Azam kukipiga na 'vigogo' Sauzi
|
Wachezaji wa Azam FC wakishangilia moja ya mechi zao |
KLABU inayokuja kwa kasi katika medani ya soka hapa nchini,
Azam FC, inatarajiwa kucheza mechi nne za kirafiki katika ziara yao nchini
Arika Kusini ikiwamo dhidi ya mabingwa wa nchi hiyo, Orando Pirates.
Azam FC, klabu inayozipa changamoto klabu kongwe za Simba na
Yanga kutokana na uimara wake kila idara, tofauti na wakongwe hao
wanaojiendesha kwa kuunga kuunga.
Meneja wa Azam FC, Said Jemedari, alisema kila kitu hadi
sasa kinakwenda sawa na inasubiriwa siku ya kukwea pipa kwenda kufanya ziara
yao, ambayo itakuwa na manufaa kwa timu nzima ambayo inakabiliwa na michuano
mbalimbali hapo mbeleni.
Jemedari alizitaja timu ambazo wataumana nazo katika ziara
yao ya siku 12 kuwa ni Amazulu, Supersport United, Bidvpst Wits pamoja na
Orando.
“Tuna imani mechi hizo nne zitamuonyesha mwalimu wapi
tuendako na kujua makosa ya kufanyia maboresho kabla ya mchezo wetu na Yanga
Agosti 17 na Ligi Kuu,” alisema Jemedari.
Katika hatua nyingine, Jemedari alisema juzi walishuka
dimbani kumenyana na Kombaini ya Majeshi, mchezo uliopigwa dimba la Chamazi nje
kidogo ya jiji na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, mabao yalifungwa na Hussein
Nyamandulu wa CISM na Tchetche Kipre kwa Azam FC.
CISM inaundwa na wachezaji wa timu za Jeshi ambazo ni JKT
Ruvu, Mgambo, Ruvu Shooting, Oljoro, Trans Camp, Kipanga na Rhino Rangers ipo
katika maandalizi ya kushiriki mashindano hayo yatakayorindima kuanzia timu za
Majeshi Afrika Mashariki yatakayofanyika Agosti 5-17 jijini Nairobi nchini
Kenya.