Thursday, August 1, 2013

Kalou atoa siri za Drogba
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea, Salomon Kalou, anayechezea Lille OSC ya hapa, amefichua kuwa Didier Drogba anataka kumalizia maisha ya soka katika Ligi Kuu ya Marekani (MLS) kwenye moja ya miji ya New York au Los Angeles.
Rafiki wa karibu wa Drogba na Kalou aliyekuwa akicheza naye Chelsea wamekiri kuwapo kwa mpango utakaofanikisha mkali huyo aliyeng’ara Stamford Bridge kwenda kumalizia maisha yake Amerika Kaskazini, ingawa alikataa mara kadhaa alipoitwa huko.
“Drogba anaipenda Amerika, daima amekuwa akienda kwa mapumziko na ni sehemu ambayo anafurahia kuwapo. Kwake yeye kufanya kazi huko litakuwa jambo la kuvutia sana. Nadhani ndio lengo lake, ni mahali anakopenda kumalizia soka,” amefichua Kalou.
“Hajaniambi moja kwa moja, lakini aliniambia kuwa kumalizia soka yake jijini New York au Los Angeles litakuwa jambo la kuvutia mno kwake. Najua kwamba hilo liko katika akili yake hivi sasa. Angependa kumalizia soka yake huko,” aliongeza Kalou.
Drogba ilikuwa karibu ajiunge na MLS miaka miwili iliyopita. Ilikuwa hivyo pia mwaka jana alipokataa kuhamia huko na kukubali kumfuata nyota mwenzake wa zamani, Nicolas Anelka, katika timu ya Shanghai Shenhua ya Ligi Kuu ya China kwa dau la euro mil. 18.
Kwa sasa Drogba anakipiga na klabu ya Galatasaray ya Uturuki, aliyojiunga nayo akitokea Shanghai, aliyoihama baada ya kushindwa kumlipa mshahara wake pamoja na Anelka.
Usajili wa Kaze wamuweka kazimoto kiporo
WAKATI beki mpya wa wa kimataifa wa Simba Gilbert Kaze aliyekuwa akicheza
Vital’ O ya  Burundi alitarajiwa kuwasili nchini jana jioni, uongozi wa Simba pamoja unatarajiwa kukutana na Shirikisho la soka Tanzania (TFF)  kwa ajili ya kumjadili kiungo wake Mwinyi Kazimoto. 
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema jana kwamba, kama mambo yatakwenda vema Kaze atasaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba katika michuano mbalimbali itakayoshiriki pamoja na Ligi Kuu Soka Tanzania Bara. 
“Tunashukuru kwamba nafasi ya beki wa Kati ambayo ilikuwa na mapungufu imepata wahusika hivyo, Kaze sasa ataungana na Mganda Joseph Owino ambaye pia ni mchezaji mpya tuliyemuongeza kwenye kikosi chetu. 
Akizungumzia suala la Kazimoto, Kamwaga alikiri kwamba wamepokea ofa kutoka timu ya moja ya Qatar lakini ni ofa ndogo sana ambayo hawawezi kuikubali kwani thamani yake haifikii ile waliyomuhamishia kutoka JKT Ruvu. 
Hata hivyo, Kamwaga alisema hawezi kuzungumzia kwa undani juu ya suala la Kazimoto kutokana na ukweli kwamba bado ana maswali ya kujibu Watanzania na klabu yake ya Simba kwa ujumla. 
“Suala la Kazimoto tumeliweka pembeni kwani tunatarajia kukaa na TFF kwa ajili ya kumjadili na baada ya hapo mambo mengine kuhusu yeye yatafuata,”alisema 
Ikumbukwe kuwa, Kazimoto alitimkia Qatar hivi karibuni baada ya kutoroka katika kambi ya timu ya Taifa siku ambayo ilikwaanza na Uganda ‘The Cranes’ katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika zinazoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).
Kazimoto aliyesajiliwa na Simba kutoka JKT Ruvu alikwenda kujaribiwa na klabu ya Al Markhiya Sc inayoshiriki Ligi daraja la kwanza ya huko na kufuzu na hivyo wakala wake, Mahmoud Abu Al Ght kuwasiliana na uongozi wa Simba kwa ajili ya ofa hiyo. 
Katika hatua nyingine, kiungo Mganda anayewaniwa na Simba Moses Oloya amekana kusaini mkataba wa kujiunga na mahasimu wao wa jadi, Yanga. 
Kamwaga alisema kwamba Oloya amezungumza kwa simu na Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage akisema anashangazwa na taaarifa hizo kwani kwa sasa anafanya mazungumzo na uongozi wa Simba na mambo yakienda vizuri atasaini mkataba. 
“Oloya amewataka wanachama wa Simba kutulia kwani anafafanya mazungumzo na uongozi wa Simba tu na akili yake ni kuichezea Simba iwapo mazungumzo hayo yatafikia muafaka,”alisema Kamwaga.
Serikali yakiri dosari Katiba TFF
Rais wa TFF, Leodegar Tenga
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo imekiri kwamba mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa Dharura Julai 13, una dosari na ndio maana imekwama kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tu tangu Gazeti Tanzania Daima liandike habari ya katiba hiyo kukwama kwa msajili kutokana na marekebisho kupitishwa pasipo kupigiwa kura kama ibara ya 30 (iii) inavyotaka pamoja.
