Tuesday, July 23, 2013

Simba yamnyatia Owino
TIMU ya Simba imeanza mkakati wa kumrejesha beki wake wa zamani, George Owino anayekipiga URA ya Uganda ambayo ilikuwa nchini kwa mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu za Simba na Yanga.
Jumamosi iliyopita, URA waliifunga Simba mabao 2-0 katika Uwanja wa Taifa, jijiji Dar es Salaam kabla ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Yanga siku iliyofuata huku Owino akimudu vema safu ya ulinzi hadi kuwavutia Msimbazi kutakani kumrejesha.
Baada ya filimbi ya mwisho, Meneja wa Simba na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Pope, waliteta  na beki huyo wakitaka arejee Msimbazi huku kukiwa na habari kuwa jana alitarajiwa kusaini fomu kama dau lake la dola 35,000 za Marekani litaafikiwa.
Owino anatua Msimbazi ikiwa ni siku chache tangu nyota wanne wa kimataifa waliokuwa wakisaka namba katika timu hiyo chini ya Kocha Abdallah Kibadeni kuwachuja wanne waliokuwa wakipigania kusajiliwa kutokana na kutoridhishwa na viwango vyao.  
“Nashukuru viongozi wananihitaji baada ya kuvutiwa na kiwango changu…sina wasiwasi kabisa kama wakifikia fedha ninayotaka nitarudi Simba kwani ni timu ninayoipenda,” alisema Owino
Habari ambazo zilipatikana jana kutoka ndani ya klabu hiyo zilizisema nyota huyo pande hizo mbili zimeendelea kuzungumza kwani kiasi anachotaka ni kikubwa kulingana na uwezo wa Simba, wakitaka kumpatia dola 25,000.
“Kuna mvutano kidogo katika majadiliano yetu, lakini naamini watafikia muafaka kwani uongozi na Kocha Kibadeni wamemkubali,” kiliongeza chanzo hicho.
Simba pia imeachana na nyota wanne wa kigeni waliokuwa wakisaka namba huku ikisitisha mkataba wa miaka miwili na kiungo wake Mganda, Mussa Mudde kwa kutodhishwa na kiwango.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala alisema wameachana na nyota hao wanne waliokuwa wakisaka namba na Mude, isipokuwa kipa Abel Dhaira na Amissi Tambwe kutoka Burundi.
Aliwataja walioachwa ni Assumani Buyinza na Samuel Ssenkoomi (Uganda) na Felix Cuipo (DR Congo) na James Kun, raia wa Sudan Kusini ambao wameshindwa kumridhisha Kibadeni.
Mtawala alisema nyota hao wameshapewa na tiketi za kurudi makwao huku  uongozi ukiwa umemalizana na Mudde ambaye alikuwa na mkataba wa miaka miwili.
Kim ahofia saumu Stars
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzani, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema vijana wake wameiva kuwakabili Uganda kwenye mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayochezwa Jumamosi, jijini Kampala.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Kim amesema tangu kikosi chake kimeingia kambini Julai 14, wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mazoezi na wako tayari kwa mechi hiyo.
“Uganda ni timu bora kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Mechi itakuwa ngumu, tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo mikakati kwa ajili ya mechi hiyo, tunakwenda kuikamilisha Kampala,” alisema Kim.
Hata hivyo, Kim amesema licha ya mwitikio mzuri wa wachezaji kwenye mazoez,  lakini wanakabiliwa na changamoto ya wengi wao kuwa wamefunga wakati wachezaji wanapokuwa kambini wanatakiwa kula, kunywa na kupumzika.
“Hiki ni kipindi kigumu kisoka, suala la kufunga ni la kiimani ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji kufunga. Karibu nusu ya wachezaji wanafunga, hii ni changamoto ambayo tunaiheshimu,” amesema Kim na kuongeza ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa na mabadiliko baada ya beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini Uholanzi.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaondoka Mwanza leo saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15 mchana.
Nyota waliomo kwenye msafara huo ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
Stars inakwenda Uganda ikiwa nyuma kwa bao 1-0 walilofungwa katika mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 13, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Julai 13; huku mshindi wa jumla baina yao atajitwalia tiketi ya kwenda Afrika Kusini kwa fainali za mwakani.
