Wednesday, October 2, 2013

Rufani Kamati ya Maadili hitimisho ni leo

Rufani Kamati ya Maadili hitimisho ni leo
SIKU tatu za walalamikiwa waliofikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kukata rufaa zinafikia tamati leo, baada ya wahusika saba kupewa taarifa ya maandishi juzi.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Maadili, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura (pichani), alisema walalamikiwa wote ambao masuala yao ya kimaadili yalifikishwa kwa kamati hiyo, wamearifiwa kimaandishi na wanajua leo ndio mwisho wa kukata rufaa kama hawajaridhika.
Wambura, aliwataja walalamikiwa hao kuwa ni Kamwanga Tambwe, Nazarius Kilungeja, Omar Abdulkadir, Richard Rukambura, Riziki Majala, Shaffih Dauda na Wilfred Kidau.
Kwa mujibu wa kanuni za maadili, wale ambao hawakuridhika na uamuzi huo wa Kamati ya Maadili wanatakiwa kukata rufaa Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF, inayoongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema ndani ya siku tatu zinazomalizika leo.
Wambura aliongeza kuwa rufani kwa watakaoamua kufanya hivyo zinatakiwa ziwasilishwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 alasiri ya leo na baada ya hapo hazitapokelewa.
Kwa mujibu wa kanuni ya 74 (1) na (2) ya kanuni za maadili, rufani zote zikionyesha sababu za kupinga uamuzi wa kamati husika, zinatakiwa kuwasilishwa ndani ya siku tatu kwa njia ya posta kwa sekretarieti.
Aliongeza kuwa rufani hizo zinatakiwa kila moja kuambatanishwa na risiti ya malipo ya ada ya rufani, ambayo ni sh milioni moja.
Aidha Wambura aliongeza kuwa Kamati ya Uchaguzi imelazimika kufanya mabadiliko madogo katika ratiba zake za uchaguzi wa Bodi ya Ligi na ule wa TFF chaguzi zinazotarajiwa kufanyika mwezi huu.
Wambura alibainisha kuwa mabadiliko hayo yametokana na ombi la Kamati ya Maadili, iliyotumia muda mrefu kutolea uamuzi hukumu za kimaadili zilizofika mezani kwao, ingawa uchaguzi wa TPL bado utafanyika Oktoba 18, kisha wa TFF Oktoba 27.

