Ozil: Sikuthaminiwa Santiago Bernabeu
MCHEZAJI Mesut Ozil, amekana kauli ya Rais wa Klabu ya Real Madrid, Florentino Perez, kwamba ameondoka kutokana na kukosa vigezo za nyota wa kimataifa.
Mbali ya kukana hilo, Ozil amesema kilichomwondoa ni kukerwa na kutopewa heshima yake Real Madrid licha ya kuwa katika kiwango bora kiuchezaji.
Ozil ameyasema hayo wakati baba yake mzazi akiwa kwenye harakati za kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Perez kwa kauli yake dhidi ya mwanaye.
Kwa mujibu wa Peres, Ozil alikuwa akitumia muda mwingi kujirusha na wasichana na kukesha kwenye baa.
Hata hivyo, nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani, hakupenda kuingia kwenye vita ya maneno na Perez, akiishia kusema aliondoka kutokana na kutothaminiwa.
"Sitaki kusema lolote baya dhidi ya Real Madrid kwa sababu miaka yangu mitatu pale ilikuwa ya mafanikio.
"Tulibeba mataji na niliisha kwa furaha, kila aliyenifahamu, alitambua mchango wangu kwa Real Madrid.
"Nikiwa pale nilicheza mechi 159, katika mazingira ya kawaida, huwezi kucheza mechi nyingi hivyo kama hupo katika kiwango bora.
"Tatizo sikupata heshima niliyostahili kulingana na mchango wangu. Nilikuwa kwenye mazingira magumu na nilipozungumza kwa simu na Kocha wa Arsenal (Arsene Wenger), alionesha kuniheshimu."
Ozil aliyewahi pia kukipiga Werder Bremen ya Ujerumani, anaamini kutua kwake Arsenal, kutaboresha zaidi kiwango chake.