Safari ya Azam ‘Sauzi’ yaiva
SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) limebariki ziara ya Azam FC (pichani) nchini Afrika Kusini kujifua kwa wiki mbili kabla ya kurejea tayari kwa msimu mpya wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 24.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Idrisa Nassoro, Azam itakayoondoka Agosti 2, itacheza mechi tatu za kirafiki ambapo baada ya kurejea itacheza mechi ya Ngao ya Hisani Agosti 17, ikiwa ni ufunguzi wa msimu mpya. 
Nassoro alisema, maandalizi ya safari hiyo yamekamilika kwani wachezaji wote wapo tayari isipokuwa wachezaji wawili Brian Umonyi na Anfrey Mieno ambao watabaki kutokana na kuwa majeruhi.
“Kila kitu kimekamilika tumebakia kuondoka tu, TFF wana taarifa juu ya safari yetu. Umonyi anasumbuliwa na maumivu ya msuli huku Mieno akiwa na maumivu ya kifundo cha mguu,” alisema Nassoro.
Alisema kukawia kwa safari yao ilikuwa ni kusubiri uhakika wa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu pia baadhi ya nyota wao kuwemo kwenye kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars inayokabiliwa na mechi dhidi ya Uganda itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii mjini Kampala.
Akizungumzia ziara hiyo, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikiri kupata barua ya ziara ya Azam na kuwatakia kila la kheri katika ziara hiyo kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu.
Mbali ya Ligi Kuu ya Bara, Azam chini ya Kocha wake Stewart Hall, inakabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo licha ya kucheza mara ya kwanza, ilifika hadi raundi ya pili iking’olewa na FAR Rabat ya Morocco.  
Fabregas aitesa Man Utd

KAMA kuna kipindi ambacho Manchester United imewahi kuteseka katika usajili, basi ni sasa katika juhudi za kupata sahihi ya kiungo wa kimataifa wa Hispania, Cesc Fabregas ambapo kutokana na ugumu, imepanda hadi pauni mil 41.
United imepanda haki kiasi hicho baada ya ofa zake mbili ikiwemo ya hivi karibuni ya pauni milioni 35 kutupwa na Barcelona ikisema haina mpango wa kumuuza na Fabregas anapenda kubaki Camp Nou.
Mbali ya kiasi hicho, United pia ilikuwa tayari kumtoa mchezaji katika mpango huo ili kumpata Fabregas, lakini bado Barcelona wakatupa ofa hiyo hivyo kuikata maini Arsenal iliyokuwa ikimtaka kwa pauni mil 29.   
Ugumu wa Barcelona kumtoa Fabregas kwa United umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuondokewa na Thiago Alcantara aliyetimkia Bayern Munich ya Ujerumani akimfuata Kocha Pep Guardiola. 
Kuondoka kwa Thiago, kunatoa nafasi kubwa kwa Fabregas kupata namba kwenye kikosi cha kwanza kusaidiana na Xavi chini ya kocha mpya Gerardo 'Tata' Martino.
Hata hivyo, kutokana na United kutokuwa na uhakika wa ofa hiyo ya tatu kukubaliwa na Barcelona, wamepanga kumshawishi Fabregas kwa mshahara wa euro 233, 000 kwa wiki.
Moyes alisema juzi kuwa wameongeza dau hilo kutokana na mazingira magumu ya kumshawishi kiungo huyo kwenda Old Trafford ikiwemo shauku ya Barcelona kutaka abaki Camp Nou baada ya Thiago kuondoka huku kukiwepo presha kutoka klabu nyingine kama Arsenal.
Moyes alisema hilo ni jaribia la mwisho kwao katika kumwania nyota huyo anayewindwa vikali ikiwemo Arsenal aliyowahi kuichezea kwa mafanikio makubwa hadi kuwa nahadha wake, lakini mwaka 2011 akaondoka kurejea Barcelona alikocheza soka yake ya utoto.
"Hii ni ofa ya mwisho kwetu katika kushawishi Fabregas ajiunge nasi japo klabu yake Barcelona imekuwa ikiweka ngumu, lakini ofa yetu ya pili tuliituma siku ambayo Tito Vilanova alitangaza kuachia ngazi kutokana na sababu za kiafya,” alisema Moyes.
