Mkude alifunga bao hilo kwa ustadi mkubwa kwa shuti ya nje ya 18 na kwenda moja kwa moja kwenye nyavu za maafande wa Tanzania Prisons, ukianzia mpira wa kona iliyopigwa na Edward Christopher.
Kabla ya bao hilo, Prisons walikianza kipindi cha kwanza kwa kasi wakicheza soka ya kujiamini wakipiga pasi nyingi za uhakika na kufanya mashambulizi kadhaa, hivyo kuwapa Simba wakati mgumu.
Dakika ya 34, Simba walimtoa Omary Salum na kumwingiza Haruna Shamte kwenda kuimarisha sehemu ya kiungo kukabiliana na presha ya vijana wa Tanzania Prisons, hivyo kwa kiasi fulani yaliwasaidia kuleta uhai.
Hata hivyo, pamoja na mashambulizi kadhaa kwa kila upande, hadi mwamuzi wa mechi hiyo Simon Mbelwa kutoka Pwani anamaliza dakika 45, kulikuwa hakuna timu iliyokuwa imepata bao.
Kipindi cha pili, vijana wa Simba chini ya kocha wake Abdallah King Kibadeni Mputa, walizidi kuonesha uhai zaidi huku maafande wa Tanzania Prisons nao wakicheza soka ya kuvutia kukiwepo kosa kosa kadhaa kwa kila lango.
Baada ya Simba kupata bao katika dakika ya 62, mechi hiyo ilionekana kuchangamka zaidi kutokana na maafande wa Prisons kucharuka wakitaka kusawazisha huku Simba nao wakipambana kuokoa hatari zote.
Dakika ya 67, Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Christopher aliyempisha Zahor Pazi, mabadiliko ambayo hata hivyo hayakuweza kubadili sana suara ya mchezo.
Dakika ya 89, Prisons nusura wapate bao kama si Peter Michael kupiga shuti hafifu licha ya kuunasa mpira uliokuwa umetemwa na kipa wa Simba, Abel Dhaira, nyoya wa kimataifa wa Uganda.
Hadi mwamuzi Mbelwa anamaliza mechi hiyo, Simba walitoka kifua mbele kwa bao hilo moja, hivyo kuendelea kuongoza ligi kwa pointi 18.
Simba: Abel Dhaira, Nassor Masoud Chollo, Omary Salum, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Abdulhalim Humud, Amis Tambwe, Edward Christopher na Haruna Chanongo.
Prisons: Beno David,Kimenya Mashaka, Raulian Mpalile, Nurdin Issa, Mwangama Lugano, Nimkaza Jumanne, Kwanga Julius, Jimmy Shoji, Peter Michael, Omega Semeni na Jeremiah Mgunda.
Katika mechi nyingine iliyochezwa Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga walivuna ushindi wa mabao 2-1 katika iliyokuwa na ushindani mkubwa.
Kwa ushindi huo Yanga wamefikisha pointi 15, hivyo kuendelea kuipumulia Simba kwa tofauti na pointi tatu huku kila moja ikiwa imecheza mechi nane tangu kuanza kwa msimu huu.
Baada ya mechi za jana, watani hao watakwenda mafichoni kujiandaa na mechi yao ya kukata na shoka itakayochezwa Oktoba 20, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa mechi ya vibonde Ashanti United ya Ilala kuikabili Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi,nje kidogo ya jijini Dar es Salaam.
Ashanti ikiwa inaburuza mkia kwa pointi zake mbili tangu kuanza kwa ligi hiyo Agosti 24, itakuwa ikipigania ushindi wa kwanza wakati Coastal Union yenye pointi 11, itakuwa ikisaka ushindi kuzidi kujiimarisha kwenye msimamo.
Nayo Ruvu Shooting ya Pwani yenye pointi 10, itakuwa mwenyeji wa Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Mabatini, Mkoani, Pwani huku Mgambo JKT ya Tanga ikiwa mwenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Azam iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 11, itakuwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kukwaruzana na JKT Ruvu ya Pwani yenye pointi 12 huku Mtibwa Sugar ikiwakaribisha JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.