Bale aipigia magoti Spurs
WINGA wa kimataifa wa Wales , Gareth Bale, amewaomba maofisa
wa klabu yake ya Tottenham kumruhusu ajiunge na klabu ya Real Madrid ya
Hispania.
Tamko la Bale limekuja saa chache baada ya
miamba hiyo ya soka ya Hispania kupandisha dau la ofa yake na kufikia ada
rekodi ya dunia ya pauni milioni 81, ambalo pia limeonekana kupuuzwa na Spurs.
Gazeti la Marca la nchini Hispania, ambalo liko
karibu mno na vyanzo vya ndani klabuni Santiago Bernabeu, limedai kuwa Bale aligeuka
mbogo kwa maofisa wa klabu yake kwa kuonesha dharau kwa donge nono.
Hasira za Bale zinatokana na Madrid kuonesha nia
ya dhati ya kupata saini yake, kwa dau linalovunja rekodi iliyowekwa na
Cristiano Ronaldo alipoihama Manchester United kujiunga na Madrid, Julai 2009.
Bale, 24, anaamini kuwa kunahitajika kukosa
uelewa kwa Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy na klabu yake kukataa dau kubwa
kama hilo kwa
ajili yake.
Gazeti la Marca limedai kuwa, Bale amevunja
ukimya na kumwambia Mwenyekiti wake Levy: “Kumbuka ulichoniahidi. Uliniahidi
kuwa kama Spurs haitofuzu michuano ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya na kisha kukaja ofa nzuri utakuwa tayari kuisikiliza.
“Naam, hatimaye ofa rekodi ya dunia imewasili na
kimsingi nataka kuichezea Real Madrid. Hivyo unapaswa kutoa ridhaa na kuingia
katika mazungumzo ya makubaliano,” amekaririwa Bale akimwambia mwenyekiti huyo
wa Spurs.
Bale alikutana na Levy na kuweka wazi kutoona
mwanga katika matarajio yake klabuni hapo na imetabiriwa kuwa dau nono zaidi ya
hapo linaweza kuvunjika mahusiano ya winga huyo na Bodi ya Spurs kama wataendelea kumbania.