Mshimshike Kombe la Mabingwa wa Ulaya

Mshimshike Kombe la Mabingwa wa Ulaya
Kocha wa Man United, David Moyes

PATASHIKA ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inaendelea tena usiku wa leo kwa miamba mingine 16 kushuka kwenye viwanja nane kupigania pointi tatu huku Manchester Utd wakiwa wageni wa Shakhtar Donetsk ya Ukraine katika kundi A.
Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Donbass Arena, ni ya kufa au kupona kwa Manchester United chini ya Kocha wake David Moyes anayekabiliwa na presha ya mwendo mbaya katika Ligi Kuu ya England.
Moyes anakwenda Ukraine akiwa na jeraha za kulimwa mabao 2-1 na West Bromwich katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa mwishoni mwa wiki, ikiwa ni kichapo cha tatu katika mechi nne zilizopita.
Kabla ya kipigo cha Jumamosi kutoka kwa West Bromwich Albion, Man Utd walikuwa wametoka kufungwa na Liverpool na Man City, hivyo timu hiyo kuambulia pointi saba katika mechi sita huku Arsenal ikiongoza kwa pointi 15.
Akijua presha na magumu yanayoikabili timu yake kwa sasa, Moyes amepanga kushusha kikosi cha uhakika kupata ushindi walau kuwashusha pumzi wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
“Tunapaswa kwenda pale na kikosi imara. Ni mechi ngumu kwa sababu Donetsk wana rekodi nzuri,” alisema Moyes mwishoni mwa wioki alipozungumzia mechi ya leo na kuongeza:
“Najua wameuza nyota kama wawili hivi, lakini wana Wabrazil kama watano au sita hivi, hivyo wana kikosi chenye vipaji mchanganyiko.
“Tulicheza vizuri dhidi ya Bayer Leverkusen, lakini sasa tunapaswa kufikiria mechi ijayo kwa sababu tunapaswa kushinda kila mechi ijayo kama tunataka kufikia mbali.
“Nafikiri historia ya timu hizo mbili inajulikana kote Ulaya; lakini Manchester United wanaponzwa na umaarufu wao,” alisema.
United ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya England, wanashuka dimbani leo wakitoka kushinda 4-2 katika mechi ya kwanza dhidi ya Bayer Leverkusen kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Wakati Man Utd wakitoka kuvuna ushindi huo, Shakhtar walishinda mabao 2-0 dhidi ya Real Sociedad.
Timu hizo zinakutana zikiwa na nyota wawili waliocheka na nyavu mara mbili katika mechi za kwanza ambapo kwa upande wa Man Utd, ni Wayne Rooney huku kiungo chipukizi Alex Teixeira akifanya hivyo kwa Shakhtar.
Uwepo wa nyota hao wawili kunaongeza mvuto wa mechi hiyo ya kundi A, japo United wana rekodi nzuri zaidi dhidi ya Shakhtar wakishinda mara tatu katika mechi nne.
Kati ya nyota wa kutumainiwa na Shaktar ni nyota wa Kibrazil, Bernard, Douglas Costa, Fernando Lucas Martins, Frederico Rodrigues Santos, Luiz Adriano na Taison.
Bernard aliyewahi kuwindwa na klabu za Arsenal na FC Porto, amecheza mechi tani, zikiwemo mbili alizopangwa kikosi cha kwanza katika msimu huu wa 2013/14.
Mechi nyingine leo katika kundi hili ni Bayer Leverkusen ya Ujerumani dhidi ya Real Sociedad huku kila moja ikitaka kushinda kupoza maumivu baada ya kuangukia pua katika mechi za kwanza.
Vita kama hiyo itakuwa katika kundi B, kwa Real Madrid kuwakaribisha FC Kobenhavn Uwanja wa Santiago Bernabeu huku Juventus ya Italia wakikwaana na Galatasaray ya Uturuki.
Wakati Real Madrid chini ya kocha wake Carlo Ancelotti wanashuka dimbani wakitoka kuwafunga Galatasaray ya Uturuki, Kobenhavn wana pointi moja waliyovuna kwa Juventus katika mechi ya kwanza.
Katika kundi C, PSG ya Uholanzi leo watakuwa nyumbani kuwakabili Benfica ya Ureno huku Anderlecht wakiwakaribisha Olympiakos ya Ugiriki katika mechi zinazotarajiwa kuwa zenye ushindani mkali.
Wakati PSG wakitaka kushinda kuendeleza wimbi la ushindi hivyo kuendelea kuongoza kundi, Benfica nayo watakuwa wakililia rekodi hiyo baada ya kushinda mechi iliyopita.
Katika kundi D, Bayern Munich ya Ujerumani chini ya kocha wake Pep Guardiola wenye pointi tatu, usiku wa leo watakuwa mjini London, England kukwaana na Manchester City.
Ni mechi inayoatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kwani timu zote mbili zinakutana zikiwa na pointi tatu walizovuna kwenye mechi zilizopita huku CSKA Moscow wakiwa wenyeji wa Viktoria Plzen zikiwa hazina pointi.
Matokokeo ya mechi zilizochezwa jana ni haya hapa.

MATOKEA KATIKA KILA KUNDI

KUNDI G
  • Zenit
    0 - 0
    Austria Vienna
  • FC Porto
    1 - 2
    A Madrid

KUNDI H
  • Celtic
    0 - 1
    Barcelona


  • Ajax
    1 - 1
    AC Milan
KUNDI E
  • Basel
    0 - 1
    Schalke
  • S Bucuresti
    0 - 4
    Chelsea
KUNDI F
  • B Dortmund
    3 - 0
    Marseille
  • Arsenal
    2 - 0
    Napoli