Nje ya Fabregas, United imekuwa ikisaka saini za nyota wengine kama Luka Modric, Yohan Cabaye na Marouane Fellaini kwa lengo la kuimarisha safu ya ushambuliaji na kiungo.
Kiasi cha pauni mil 41, ni dau la tatu kwa United katika harakati za kumpata Fabregas kwani ofa ya kwanza ilikuwa ni pauni mil 29 kama Arsenal kabla ya kupanda hadi 35. 
Fabregas alirejea Barcelona mwaka 2011 baada ya kucheza Arsenal kwa miaka nane, lakini amekuwa hana uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza Camp Nou, akicheza mara 32 na kufunga mabao 11 na kuchangia 11.
Cameroon yafutiwa kibano
SHIRIKISHO la soka la Kimataifa (Fifa) imekiondolea kifungo chama cha soka cha Cameroon
(FECAFOOT) baada ya matakwa yake ya kutaka kuundwa Kamati ya Mpito kuelekea uchaguzi mkuu, kutekelezwa.
Julai 4, mwaka huu, Fifa walisimamisha uanachama wa Cameroon baada ya serikali ya nchi hiyo kuingilia uendeshaji wa soka wa Fecafoot, hivyo ikaagiza kuundwe Kamati kwa sharti kuwa atakayekuwemo huko asiwe na ndoto ya kugombea uchaguzi ujao.
Chini ya kifungo hicho, Caneroon iliondolewa kwenye kampeni ya kupigania tiketi ya Kombe
la Dunia nchini Brazil ambapo Septemba itacheza na Libya kuwania hatua ya 10 bora itakayotoa tano za kwenda Brazil mwakani.
Cameroon ndio kinara wa kundi I, ikiwa na pointi 10 ikifuatiwa na Libya yenye pointi tisa huku DR Congo ikiwa ya tatu kwa pointi sita na Togo ya mwisho kwa pointi moja iliyovuna katika mechi tano.
Kwa msinamo wa kundi hilo, mechi baina ya Cameroon na Libya ndio itaamua timu ya kutinga hatua ya 1o bora ingawa Cameroon itakuwa ikihitaji walau sare tu kusonga mbele wakati Libya ikihitaji ushindi.
Juzi, Fifa ilitoa taarifa kuwa imeridhia na utekelezwaji wa maagizo yake kwa FECAFOOT, hivyo inaondoa kifungo na kuwataka kuendelea na mchakato zaidi wa kuelekea kwenye uchaguzi chini ya vyomvyo husika wakiwemo Fifa (Primo Cavaro) na Shirikisho la soka Afrika (CAF).
Mgogoro wa soka ulitokana na Rais wa FECAFOOT Iya Mohammed kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni licha ya kuzuiwa kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.
Cameroon ilipata nguvu baada ya kupewa pointi tatu za Togo kwa kosa la kumchezesha Alaixys Romao ambaye si raia katika mechi ya Juni 9.
Licha ya Cameroon kufungwa 3-0, wamepewa ushindi hivyo wana pointi 0, hivyo kuhitaji walau pointi moja kutinga hatua ya 10 bora.
Kivuli cha Ferguson chamtesa Moyes
KOCHA David Moyes aliyeziba nafasi ya Sir Alex Ferguson tangu miezi miwili iliyopita baada ya kuinoa timu hiyo kwa miaka 27, anakabiliwa na kibarua kigumu cha kujenga heshima yake ndani ya Old Trafford.
Kibarua kwake ni kuyalinda kwa kuyaendeleza mafanikio makubwa ya timu hiyo yaliyopatikana chini ya Ferguson (71) ambaye ameondoka baada ya kuipa mataji lukuki yakiwamo 13 ya Ligi Kuu, mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Klabu Bingwa ya Dunia na mengine ya ndani. 
Ferguson kwa upande wake anaamini Moyes ni mtu sahihi atakayeweza kulinda heshima ya klabu hiyo na kuwataka wapenzi kumpa sapoti katika jukumu hilo akitokea Everton alikodumu kwa miaka 11.
