MGOMBEA urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amesema anatarajia kuzindua ilani yake ya Uchaguzi Mkuu Jumatano, kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, huku akiwataka wagombea wa nafasi tofauti kufanya kampeni za kistaarabu.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Malinzi alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa juhudi zao na umakini katika kusimamia mchakato wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 27.
“Nichukue fursa hii kuwatakia kila la kheri wagombea wote, niwatakie kampeni njema, kampeni zenye wingi wa baraka na fanaka tele, na nina imani tutafanya kampeni za kistaarabu zisizoonyesha hisia za ubaguzi wa dini, kabila, jinsia au ueneo,” alisisitiza Malinzi.