Azam TV, TFF zasaini mkataba
HATIMAYE Kampuni ya Azam Media Limited na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wmesaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya sh. bil 5.6/- ili kuhodhi haki za matangazo ya Ligi Kuu Tanzania bara.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo mbele ya waandishi wa habari, Makamu wa Rais
wa TFF , Athuman Nyamlani alisema mkataba huo ni ukombozi kwa klabu za Ligi Kuu ambazo zitakuwa zikipata sh mil 100 kila msimu.
Nyamlani anayegombea nafasi ya Rais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 27, aliwapongeza Azam TV kwa mkataba huo mnono uliofungua fursa kwa klabu sio tu kushiriki vema Ligi Kuu kwa kila moja kupata fedha, pia utavutia wadhamini wengine katika ligi hiyo.
“Mkataba huu mnono kutoka Azam utafungua fursa kwa klabu zetu kushiriki vema katika Ligi pia itavutia wadhamini wengine kujitokeza,” alisema Nyamlani aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha soka Wilaya ya Temeke (Tefa) na Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).
Nyamlani alitumia fursa hiyo kuwasihi watanzania kutambua mafanikio ya kweli ya mchezo huo yanahitaji uwekezaji utakaowezesha klabu kuondokana na mfumo wa kutegemkea viingilio vya milangoni ambavyo havikidhi mahitaji halisi ya uendeshaji wa timu na klabu kwa ujumla.
“Watanzania wote na wapenda michezo wanapaswa kutambua soka haiwezi kunedeshwa kwa mapato ya milangoni, hii iko duniani kote tunaishukuru sana Azam,” alisema
Aliongeza anaamini udhamini huo utaongeza ushindani katika ligi kwa timu kumudu gharama za uendeshaji kama usafiri, malazi, posho za wachezaji na mambo mengine muhimu ambayo yalikuwa yakizisumbua klabu nyingi ambazo hazina udhamini binafsi.
Kuhusu urushwaji wa matangazo ya mechi za Ligi Kuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Azam, Rys Torrington amesema yataanza ndani ya wiki chache zijazo na kuahidi itakuwa TV yenye ubora wa kiwango cha kimataifa.
Kwa niaba ya Azam, Rys aliishukuru TFF kufikia hatua hiyo muhimu itakayosaidia kuitangaza soka ya Tanzania kimataifa na kuahidi itakuwa na mvuto wa aina yake ili kuwavuta mashabiki wa soka kupitia Azam TV.
Akifafanua zaidi, Rys alisema mbali ya mechi za Ligi Kuu, pia televisheni hiyo itakuwa ikirusha vipindi mbalimbali kama filamu, vipindi vya kijamii, michezo mbalimbali kama tenisi ngumi na mingine.
Juu ya msimamo wa Yanga kugomea mechi zao kutorushwa kwenye Azam TV, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema Azam na Yanga wako kwenye mazungumzo na anaamini watafikia muafaka kwa maslahi ya pande zote na soka kwa ujumla.