Sunday, July 21, 2013

Yanga yakwepa kipigo cha Simba 
Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la kuzawazisha dhidhi ya URA ya Uganda, lililofungwa na Jerson Tegete katika dakika ya 90 ya mchezo na kufanya matokeo kuwa 2-2. Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki umefanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
MABINGWA wa Soka Tanzania Bara, Yanga, jana almanusra wapate aibu kama ya watani wao Simba, baada ya kulazimisha sare ya mabao 2-2 kwa URA ya Uganda.
Simba, juzi ilikumbana na kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kutoka kwa Watoza Ushuru hao wa Uganda, mabao yote yakifungwa Litumba Yayo.
Lakini katika hali ya kushangaza, mshambuliaji anayetarajiwa kusajiliwa na Yanga, Ogbu Brendan, raia wa Nigeria, licha ya kupangwa kikosi cha kwanza, hakuonekana dimbani kwa kile kilichoelezwa kuumia, hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Didier Kavumbagu.
Beki wa URA ya Uganda, Lutimba Yayo akimpa 'konga' Mshambuliaji
wa Yanga, Jerson Tegete huku akimiliki mpira.
Mechi hiyo ya jana iliyopigwa kwenye uwanja huo, ilianza kwa kasi na dakika ya 41, mtambo wa mabao wa URA, Litumba Yayo, ulimtungua kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.
Kama haitoshi, alikuwa ni Yayo tena dakika ya 51, aliyepachika bao la pili kwa mkwaju wa adhabu ndogo.
Yanga walifanya mabadiliko kadhaa, ambayo yalibadilisha sura ya mchezo na kufanikiwa kujipatia bao la kwanza dakika ya 66 likifungwa Kavumbagu kwa kichwa baada ya krosi ya Juma Abdul.
Ndipo dakika ya 72 alipoingia kiungo wa kimataifa Rwanda Haruna Niyonzima kwa kuchukua nafasi ya Bahanunzi, nakuanza kuubadilisha mchezo kwa ujumla huku tetesi zikisema kuwa alifika uwanjani akitokea moja kwa moja Uwanja wa ndege wa Mw.J.K. Nyerere alipowasili wakati anatokea nchini kwao Rwanda.
Wakati mashabiki wakianza kuondoka uwanjani wakiamini Yanga imelala 2-1, alikuwa ni Jerry Tegete aliyefuta aibu kwa kupachika bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi.
Heka heka nguo kuchanika ndani ya dimba
Yanga: Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajab Zahir, Salum Telela, Saidi Bahanuzi, Hamis Thabit, Jerry Tegete, Brendan Ogbu, Shaban Kondo.
URA: Mugabi Yastin, Derick Walulya, Sekito Samwel, Docea Mussa, Joseph Owino, Nkungwa Elkanel, Peni Ali, Lutimba Yayo, James Kasibante, Ngama Emmanuel, Bwete Brian.
URA itashuka katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga, Jumatano kukipiga na Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Wachezaji wa URA wakishangilia bao la pili

No comments:

Post a Comment