Monday, September 9, 2013

Serena atetea taji la US Open

Serena Williams atetea taji la US Open
NYOTA namba moja kwa ubora wa tennis kwa wanawake, Serena Williams, ameseka kama angeshindwa kutetea ubingwa wa michuano ya US Open ukiwa wa tano katika historia yake, mwaka 2013 ungekuwa mbaya kwake.
Serena (31), juzi alitetea taji akimshinda Victoria Azarenka raia wa Belarus kwa 7-5 6-7 (6-8) 6-1, likiwa taji lake la pili la kimataifa kwa mwaka huu, akianza na French Open.
Aidha, Williams amefikisha taji la 17 la kimataifa katika historia yake kama ilivyo kwa Roger Federer, raia wa Uswis ambaye ni nyota namba saba kwa ubora.
Pia, kwa ushindi wa jana, Serena ameweka rekodi ya kushinda mechi 34 kwa mwaka huu wa 2013.
"Licha ya kutwaa ubingwa wa French Open, kama nisinngetetea ubingwa wa US Open, mwaka huu ungekuwa mbaya kwangu.
"Mambo yaliniendea vizuri katika fainali hii ya US Opena kuliko ilivyokuwa French Open.
Hata hivyo, pamoja na Azarenka ambaye ni nyota namba mbili kwa ubora kufungwa mechi hiyo, alionesha upinzani mkubwa kwa Serena aliyetumia mbinu na uzoefu zaidi kupindua matokeo hayo na kuibuka mshindi.
Kwa Azarenka ni bahati mbaya kwake kufungwa katika fainali ya michuano hiyo kama ilivyokuwa mwaka jana alipofungwa pia na Serena.

Gareth Bale apata majeraha

Gareth Bale apata majeraha
GARETH Bale aliyetua Real Madrid akitokea Tottenham kwa dau kubwa linalomfanya kuwa ghari zaidi, ameumia nyonga kwenye mazoezi kuelekea mechi ya kimataifa kati ya Wales na Macedonia iliyochezwa Ijumaa iliyopita.
Baada ya Bale kukosa mechi hiyo ambayo Wales walifungwa, kocha wake Chris Coleman amesema atafanyiwa vipimo zaidi kuona kama atacheza mechi dhidi ya Serbia, itakayochezwa mjini Cardiff.
"Tunapaswa kufanya kitu kwa Gareth kabla ya mechi kwa sababu ana maumivu ya nyonga," alisema kocha huyo na kuongeza kuwa kipimo hicho ndio kitatoa majibu yote.
Wakati nyota huyo akiwa majeruhi, Klabu yake ya Real Madrid aliyojiunga nayo hivi karibuni kwa kitita cha pauni mil 86, ilipanga kumchezesha katika mechi la La Liga ya Septemba 14 dhidi ya Villarreal.
Bale sasa anaungana na Cristiano Ronaldo ambaye naye anaweza kukosa mechi hiyo kutokana na kukabiliwa na maumivu.
Kuhusu Bale, kuna habari kuwa Real Madrid ndio iliomba asipangwe kwenye mechi ya Ijumaa dhidi ya Macedonia na Serbia itakayochezwa leo.
Pamoja na hayo, Bale mwenyewe anataka kucheza ili kuboresha kiwango chake, pia ni heshima kuichezea nchi yake na kuisaidia katika kampeni ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia.
"Nina maumivu madogo yatakayochukua muda mfupi kupona, lakini mara zote nipo hapa kuiwakilisha Madrid. Naamini nitapangwa katika mechi ya nchi yangu (Wales) ili kuboresha kiwango changu kuelekea mechi ya Real Madrid dhidi ya Villarreal," alisema.

Kocha Cameroon akerwa Eto’o kustaafu soka

Kocha Cameroon akerwa Eto’o kustaafu
KOCHA wa timu ya taifa ya Cameroon, Volke Finke amekanusha habari kuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Samuel Eto'o ameamua kustaafu soka ya kimataifa.
Kauli ya kocha huyo inatokana na habari kuwa, Eto’o (32), nyota bora mara nne wa Afrika kwamba mechi ya Jumamosi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia dhidi ya Libya, ilikuwa ya mwisho kwake.
Katika mechi hiyo ya kundi I, Cameroon walishinda bao 1-0, hivyo kumaliza kinara wa kundi hilo kwa pointi 13 na kutinga hatua ya 10 bora itakayotoa timu tano za kwenda Brazil kwa fainali za Kombe la Dunia.
Nyingine zilizotinga hatua ya 10 bora ni Ethiopia, Algeria, Senegal, Burkina Faso, Nigeria, Misri, Ghana, Ivory Coast na Cape Verde kucheza hatua hiyo ya kupigania nafasi tano za kwenda Brazil, mwakani.
Baada ya miamba 10 kujulikana, Septemba 16 kutafanyika droo itakayozingatia ubora kwa mujibu wa viwango vipya vya Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa) kwa timu kucheza mechi mbili, nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla kujitwalia tiketi.
"Samuel Eto'o ni mchezaji mahiri, hivyo ingependeza kama kauli hiyo ingetoka kwake. Yeye pekee ndiye wa kufanya maamuzi sahihi," alisema Finke.
"Ameiletea mafanikio makubwa soka na Cameroon, ndio maana nasema yeye ndiye angeweza kulisema hilo sio kusemewa."
Eto'o aliyetua Chelsea hivi karibuni akitokea Anzhi Makhachkala ya Russia, hakutokea kwenye mkutano na waandishi wa habari kuelezea kama kweli amestaafu timu ya taifa au hapana.
Hata hivyo, kuna habari kuwa nyota huyo anakusudia kustaafu soka ya kimataifa akitaka kujielekeza zaidi katika kuendeleza kituo chake cha soka ya vijana.
Aidha, Eto'o amekuwa na jukumu la kumtibia aliyekuwa kocha wa Cameroon, Jean Paul Akono, aliyepatwa na maradhi ya kupooza mapema mwaka huu.
Baaada ya Cameroon kuifunga Libya katika mechi ya jana usiku, Finke alimpongeza Akono, aliyemrithi kwenye nafasi hiyo ya Indomitable Lions.
"Nampongeza Jean Paul Akono, aliyeshinda mechi tatu za kwanza katika kampeni hii, hivyo ni sehermu ya mafanikio ya leo," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.
Baada ya kutinga hatua ya 10 bora, kazi kubwa iliyobaki kwa Cameroon ni kusubiri kuona inapangwa kucheza na nani katika mtoano kwenye droo itakayofanyika Septemba 16, itakayofanyika Cairo, Misri.

Manchester Utd kumsajili Benteke Januari

Manchester Utd kumsajili Benteke Januari
KLABU ya Manchester United imeonesha nia ya kumtaka mchezaji wa Aston Villa, Christian Benteke.
David Moyes amekuwa shabiki mkubwa wa mchezaji huyo katika Ligi Kuu England ambaye anaamini anaweza kuziba pengo la Wayne Rooney kama hatoweza kuongeza mkataba mpya.
Moyes amemtengea mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, mshahara wa Pauni 60,000 kwa wiki.
Kocha wa Aston Villa, Paul Lambert  amesema hatokuwa na uweza wa kumzua mshambuliaji huyo kutimka kwa kuwa ofa hiyo ya mshahara ni kubwa kwake.
Moyes pia ameonesha nia ya kumuhitaji mwengine mshambuliaji Edinson Cavani anayekipiga Paris Saint-Germain. 
Benteke ndiyo tarajio lao kubwa katika usajili wa dirisha dogo la Januari.