Moyes yeye anajiamini kuwa ni mtu sahihi wa kuziba nafasi hiyo akisema hizi ni zama zake, hivyo ni jukumu lake kuiwezesha timu hiyo kuanza kuandika historia mpya chini yake.
"Hizi ni zama zangu," alisema. Nimechukua nafasi na nipo kazini. Ni wakati wangu wa kuweka historia.
"Tangu siku ya kwanza nilipokuja hapa, nilisema nitamtumia Ferguson kwa vile ni mtu menye maarifa mengi.
"Lakini, ukweli ni kuwa bado jukumu hili sasa ni langu, ninapaswa kulibeba. Unapofikiria mafanikio ya Sir. Matt Busby na Sir Alex Ferguson katika historia ya klabu hii, nina kazi kubwa ya kufanya.
"Ni jukumu langu sasa kuhakikisha nami ninajenga historia yangu katika klabu hii kwani hicho ndocho kinasubiriwa kwa hamu na wapenzi wa klabu hii kote duniani.
"Siweze tena kumtegemea Sir Alex kwa kila jambo, ingawa nitabaki kuyaheshimu mafanikio yake (Ferguson).  
"Nitabaki kumheshimu Ferguson kama Manchester United ambavyo wamekuwa wakifanya mara zote."
Hata hivyo, Moyes amekiri kuwa angependa kupata mafanikio kama ya hao watangulizi wake japo anajimini katika kazi yake kwamba ni mtu sahihi katika nafasi hiyo ndani ya Manchester United.
Kipimo cha awali kwa Moyes, ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 17 kwa kuwafuata Swansea City kabla ya kuzivaa Chelsea, Liverpool, Crystal Palace na jirani zao Manchester City.
Kwa upande mwengine Man United leo imepewa kichapo cha goli 3-2 kutoka kwa Yokohama F Marinos ya Japan.Katika mechi hiyo mabao ya Yokohama F Marinos yametiwa kambani na M MARQUINHOS, F AGUIAR,Y FUJITA, huku United wakijipatia mabao yao kutoka kwa LINDARD na lengine TASHIRO ambaye ni mchezaji wa Yokohama aliyejifunga.
Shinji Kagawa (kulia) akiwa kwenye hekaheka uwanjani.
Martino amrithi Vilanova Barca
Gerardo Martino
KOCHA Gerardo Martino amepewa mkataba wa miaka miwili kuinoa Barcelona akichukua nafasi ya Tito Vilanova aliyejiuzulu kwa sababu za kiafya.
Martino maarufu kama Tata, ametua Camp Nou kwa ushawishi mkubwa wa Mkurugenzi wa Michezo wa klabu hiyo, Andoni Zubizarreta aliyezungumza naye kabla ya jana kutangazwa rasmi.
Tata aliondoka Hispania tangu juzi kwenda Hispania kwa mazungumzo kabla ya kusaini mkataba kubeba mikoba ya Vilanova aliyejiuzulu Ijumaa iliyopita kujipa muda zaidi wa kupigania afya yake.
Vilanova aliyekuwa amechukua nafasi ya Pep Guardiola mwaka mmoja uliopita, amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa ya koo ambapo mara kadhaa amekuwa akitibiwa na kupata nafuu ya muda.
Tata (50), atasaidiwa na kocha wa viungo, Elvio Paolorroso na Kocha Msaidizi, Jorge Pautasso, ametwaa nafasi hiyo akimpiku kiungo wa zamani wa timu hiyo, Luis Enrique aliyekuwa akitajwa.
Martino ni Muargentina wa nne kuinoa Barcelona, akitanguliwa na Helenio Herrera, Roque Olsen na Cesar Luis Menotti.
Nje ya ukocha, Enrique ataungana na Muargentina mwenzake, Lionel Messi nyota mahiri katika kikosi hicho ambacho kitaingia kwenye msimu mpya wa La Liga kama bingwa mtetezi.
Jumatatu hii Messi alizungumza na Tata aliyewahi kuinoa Newell na Paraguay na kaka yake Matias Messi na kumpongeza Martino kwa jukumu jipya Camp Nou.

"Karibu Tata!!" aliandika Messi kupitia Twitter. " Naamini utaendelea kupata mafanikio ukiwa hapa!! Asante Tito!! Mungu akubariki!!"