Ibrahimovic amponda Pep Guardiola, ampa tano Jose Mourinho
ZLATAN Ibrahimovic amesema alikuwa tayari kufa kwa ajili ya kocha Jose Mourinho kuliko Pep Guardiola ambaye kwake anaamini hakuwa lolote bali mwoga.
Ibrahimovic aliyecheza akiwa chini ya Mourinho katika klabu ya Inter Milan amesema kuwa alileta msukumo kutokana na aina yake ya ufundishaji na uwezo wake kitaalam.
"Mourinho alikuwa kocha bora ambaye alinifanya niwe tayari kufa kwa ajili yake," hayo aliandika kwenye mtandao unaoelezea maisha yake binafsi na baadaye kuripotiwa na mtandao wa Daily Mail.
"Alikuwa akifanya kazi mara mbili zaidi ya mapumziko yake. Maisha yake kwa asilimia kubwa ilikuwa ni soka. Sijawahi kuonana na kocha wa aina hiyo mwenye maarifa ya kutatua tatizo. Kwani ana kila kitu.
"Nilipokutana naye na kumchunguza niligundua kuwa ni jasiri na alinishtua. Kwani amekuwa akijishusha kwa wachezaji, nikadhani ni kwa mara ya kwanza lakini hali hiyo niliendelea kuishuhudia kila mara kwake.
"Mourinho ni bingwa wa kuunda mahusiano binafsi na wachezaji kwa kutumia maneno yake yaliyokuwa yakijenga."
Ibrahimovic alikwenda Barcelona kutafuta fungu kubwa mwaka 2009 lakini alikaa kwa muda wa mwaka mmoja Camp Nou na kujikuta akimlalamikia kocha Guardiola kuwa na matatizo.
Akikumbuka tukio moja lililomuudhi la Barca kupoteza kwa klabu aliyokuwa akiifundisha Mourinho ya Inter kwenye nusu fainali ya kombe la UEFA alisikia uchungu na kujikuta akimpigia kelele kocha wake akisema "Nimepoteza mchezo huu, kwa sababu yako lakini kocha hakusema kitu hivyo nikagundua kocha huyu ni mwoga."
Ibrahimovic alisema kuwa alikuwa akishangaa namna ambavyo Barcelona ilikuwa na wachezaji wazuri lakini wakijikuta wanafungwa kijinga hali aliyoiona ilichangiwa na mahusiano mabovu kati yao na Guardiola.
Mchezaji huyo ambaye kwa sasa anakipiga Paris St Germain, anaeleza kuwa "kwa kocha huyo hawezi kufanya jambo kubwa lolote na watajikuta inarudi kuwa ndogo na kuwa kama ilivyokuwaAjax hapo nyuma.
"Nimeamua kujitoa hapo si kwa sababu ya pesa pekee bali pia kugombana na kocha huyu ambayo ilikuwa sababu kubwa.
Alisema "Guardiola aliamua kunitoa kafara, na hiyo ni kweli na hata baadhi ya wachezaji wenzangu walinieleza kwamba 'Zlatan, suala lako ni sawa na Barca kununua Ferrari na wanaiendesha kama Fiat,' kwani Guardiola alinitumia kama mchezaji wa hali ya chini wakati nilikuwa mkubwa pengine kuliko timu yake yote.
Anaongeza kuwa "Ilifika wakati nikimsalimia hajibu kitu. Alikuwa akiogopa kunitazama. Nilipokuwa nikiingia ndani, nikimkuta yeye alikuwa akitoka. Hali iliyonifanya nijiulize kipi kinaendelea,' nikajiuliza je kuna jambo nililolifanya ambalo haliko sawa? Au kuna nililolifanya lisilo sawa? Jambo hilo lilikuwa likiniumiza kichwa na kunifanya kushindwa kulala.
"Sikuwa namfikiria kocha huyo bali nilikosa usingizi kwa ajili ya kuangalia maendeleo yangu. Nilikuwa namchukia.
"kwa sababu ya matatizo yangu na Guardiola ilisababisha hata klabu kulazimisha kuuzwa kwangu. Kwani nilikuwa nimeifunga bao 22 klabu hiyo.