Katika mechi hiyo, Simba walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi kali katika dakika ya 13, lakini nyota wake Vincent Barnabas, alishindwa kuipatia timu yake bao.
Dakika ya 18, Salim Abdallah wa Mtibwa Sugar alilimwa kadi ya njano na dakika ya 30, Shaaban Kisiga wa Mtibwa Sugar alishindwa kuitendea haki krosi ya Hassan Ramadhani aliyewalamba chenga mabeki wa Simba.
Dakika ya 40, Masoud Mohamed wa Mtibwa Sugar, alilimwa kadi ya njano kwa kucheza vibaya na hadi mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma anamaliza kipindi cha kwanza, kulikuwa hakuna bao.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa kila moja kutaka kupata bao na dakika ya 67, Simba walipata bao likifungwa na mtoke benchi, Henry Joseph Shindika aliyerejea Msimbazi msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake nchini Norway.
Shindika alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha pasi ya Haruna Chanongo iliyotokana na kona ndogo, hivyo kuongeza kasi ya mchezo huo.
Bao hilo lilifungwa wakati ambao Mtibwa Sugar wakionekana kucheza soka ya kutulia zaidi wakimpa wakati mgumu kipa Dhaira, aliyefanya kazi kubwa ya kuokoa michomo ya nyota wa Mtibwa Sugar, mabingwa mara mbili wa Ligi Kuu, mwaka 1999 na 2000.
Dakika ya 72, Dhaira alilimwa kadi ya njano kwa kupoteza muda kwa makusudi.
Dakika ya 90, Simba walipata bao la pili likiwekwa wavuni na mtokea benchi, Betram Mwombeki, ikiwa ni dakika tano tangu alimwe kadi ya njano kwa kumchezea vibaya beki wa Mtibwa Sugar chini ya kocha wake Mecky Maxime, nahodha wa zamani wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.
Matokeo hayo yameiwezesha Simba chini ya kocha wake Abdallah ‘King’ Kibadeni Mputa na Jamhuri Kihwelo Julio, wamefikisha point na Jamhuri Kihwelo Julio, wamefikisha pointi saba, wakishinda mechi mbili na sare moja.
Simba: Abel Dhaira, Nassor Masoud Chollo, Issa Rashid, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas
Mkude, Twaha Ibrahim, Said Hamis, Amis Tambwe, Amri Kiemba na Haruna Chanongo.
Mtibwa Mtibwa: Hussein Shariff, Hassan Ramadhan, Paul George, Dickson Mbeikya, Salim Abdalla, Shaban Nditi, Ally Shomari, Soud Mohamed, Juma Liuziog, Shaaban Kisiga na Vincent Branabas.
Jijini Mbeya, Mbeya City jana walivuna sare ya bao 1-1 dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga katika mechi kali ambayo mabingwa watetezi, Yanga, walifanya kazi ya ziada kuepuka kichapo.
Mbeya City walianza kufika langoni mwa Yanga dakika ya kwanza tu kwa shambulizi kali na Yanga wakijibu dakika ya tano.
Wenyeji walirejea mara ya pili kwenye lango la Yanga dakika ya sita, wakifanya mashambulizi mawili, lakini mabeki wa Yanga wakiongozwa na Nadir Harob Cannavaro, walifanya kazi kubwa.
Yanga walifanya shambulizi jingine dakika ya tisa baada ya Said Bahanuz kupata nafasi nzuri, hata hivyo shuti yake ikipaa juu ya lango la Mbeya City.
Dakika ya 11, shuti ya Steven Mazanda wa Mbeya City ilipaa juu ya lango la Yanga
na dakika ya 16, Mbeya City walipata kona baada ya Cannavaro kuutoa mpira nje.
Dakika ya 17, Mbeya City tena walifanya shambulizi kali, lakini Deus Kisika aliyekuwa mwiba kwa Yanga, alishindwa kuifunga kutokana na kazi kubwa ya mabeki wa Yanga.
Yanga walipata nafasi nzuri ya kuweza kufunga dakika ya 25, lakini Nizar Khalfan alishindwa na dakika ya 36, Mbeya City nao walikosa bao baada ya shuti ya Anton Matogoro kwenda nje.
Dakika ya 38, Deus Kisika na Steven Mazanda wa Mbeya City walionana vizuri, lakini tatizo likawa umaliziaji.
Dakika ya 44, Mbuyu Twite wa Yanga, alilimwa kadi ya njano kutokana na mchezo mbaya.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa cha ushindani mkali huku Mbeya City chini ya kocha wake Juma Mwambusi wakicheza soka murua na kutangulia kupata bao dakika ya 49, likifungwa kwa kichwa na Mwagano Yeya akiitendea haki pasi ya Hassan wasapili.
Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo huo kwa Yanga kuongeza nguvu zaidi, lakini Jerry Tegete akishindwa kufunga dakika za 63 na 66 kabla ya Mwagane Yeya wa Mbeya City naye kushindwa kuifungia timu yake dakika ya 67.
Dakika ya 70, Yanga walisawazisha bao likifungwa na Tegete, mtoto wa Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba wa Mwanza, John Tegete, akisawazisha makosa yake ya kushindwa kuzitumia nafasi mbili.
Licha ya timu hizo kupambana kupata bao la uongozi, milango bado iliendelea kuwa migumu huku wenyeji Mbeya City wakionesha uhai mkubwa kiasi cha kulifanya lango la Yanga liwe kwenye msukosuko mkubwa hadi filimbi ya mwisho.
Kwa matokeo hayo, Yanga wamefikisha pointi tano, baada ya kushinda mechi moja na sare mbili kama wenyeji wao Mbeya City, waliopanda msimu huu pamoja na Ashanti Utd ya Ilala na Rhino Rangers ya Tabora
Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, mayai matatu yaliokotwa katikati ya uwanja na Meneja wa Uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine, Modestus Mwaluka baada ya kupewa taarifa na waamuzi waliokuwa wakipasha.
Tukio jingine kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, ni gari iliyokuwa imebeba wachezaji wa Yanga, kupopolewa mawe wakati inaingia uwanjani hapo na mashabaki wanaodhaniwa ni Mbeya City huku dereva wake akipata jeraha.
Mbeya City: David Burhani, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Anton Matogoro, Yohana Morris, Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Deus Kisika, Yusuph Wilson/Alex Sett.
Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez,’ Mbuyu Twite. David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro,’ Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji,’ Nazar Khalfan, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Hussein Javu na Said Bahanuzi.
Nayo Ashanti United ya Ilala, imeendelea kuwa gunia la mazoezi kwenye ligi hiyo baada ya kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja
wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam. Ashant imecheza mechi tatu na kungwa zote.
Katika Uwanja wa Mlandizi, Kibaha, Pwani, Ruvu Shooting pia ya Pwani, walichanua kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande wenzao, Mgambo JKT ya Tanga.
Coastal Union ya Tanga nayo jana ilivuna pointi moja baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Prisons ya Mbeya katika Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Kutoka Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera, Kagera Sugar walivuna sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam huku bao la wenyeji likifungwa na Felix Themi Hamis Mcha akifunga kwa upande wa Azam.
Katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, JKT Oljoro walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, moja ya timu ngeni katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.