Thursday, August 15, 2013

Yanga TV kuonekana ndani ya Azam Media

Yanga TV kuonekana ndani ya Azam Media
HATIMAYE mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, wameamua kufuata nyayo za watani wao Simba, baada ya kukubali kuingia mkataba na Azam Media ili kurusha kipindi chao kitakachojulikana kama Yanga TV.
Awali, Yanga walikataa udhamini wa Azam TV kurusha mechi zao za Ligi Kuu Bara, kwa madai mbalimbali, ikiwamo kupinga dai la sh milioni 100, kabla ya juzi kulipeleka suala hilo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ambako lilijadiliwa na pande zinazovutana kufikia mwafaka.
Klabu nyingine za Ligi Kuu ikiwamo Simba, ziliafiki udhamini, ambapo mbali ya sh milioni 100 hizo za udhamini wa Ligi Kuu, Wekundu hao wa Msimbazi, awali waliingia mkataba wa sh milioni 300 na Azam Media kurusha vipindi vyao vikijulikana kama Simba TV.
Habari zilizoifikia zinasema kuwa Yanga na Azam Media, walianza vikao juzi na kuzungumza mambo mengi likiwamo la kipindi chao cha TV kurushwa Azam TV, ili waweze kuwa tofauti na timu nyingine, kutokana na ukubwa wa jina na idadi kubwa ya mashabiki.
“Baada ya kukutana na Naibu Waziri, Yanga na Azam Media walikaa na kuanza mazungumzo na wamefikia pazuri, ambapo na wao watapewa udhamini kama waliopewa Simba wa sh milioni 300 kuonesha kipindi chao katika Azam TV,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake, kwa kuwa bado pande hizo zinaendelea na mazungumzo, japokuwa wamefikia pazuri.
Aidha, chanzo chetu cha habari kiliwasaka viongozi wa pande hizo, Azam TV, Said Mohamed na Yanga, Clement Sanga, ambao walikuwapo juzi katika kikao na wizara.
Mohamed alisema bado wanaendelea kuzungumza na mara baada ya kufikia mwafaka wataweka wazi suala hilo kuanzia leo huku Sanga simu yake ya kiganjani ikiwa haipatikani.

Surez aamua kubaki Liverpool

Surez aamua kubaki Liverpool
HATIMAYE nyota wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez ametamka bayana kuwa ameamua kubaki Liverpool kutokana na mpango wake kutaka kuondoka kugubikwa na mizengwe ikiwemo kubaniwa na klabu yake ya Liverpool inayotaka abaki.
Licha ya shauku ya nyota huyo kutaka kuondoka kutokana na kuandamwa na vyombo vya habari vya England kiasi cha kutamani kuondoka Anfield na kwenda Arsenal, amesema sasa atabaki hapo kwani Liverpool imegoma kumwachia.
Mbali ya kuandamwa na vyombo vya habari, pia Suarez alikuwa na hamu ya kutua Arsenal akitamani kucheza Ligi ya Mabingwa huku wakali hao wa Emirates wakiwa tayari kutoa pauni mil 42, Liverpoo wakatupa ofa hiyo.
Nyota huyo aliyetua Liverpool misimu kadhaa kutoka Ajax, amesema anabaki Anfield kutokana na kupendwa na mashabiki wa timu hiyo
Akizungumza na gazeti la El Observador la nchini kwao Uruguay, Suarez alisema: "Kwa sasa nimeamua kubaki kutokana na upendo wa mashabiki," alisema.
Juzi, mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha GolTV, Martin Charquero, alikuwa wa kwanza kutangza kuwa nyota huyo alikuwa amemweleza kuwa atabaki Liverpool licha ya kutakiwa na Arsenal.
Habari hiyo ya mwandishi wa kituo hicho ilitanguliwa na ile ya nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard akisema Suarez hatahama japo kuna presha kubwa ya Arsenal kutaka ahamie Emirates.
"Luis Suarez amenihakikishia kuwa hataondoka Liverpool kutokana na ushawishi mkubwa wa mashabiki wa," alisema Mwandishi huyo kupitia akaunti yake ya twitter.
Uamuzi huo wa Suarez ni habari njema kwa Liverpool iliyokuwa ikihaha kumbakisha na mbaya zaidi pale nyota huyo alipotaka suala hilo lichukue mkondo wa kisheria kuangalia uwezekano wa kutimkia Arsenal.
Hata hivyo, Kocha wa Liverpool Brendan Rodgers, akamtaka Suarez aombe radhi kwa klabu na wachezaji wenzake kwa kauli hiyo, vinginevyo ataendelea kufanya mazoezi kivyake katika kipindi
hiki kuelekea msimu umpya wa Ligi Kuu.
Suarez abayetumikia adhabu ya mechi sita za Ligi Kuu kwa kosa la kumng’ata Branislav Ivanovic wa Chelsea mwishoni mwa msimu uliopita, alimaliza msimu huo akifunga mabao 23, hivyo kuwa nafasi ya pili kwa ufungaji.

