Klabu 10 zasusia uchaguzi SLFA
KLABU 10 miongoni mwa 14 za Ligi Kuu ya soka ya nchini hapa,
zimegomea ligi hiyo kupinga kitendo cha Mohamed Kallon na wengine wanne
kuchujwa kwenye mbio za uchaguzi wa Chama cha Soka (SLFA).
Tayari klabu hizo zimeandika barua ya kutoshiriki ligi hiyo
na kuikabidhi kwa Bodi ya Ligi Kuu kutohusishwa kwenye ratiba ya ligi hiyo
iliyokuwa itolewe hivi karibuni kwamba Kallon na wenzake wamechujwa kimizengwe.
Kalabu hizo zilizogomea ligi hiyo ni Diamond Stars, Gem
Stars, Kambui Eagles, Old Edwardians FC, FC Kallon, Bo Rangers, Ports Authority
FC, Mighty Blackpool, Central Parade FC na Freetown City FC.
Wakati hizo zikigoma, nyingine nne zilikuwa tayari kuendelea
na ligi hiyo iliyokuwa ianze Jumatatu ijayo kwa mechi kati ya Bo Rangers na
Mighty Blackpool.
Kallon, nyota wa zamani wa Inter Milan ya Italia na AS
Monaco ya Ufaransa, alichujwa kwenye mbio hizo kwa kile kilichoelezwa kutokidhi
vigezo kwa mujibu wa Ibara ya 32 (4) ya Katiba ya SLFA.
Kipengele hicho kinataka mgombea katika uchaguzi huo awe ni mkazi wa Sierra Leone si chini ya miaka mitano, kigezo
ambacho kinamtupa nje Kallon ambaye anasema ni siasa za soka.
Wagombea wengine waliochujwa kwa nafasi ya rais wa chama
hicho ni Rodney Michael na Foday Turay ambao ni kutokana na kutokidhi matakwa
ya katiba hiyo ibara ya 25, inayohusu maadili kwa upande wa shughuli za kamari.
Hata hivyo, wagombea hao wamepinga kuchujwa kwao kwa hoja
kuwa imetafsiriwa isivyo na kamati iliyowachuja, hivyo wanataka majina yao
yarejeshwe kwenye kipute hicho.
Mashabiki wa Kallon na Michael wameitisha maandamano ya
amani kuelekea Ikulu mjini hapa Jumatatu kutaka wagombea hao warejeshwe katika
uchaguzi huo wa Agosti 3.
Rais wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma, amekutana na Kallon na wafuasi wake na kuahidi
kulishughulikia suala hilo kwa masilahi ya soka ya nchini hapa.
Kallon, nahodha wa zamani wa timu ya taifa, Leone Stars,
ameiambia BBC kuwa anaamini Rais Koroma atamaliza mgogoro huo.
Wengine waliochujwa katika uchaguzi huo katika nafasi
nyingine ni Idrissa Taralley na John Dissa kutokana na kuhusika kwao na
shughuli za uendeshaji wa kamari.
Uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Jumamosi chini ya Kamati
ya Maridhiaano, ni baada ya kuahirishwa mara kadhaa kabla ya Shirikisho la Soka
la Kimataifa (Fifa), kuingilia kati Desemba mwaka jana.
Kuchujwa kwa Kallon na wengine kunatoa nafasi kwa mgombea,
Isha Johansen, kushinda kirahisi nafasi ya urais kutokana na kukosa mpinzani.
No comments:
Post a Comment