sababu marekebisho yaliyofanywa bado hayajapata baraka kisheria,” kilisema chanzo hicho.
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Msajili, Mercy Rwezaura kupata kauli yake
juu ya madai hayo, alisema hawezi kusema lolote kwa vile ofisi yake bado inaendelea kuipitia.
“Kwa sasa siwezi kusema lolote kwa vile bado tunaendelea kuipitia,” alisema Msajili huyo.
Alipoulizwa juu ya madai kwamba dosari ndizo zimeifanya ofisi yake ishindwe kupitisha rasimu hiyo kwa wakati, alisema hana taarifa yoyote na kusisitiza  wanaendelea kuipitia rasimu ya katiba hiyo.
Tanzania Daima lilimtafuta Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kujua mustakabali mzima wa katiba na mchakato wa uchaguzi huo kwa ujumla, alisema bado wanasubiri majibu kutoka kwa msajili kabla ya mengine kuendelea.
Kuhusu madai ya dosari ya akidi, Osiah alisema wakati wa kukabibidhi marekebisho hayo kwa Msajili, waliambatanisha na muhtasari wa mkutano huo ambao unaonesha kila kitu kilichofanywa na wajumbe wa Mkutano Mkuu.
“Katika katiba tuliyoipeleka kwa Msajili, tuliambatanisha muhtasari ya wajumbe walioshiriki, sasa sijui idadi ipi inayohojiwa,” alisema
Kuhusu uteuzi wa Kamati mbili mpya za Maadili, Osiah alisema kwa mujibu wa katiba hiyo hiyo ya TFF, mabadiliko yaliyopitishwa huanza kutumika mara moja hata kabla ya kupitishwa na Msajili.
Awali, uchaguzi wa Shirikisho hilo ulipangwa kufanyika Februari 24, mwaka huu, lakini ukaota mbawa baada ya Shirikisho la Soka kutaka iwe hivyo kutokana na baadhi ya wagombea kulalamika kuchujwa isivyo halali.
Baada ya Fifa kumtuma mjumbe wake, Primo Carvaro kuja nchini na kupeleka ripoti, ndipo Shirikisho hilo lilipoagiza uundwaji wa Kamati mbili za Maadili na kutaka uchaguzi uwe umefanyika hadi ifikapo Oktoba 30.
Hata hivyo, habari zinasema pamoja na dosari hizo, Ofisi ya Msajili yaweza
kuipitisha katiba hiyo kwa sharti la dosari hiyo kifanyiwe kazi katika Mkutano
Mkuu wa Uchaguzi kama ilivyokuwa uchaguzi wa Desemba 27, 2004.