Wednesday, July 31, 2013

Zidane aingili kati usajili wa Bale
NGULI wa klabu ya Real Madrid, Mfaransa, Zinedine Zidane, ameingilia kati mchakato wa usajili tata unaobaniwa na Tottenham na kuiambia klabu hiyo: Mwacheni Gareth Bale azungumze nasi, vinginevyo hatapata tena nafasi nyingine ya kufanya hivyo.
Zidane, mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ufaransa, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Michezo klabuni Bernabeu, alisema: “Kama yeye ameonesha kuvutiwa kujiunga Madrid, basi Tottenham inapaswa kumruhusu kuzungumza nasi.
“Nafasi ya kuichezea klabu ya Real Madrid inakuja mara moja tu katika mzunguko wa maisha ya mchezaji yeyote yule. Na inaeleweka wazi kuwa Bale hataki kuipoteza nafasi hiyo ya kushindwa kujiunga nasi,” alisema Zidane maaarufu kama Zizzou.
Bale, 24, winga wa kimataifa wa Wales, amebaki kuwa chaguo pekee linaloongoza klabuni Bernabeu, ambapo Madrid iko tayari sasa kuvunja rekodi ya dunia iliyoweka yenyewe kwa kukubali kulipa pauni milioni 95 kumng’oa Spurs.
Licha ya harakati hizo za Madrid kupandisha kila uchao dau la Bale, Tottenham chini ya Mwenyekiti wake, Daniel Levy, imeendelea kukataa kumruhusu nyota huyo kuhama, huku ikisisitiza kuwa winga huyo hauzwi kwa dau lolote.
Zidane, nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, ameongeza presha kwa Spurs kwa kumwambia Bale anapaswa kulazimisha kuvua jezi nyeupe za kikosi chake tayari kuvaa nyeupe zilizo maarufu zaidi za Madrid – mabingwa mara tisa wa soka Ulaya.
Zizzou aliongeza kuwa: “Inakuwa hali isiyo ya kawaida moyoni mwa mchezaji yeyote anapotambua kuwa anahitajiwa Real Madrid, ni kwamba lazima apate msisimko na hamasa kubwa kutokana na hilo.
“Hakuna kitu cha fahari zaidi kwa mchezaji kama kuvaa jezi nyeupe za Real Madrid,” alisisitiza Zidane ambaye kwa sasa yuko na kikosi cha Madrid nchini hapa, kwa ajili ya mechi dhidi ya LA Galaxy.

No comments:

Post a Comment