Yanga yafungua msimu kwa
mbwembwe, Simba manjanga
Kikosi cha Yanga kikiwa katika pozi la pamoja |
Wachezaji wa Yanga wakipongeza baada ya ushindi wa mabao 5-1. (Picha zote kwa hisani ya HABARI MSETO BLOG) |
YANGA, jana iliuanza kwa kishindo msimu mpya kwa kuwatandika Ashanti United ya Ilala mabao 5-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Slaam huku Simba akivuna sare ya 2-2 na Rhino ya Tabora, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Vijana wa Ernie Brandts, walipata bao la kwanza dakika ya 11, likifungwa na Jerry Tegete akimchambua kipa wa Ashanti United kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Simon Msuva
aliyetoa pasi kwa mfungaji.
Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo kwa Yanga kutaka kuongeza huku Ashanti United chini ya Kocha wake Mbaraka Hassan ikipambana vilivyo kusawazisha, lakini hadi mapumziko mabingwa watetezi, Yanga walikuwa mbele kwa bao hilo moja.
Ndani ya dakika hizo 45 za kwanza, kama si wachezaji kadhaa wa Yanga kucheza kwa staili ya kuremba, wangeweza kwenda mapumziko wakiwa na mabao zaidi kutokana na kumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa.
Kikwazo cha mabao, kilikuwa ni nyota wa Yanga kushindwa kutumia vizuri nafasi kadhaa walizopata katika dakika ya 40 kwa Haruna Niyonzima licha ya kumchambua kipa Ibrahim Abdallah, akishindwa kufunga kutokana mbwembwe.
Dakika ya 44, Tegete naye alipata nafasi nzuri ya kuweza kufunga baada ya kumzidi mbinu kipa wa Ashanti Utd, lakini akishindwa kuukwamisha mpira katika nyavu huku wapinzani wao wakionekana kupambana na kucheza soka ya kuvutia wakiongozwa na Hussein Sued na Joseph Mahundu.
Tatizo la Asanti United ilikuwa kushindwa kumalizia kwani licha ya kufanya kazi nzuri ya kufika mara kwa mara katika lango la wapinzani wao kiasi cha kufanya kazi kuhimili kishindo cha wageni hao katika Ligi Kuu, mashuti yao yalishindwa kuzifikia nyavu za Yanga
Katika kipindi hicho cha kwanza, Yanga ilipata pigo baada ya Athumani Idd Chuji kuumia hadi kushindwa kuendelea huku nafasi yake ikitwaliwa na Frank Domayo.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mashambulizi makali na dakika ya 48, Msuva aliifungia bao la pili kwa shuti kali ya mbali na kumsihinda kipa wa Ashanti Utd, ambaye jana alifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo langoni mwake.
Dakika ya 58, Yanga ilipata bao la tatu, likifingwa na Tegete kwa krosi murua ya Msuva ambaye katika mechi ya jana alikuwa mwiba mkali kwa ngome ya Ashanti, ikiwa ni dakika mbili tu tangu beki Ramadhani Malima kufanya kazi kubwa ya kuzuia shuti ya Tegete isiguse nyavu.
Dakika ya 73, Niyonzima alifunga bao la nnne kwa kichwa akiunganisha mpira uliotokana na adhabu ya moja kwa moja uliyopigwa na Luhende na dakika ya 77, beki Emmanuel Kichiba wa Ashanti Utd alitolewa na mwamuzi Oden Mbaga kwa kumchezea vibaya Msuva.
Dakika ya 90, Ashanti United ilipata bao la kufutia machazi, likifungwa na Shaaban Juma kabla ya Nizar Khalfan kuifungia Yanga bao la tano katika dakika za majeruhi, hivyo kuanza ligi hiyo kwa kishindo cha mabao 5-1.
Katika mechi nyingine, Coastal Union ya Tanga, jana walianza vizuri kampeni yao kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Coastal Union, walipata bao la kwanza dakika ya 11, likifungwa na Abdi Banda kwa shuti kali ya umbali wa mita 45 kabla ya Cyprian Odula kufunga la pili dakika ya 34 na kudumu hadi filimbi ya mwisho.
Nayo JKT Ruvu ya Pwani chini ya Kocha wake Mbwana Makata, jana ilianza ligi kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga katika Uwanja wa Mkwakwani, jijini humo katika mechi nyingine ya ufunguzi wa ligi.
Mabao yake kufungwa na Bakari Kondo dakika za 80 baada ya kutokea piga-nikupige langoni mwa Mgambo kabla ya kufunga la pili dakika ya 83, akiwatoka mabeki.
Mbeya City ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya, ilitoka sare ya 0-0 na Kagera Sugar ya Kagera.
Rhino Rangers ya Tabora, jana ikionja Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, ilifanikiwa kuibana mbavu Simba kwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na kugawana pointi.
Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro, ikicheza kwenye Uwanja wake wa Manungu, ilitoka sare ya 1-1 na Azam FC, washindi wa pili wa msimu uliopita huku Ruvu Shooting ya Pwani chini ya kocha wake Charles Boniface Mkwasa, ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Mabatini, Kibaha, Pwani.