Kalou atoa siri za Drogba
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea, Salomon Kalou,
anayechezea Lille OSC ya hapa, amefichua kuwa Didier Drogba anataka kumalizia
maisha ya soka katika Ligi Kuu ya Marekani (MLS) kwenye moja ya miji ya New
York au Los Angeles.
Rafiki wa karibu wa Drogba na Kalou aliyekuwa akicheza naye
Chelsea wamekiri kuwapo kwa mpango utakaofanikisha mkali huyo aliyeng’ara
Stamford Bridge kwenda kumalizia maisha yake Amerika Kaskazini, ingawa alikataa
mara kadhaa alipoitwa huko.
“Drogba anaipenda Amerika, daima amekuwa akienda kwa
mapumziko na ni sehemu ambayo anafurahia kuwapo. Kwake yeye kufanya kazi huko
litakuwa jambo la kuvutia sana. Nadhani ndio lengo lake, ni mahali anakopenda
kumalizia soka,” amefichua Kalou.
“Hajaniambi moja kwa moja, lakini aliniambia kuwa kumalizia
soka yake jijini New York au Los Angeles litakuwa jambo la kuvutia mno kwake.
Najua kwamba hilo liko katika akili yake hivi sasa. Angependa kumalizia soka
yake huko,” aliongeza Kalou.
Drogba ilikuwa karibu ajiunge na MLS miaka miwili iliyopita.
Ilikuwa hivyo pia mwaka jana alipokataa kuhamia huko na kukubali kumfuata nyota
mwenzake wa zamani, Nicolas Anelka, katika timu ya Shanghai Shenhua ya Ligi Kuu
ya China kwa dau la euro mil. 18.
Kwa sasa Drogba anakipiga na klabu ya Galatasaray ya
Uturuki, aliyojiunga nayo akitokea Shanghai, aliyoihama baada ya kushindwa
kumlipa mshahara wake pamoja na Anelka.
No comments:
Post a Comment