Fabregas, Ronaldo na Rooney |
Fab, Rooney, Ronaldo wamtesa Moyes
MRITHI wa Sir Alex Ferguson, David Moyes, anapitia kipindi
kigumu katika timu ya Manchester United kutokana na kukabiliwa na vita ya
kumbakisha Wayne Rooney huku akiwatamani Cesc Fabregas wa Barcelona na
Cristiano Ronaldo wa Real Madrid.
Kocha huyo yuko katikati ya shinikizo kutoka kwa Chelsea,
Barcelona na Real Madrid kuwahusu nyota hao watatu.
Chelsea wameongeza presha kwa Moyes baada ya kusema wapo
tayari kumtwaa Rooney
kwa dau la pauni milioni 24 huku yeye akiboresha ofa ya
kumpata Fabregas hadi pauni milioni 30.
Wakati hajajua majaaliwa ya Rooney na ujio wa Fabregas Old
Trafford ukiota mbawa kutokana na kung’ang’aniwa na Barcelona na yeye kusema yu
tayari kubaki, Moyes amechanganyikiwa kwani hata Madrid wamesema hawana mpango
wa kumtoa Ronaldo.
Carlo Ancelotti wa Real Madrid, amemwaga dharau kwa Man
United juu ya mpango wao wa kumrejesha winga huyo wa Kireno Old Trafford,
akisema anawaza kusaini mkataba mpya Bernabeu.
Bosi wa Chelsea, Jose Mourinho amevuta kasi ya aina yake
katika jaribio la kumng’oa Rooney na kupandisha dau lake kutoka pauni milioni
20 mapema wiki jana hadi kufikia pauni milioni 24 licha ya Moyes kukana
kumuuza.
Kubwaga manyanga kuinoa Barca kulikofanywa na kocha
Vilanova, kunailazimisha miamba hiyo ya Nou Camp kuachana na wazo la kumuzaa
Fabregas, mshindi wa Kombe la Dunia, hadi itakapojua kocha mpya na mahitaji
yake kikosini.
Kutokana na kuyumba kwa jaribio la kumnasa Fabregas na
kumbakisha Rooney, maelezo ya Ancelotti kuhusu Ronaldo si habari nzuri kusomwa
au kusikiwa Moyes, ambaye alikuwa na matumaini makubwa akishirikiana na Fergie
kupata saini ya Mreno huyo.
Ancelotti aliyerithi mikoba ya Jose Mourinho aliyetimkia
Chelsea, alimmwagia sifa nyota wake huyo aliyedai kuwa anaweza kuwa msukumo kwa
nyota vijana klabuni Bernabeu.
Mtaliano huyo alisema: “Cristiano ni nyota wa daraja la juu.
Ni mchezaji mkubwa. Kwa klabu hii, jambo muhimu ni kuhesabu wachezaji wakali wa
kulipwa waliopo. Wachezaji vijana humuangalia bingwa katika kuhakikisha
wanafanya kama yeye.
“Sio jukumu langu linapokuja suala la kumpa mkataba mpya
kubaki hapa, lakini sidhani kama kunaweza kuwa na tatizo lolote katika hilo,”
alimaliza kocha huyo aliyeipa ubingwa wa Ligue 1 klabu ya PSG na kutimkia
Bernabeu.