Dosari nyingine ambayo ilielezwa awali iliyomfanya Msajili Mercy Rwezaura kusita kupisha marekebisho hayo, ni kitendo cha TFF kuunfa Kamati za Maadili kabla ya katiba hiyo kupata baraka rasmi za ofisi yake.
Akizungumza na Chanzo chetu cha habari kwa njia ya simu kutokea Jimboni kwake Mvomero, Morogoro, Naibu Waziri Amos Makala, alikiri kuarifiwa jambo hilo na Msajili kuwa  mchakato wa upitishaji marekebisho hayo una dosari kwa mujibu wa katiba.
“Ni kweli nimejulisha na ofisi ya Msajili kuwa kuna dosari, tena tunataka TFF wenyewe wawaeleze ukweli Watanzania  kwa sababu wakati mwingi serikali imekjuwa ikitupiwa lawama kwamba inataka kuharibu mambo,” alisema Makala.
Akifafanua zaidi, Makala alihoji inawezekana vipi marekebisho ya uundwaji wa Kamati za Maaadili kabla ya kupata baraka za Ofisi ya Msajili, wao TFF tayari wameshaunda Kamati husika na kutangaza wajumbe wake.
“Hivi inaingia akilini kweli, ninyi mmefanya mabadiliko ya katiba ili itambue uwezpo wa Kamati za Maadili na mmepeleka kwa Msajili ipate baraka, lakini kabla haijapita, ninyi mnaziunda kamati,” alihoji Makala.
Alipoulizwa juu ya hatma ya uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo ambao umetakiwa uwe umefanyika hadi kufikia Oktoba 30 mwaka huu, Waziri Makala alisema lolote litakalotokea mbelke ya safari, Serikali haipaswi kulaumiwa.
“Kuhusu ukomo wa muda ambao Fifa (Shirikisho la soka la Kimataifa) limetaka kwa kipindi fulani uchaguzi mkuu uwe umefanyika, sisi hilo tunawaachia TFF wenyewe waamue nini cha kufanya, sisi tunaangalia sheria na taratibu za nchi zinasema nini,” alisema.
Utata huo katika marekebisho ya Katiba yaliyofanywa kwa maelekezo ya Fifa, ni mwendelezo wa mchakato wa uchaguzi wa shirikisho hilo kuwa na dosari kwani
awali ulipangwa kufanyika Februari 24, lakini ukasimamishwa.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya soka, wanasema pamoja na mapungufu hayo,  katiba hiyo inaweza kupitishwa na Msajili, lakini kabla haijatumika kwenye uchaguzi, itapaswa kupata baraka za Mkutano Mkuu kisha kugongwa mhuri siku hiyo.
Neymar atabiriwa makubwa Barcelona
SIKU moja baada ya Neymar kuanza kwa sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kirafiki na Lechia Gdansk, kiungo wa FC Barcelona, Xavi Hernandez, amemtabiria neema, ustawi na mafanikio dimbani kwa Mbrazil huyo aliyesajiliwa kwa dau la dola milioni 75.
Xavi amesema ana imani kuwa nyota huyo aliyetua hapo akitokea Santos ya nyumbani kwao Brazil, atapata mafanikio akiwa Blaugrana, anakotarajiwa kubebwa na ushirikiano wake na Lionel Messi na nyota wengine Camp Nou.
“Neymar atafanya vitu tofauti akiwa Barca,” alisema Xavi, 33 na kuongeza: “Ana kasi ya ajabu na anafunga mabao. Kuwa na Messi, Neymar na wachezaji wengine wote ni uhakika wa kutusaidia kila mmoja kufanya kilicho bora mchezoni.
“Wachezaji bora na wakubwa hutoa ubora wao kwa wengine mchezoni. Naamini Neymar atakuwa bora zaidi akiwa pamoja na Messi na Messi atakuwa bora zaidi kwa kuwa tu pamoja na Neymar kikosini.
“Tutajaribu kadri tuwezavyo kumsaidia Neymar kukabiliana na changamoto mpya Camp Nou, kumfanya awe na furaha na kufikia ubora wake kama aliokuwa nao akiwa anacheza Brazil.”
Aidha, ingawa Real Madrid imeripotiwa kutenga kitita cha euro milioni 115 kufanikisha uhamisho wa Gareth Bale kutoka Tottenham kwenda Bernabeu, Xavi amedai kuwa yeye binafsi anajua mambo machache kumhusu winga huyo wa kimataifa wa Wales.
“Sijui kabisa kama Bale ana thamani hiyo wanayosema Madrid,” alibainisha Xavi na kuongeza: “Kusema ukweli ni kuwa sijawahi kumuona Bale akicheza angalau kwa dakika 90.”

Angali video ya Shabiki wa Yanga aliyelia wakati timu yake ilipofungwa mabao 5 na mtani wao Timu ya Simba, akimlamu Salama jabir baada ya kutolewa katika shindano la Epic Bongo Star Search (EBSS)