Uchaguzi Mkuu TFF kupigwa Okt. 20

Uchaguzi Mkuu TFF kupigwa Okt. 20
Rais wa TFF, Leodegar Tenga
UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), sasa unatarajiwa kufanyika Oktoba 20, ukitanguliwa na ule wa Bodi ya Ligi (TPL Board), Oktoba 18, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mchakato kuelekea uchaguzi huo umepangwa kuanza kesho kwa wadau kuanza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Hamidu Mbwezeleni, alisema kuwa nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi wa Shirikisho ni Rais, Makamu wake na wajumbe 13 wa Kamati ya Utendaji, watakaowakilisha kanda tofauti, huku uchaguzi wa Bodi ya TPL ikiwa ni nafasi ya Mwenyekiti, Makamu na wajumbe wa bodi hiyo.
Akizungumzia mchakato huo uliosimamishwa awali na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Mbwezeleni alisisitiza kuwa wagombea wanapaswa kuzijua sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi huo, ambazo zinapatikana katika ‘Election Menu’ ya TFF, ili kujua miongozo na taratibu ili kuondoa malalamiko.
“Sababu za kuchelewa kwa uchaguzi huu ziko wazi, ni agizo la Fifa kutaka kuwapo kwa Kamati ya Maadili. Kamati iko tayari, imekuja wakati mwafaka ambao taifa linaugua ugonjwa mbaya wa ukosefu wa uadilifu miongoni mwa viongozi,” alisema Mbwezeleni.
Alisema anaamini kamati yake ikishirikiana na ile ya Maadili, watafanikisha mchakato sahihi, huru na wa haki wa uchaguzi, huku akitoa angalizo kwa watakaojaribu kudanganya kwa kuwasilisha sifa bandia, kuwa wataingia kitanzini.
Alifafanua kuwa fomu kwa wagombea zitatolewa kuanzia kesho saa 3 asubuhi hadi saa 10:00 alasiri kwenye ofisi za TFF na mwisho wa kuchukua na kuzirudisha itakuwa Agosti 20.
Mbwezeleni, alitaja bei za fomu hizo kuwa ni sh 500,000 kwa nafasi ya Rais, sh 300,000 Makamu wa Rais na wajumbe sh 200,000.
Kwa Bodi ya Ligi Kuu, Mbwezeleni alisema Mwenyekiti ni sh 300,000, Makamu wake sh 200,000 na wajumbe sh 100,000, ambapo kwa wale waliolipia fomu za uchaguzi uliofutwa na wanakusudia kugombea nafasi zile zile, hawatalipia tena ada ya fomu husika, bali wataambatanisha stakabadhi za malipo (risiti), wakati wa kuzirejesha.
Mbwezeleni, mwanasheria mkuu wa zamani wa Zanzibar, aliongeza kuwa hakuna kizuizi kwa wagombea waliokuwa wamekataliwa katika mchakato wa awali kujitosa katika uchaguzi huu.
Akielezea suala la pingamizi kwa wagombea, Mbwezeleni alisema kuwa utaratibu wa awali wa yeyote kuweka pingamizi, kwa sasa hautotumika, kwani ulichangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa pingamizi ‘hewa,’ ambapo waliopinga hawakutoa ushahidi kwa kamati.
“Kwa sasa watakaoruhusiwa kuweka pingamizi ni wanachama wa TFF, ambao ni vyama vya soka vya mikoa, vyama vya waamuzi, wachezaji, viongozi wa klabu na viongozi wa kuteuliwa, ili kukwepa usumbufu wa baadhi ya wanaopinga kutotoa ushirikiano unaohitajika,” alisema Mbwezeleni.
Katika mchakato uliofutwa, aliibuka mdau aliyejiita Agape Fue na kumwekea pingamizi mmoja wa wagombea, huku mwenyewe akiwa hajawahi kujitokeza hata siku moja, kitendo kilichoibua malalamiko lukuki.
Aidha, Mbwezeleni alivitaka vyombo vya habari kuzisaidia kamati za Uchaguzi na ile ya Maadili kwa kufanikisha uchaguzi huru na wa haki, usio na malalamiko yatokanayo na upotoshaji wa habari na madai ya kupandikiza kutoka kwa wagombea watakaopingana na uamuzi wa kamati.
“Hii ni ngoma, wachezaji ni kamati husika na wagombea. Wanahabari msigeuke wachezaji, nyie ni watazamaji na mnapaswa kubaki hivyo, ili kujua nani kati ya sisi (kamati) na wao (wagombea) wanacheza vizuri na kwa usahihi,” alisisitiza Mbwezeleni.
Wakati huo huo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokuwa ikutane juzi Agosti 13 na jana Agosti 14 kupitia usajili wa wachezaji kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza, haikufanya hivyo na sasa itakutana kesho saa 4 asubuhi.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Alex Mgongolwa, amepanga kesho, baada ya vikao vya juzi na jana kushindwa kupata akidi.