Saturday, August 17, 2013

Arsenal yalia, Liverpool kicheko

Arsenal yalia, Liverpool kicheko
Ujumbe kutoka kwa mashabiki haukuwa nyuma


MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England umeanza vibaya kwa timu ya Arsenal ambayo ikicheza nyumbani ilikubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Aston Villa.
Arsenal wakicheza mbele ya mashabiki 60,003, walionekana kushindwa kuhimili kishindo cha wageni Aston Villa, licha ya kutangulia kupata bao dakika ya sita likifungwa na Olivier Giroud.
Hata hivyo Aston Villa walicharuka na kusawazisha bao hilo dakika ya 22, likifungwa na Christian Benteke, hivyo kwenda mapumziko matokeo yakiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa cha mashambulizi kwa pande zote mbili na dakika ya 61, Benteke aliifungia bao la pili Aston Villa kabla ya Antonio Luna kufunga la tatu, hivyo kuondoka na ushindi wa mabao 3-1.
Katika mechi nyingine ya mapema, Liverpool wakicheza kwenye Uwanja wao wa Anfield, waliianza ligi kwa furaha baada ya kuvuna ushindi wa bao 1-0, likifungwa na Daniel Sturridge.
Nayo West Ham  United ilishinda 2-0 dhidi ya Cardiff na Sunderland ikichapwa bao 1-0 na Fulham huku Norwich City ikitoka sare ya 2-2 na Everton.
Aidha, timu ya West Bromwich Albion ikicheza nyumbani, ilianza msimu kwa kipigo cha bao 1-0m kutoka kwa Southampton.
 Ligi hiyo inayoshindanisha timu 20, itaendelea tena kesho kwa miamba ya ligi hiyo kuendelea kutupa karata za kwanza kwa wageni Crystal Palace kuwaalika Tottenham  huku Chelsea wakiwa wenyeji wa Hull City.
Manchesster City wao watasubiri hadi kesho kuwakaribisha Newcastle United.

Yanga yanyanyua Ngao kwa mbwembwe

Yanga yanyanyua Ngao kwa mbwembwe
BAO la dakika ya tatu likifungwa na kiungo Salum Telela, jana lilitosha kuipa Yanga ubingwa wa Ngao ya Jamii katika mechi kali iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kuukaribisha rasmi msimu mpya wa Ligi Kuu ya Bara itakayoanza Agosti 24.
Kuingia kwa bao hilo kuliongeza kasi ya mchezo kwa Azam kucheza kwa nguvu wakitaka kusawazisha huku Yanga nao wakitaka kuongeza la pili, hivyo kuwapo kwa kosa kosa kwa kila upande.
Azam ambao jana walishuka dimbani kwa mara ya kwanza tangu warejee nchini kutoka Afrika Kusini kupiga kambi ya wiki mbili tangu Agosti 3 hadi 13, wakicheza mechi nne za kirafiki, walionesha kiwango kizuri huku wakishangiliwa na mashabiki wa Simba.
Hata hivyo, Yanga watapaswa kujilaumu kushindwa kuondoka na ushindi mnono kutokana na wachezaji wake kushindwa kuzitumia nafasi walizopata, akiwamo Jeryson Tegete, Didier Kavumbagu na Haruna Niyonzima.
Dakika ya 30, Azam FC walipata nafasi nzuri ya kuweza kufunga bao la kusawazisha, lakini kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’, akafanya kazi kubwa ya kuokoa hatari hiyo.
Barthez aliumia hadi kutolewa nje akishindwa kuendelea na mchezo baada ya kugongana na John Bocco katika hekaheka langoni, hivyo nafasi yake kutwaliwa na Deogratius Munish ‘Dida’ aliyewahi kuidakia Azam FC.
Dakika ya 41, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alilimwa kadi ya njano na mwamuzi, Oden Mbaga, baada ya kumchezea rafu Bocco na dakika ya 45, Tegete alikosa bao kwa shuti kwenda nje sentimeta chache.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kucheza kwa nguvu huku Azam wakicheza rafu na katika dakika ya 52, David Mwantika, alilimwa kadi ya njano baada ya kumwangusha Kavumbagu.
Dakika ya 57, Yanga walipata nafasi nzuri baada ya Simon Msuva kutoa pande kwa Tegete ambaye alishindwa kufunga.
Dakika ya 62, Azam walipata nafasi ya kusawazisha bao hilo, lakini mpira wa kichwa uliopigwa na Bocco ulitolewa nje na kuwa kona ambayo ilipigwa na Hamis Mcha na kupanguliwa na kipa Dida wa Yanga.
Dakika ya 67, Kavumbagu alikosa bao baada ya shuti lake la ‘tick-tack’ kwenda nje kabla ya kukosa tena dakika mbili baadaye.
Dakika ya 70, Bocco aliumia baada ya kukumbana na Twite na kurejea dimbani baada ya matibabu, lakini akicheza kwa dakika tatu kabla ya kutolewa, safari hii akimpisha Gaudence Mwaikimba.
Dakika ya 79, kwa mara nyingine Kavumbagu alishindwa kuifungia Yanga bao baada ya shuti lake la kichwa kugonga mwamba, baada ya kupata pasi iliyotokana na mpira wa krosi ya David Luhende.
Katika kipindi hicho cha pili, Yanga walionekana kufunika zaidi, wakicheza watakavyo licha ya vijana wa Azam kupambana vilivyo kusawazisha bao na hadi filimbi ya mwisho, Yanga walitoka kifua mbele kwa bao 1-0.
Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuukaribisha vizuri msimu mpya, kwani wametwaa Ngao ya Jamii zikisalia siku saba tu kabla ya kuanza kwa mbio za Ligi Kuu, ambapo Yanga wakiwa mabingwa watetezi, wataanzia kwa Ashanti United ya Ilala.
YANGA: Ally Mustapher ‘Barthez,’/DIDA, Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondani/Mbuyu Twite, Athuman Idd ‘Chuji,’ Simon Msuva, Salum Telela, Jeryson Tegete, Didier Kavumbagu na Haruna Niyonzima.
AZAM: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Agrey Morris, Himid Mao, Kipre Tchetche, Salum Aboubakar, Kipre Balou, John Bocco/ Gaudence Mwaikimba na Hamis Mcha.