Friday, July 19, 2013


Titi Vilanova

Kansa yamuachisha kazi Vilanova

 KLABU ya Barcelona imezungumza na wanahabari na kuwambia kwamba kocha wake Tito Vilanova ameacha kazi kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kansa ya koo.
Vilanova, ambaye alijiunga Nou Camp akichukua nafasi ya Pep Guardiola katika msimu uliopita, lakini mwaka 2011, alijikuta akisumbuliwa na maradhi ya kansa.
Maradhi hayo yalionekana kukua kila uchwao hali iliyosababisha Desemba kufanyiwa upasuaji katika tezi yake kabla ya kuanza matibabu kwenye kituo cha mionzi cha New York.
Mwaka huu tatizo limekuwa kubwa hali iliyosababisha kufanyiwa matibabu makubwa ikiwa ni pamoja na kuwa na mwangalizi.
Katika mkutano huo wa wanahabari uliohudhuliwa pia na wanachama wa klabu hiyo, Rais wa Barca, Sandro Rosell alisema "Habari ambayo ninayo ni kuhusu jambo nisilohitaji kuwaeleza.
“Baada ya kutathmini juu ya Tito na kumfanyia vipimo nasikitika kuwaambia kwamba hataweza kuwa kocha chaguo la kwanza.
Baadhi ya wachezaji waliohudhulia mkutano huo alikuwa mchezaji Lionel Messi na baadhi ya wachezaji wengine.
Akizungumzia kuhusu kama klabu hiyo itatafuta kocha mwingine katika siku za hivi karibuni.
"Tutatangaza jina la kocha mpya wa FC Barcelona mapema wiki ijayo," Rosell aliongeza katika maelezo yake.
Tetesi kutoka Hispania zinasema kuwa huenda kati ya makocha hawa watapewa timu hiyo ambao ni Joan Francesc Ferrer ‘Rubi’, na kocha wa Tottenham, Andre Villas-Boas.
Alvaro Negredo
Negredo atua Man City kwa rekodi Sevilla
MANCHESTER City imefanikiwa kumsajili Alvaro Negredo kwa kitita cha pauni mil 24 kutoka Sevilla ya Hispania kwa ajili ya msimu ujao.
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania, ametua Manchester City akiwa mchezaji wa tatu kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao huku ikikaribia kumnasa pia  mshambuliaji wa Fiorentina,
Stevan Jovetic.
Wakati ikicheua pauni mil 24 kumpata Negredo, inaweza kumpata Jovetic kwa kiasi cha pauni mil 23, hivyo hadi sasa imetumia jumla ya pauni mil 90 kwa usajili.
Tayari Negredo (27), ameshafanyiwa vipimo tangu Alhamisi kabla ya kujiunga rasmi na Manchester City iliyomaliza ziara yake nchini Afrika Kusini tangu juzi ikifungwa 2-1 dhidi ya AmaZule.
Negredo ni kati ya washambuliaji wazuri kwani katika msimu uliopita, alimaliza nafasi ya nne kwenye La Liga kwa kufunga mabao 25, nyuma ya Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Radamel Falcao.
Nyota huyo aliyeweka rekodi ya usajili kwa klabu yake ya Sevilla, ameondoka baada ya kuitumikia kwa misimu minne akiifungia mabao 70.
Kwa upande wa timu ya taifa ya Hispania, amecheza mechi 14 na kuifungia mabao sita.
Akizungumzia kuhama kwake, Negredo alisema miaka yake mine ya kucheza Sevilla ilikuwa ya furaha kubwa, lakini wakati wa kucheza hapo, umekwisha anafurahia kujiunga na timu kubwa.
Negredo ni kama amemfuata nyota mwingine wa zamani wa  Sevilla, Jesus Navas aliyetua Etihad mwezi uliopita pamoja na kiungo mwingine Mbrazil Fernandinho.
Negredo atakuwa akivalia jezi namba tisa ambayo ilikuwa haina mtu tangu aondoke  Emmanuel Adebayor, nyota wa kimataifa wa Togo.
Fabregas
Wenger: Man United hawampati Fabregas
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amewakatisha tamaa Manchester United kuhusu kumwania Cesc Fabregas wa FC Barcelkwa ya Hispania akisema wanajisumbua bure kwani hawatampata kwa msimu huu.
Wenger aliyewahi kumwania nyota huyo bila mafanikio kumrejesha Emirates msimu ujao ikiwa ni misimu miwili tangu aondoke Emirates, alisema Fabregas hawezi kwenda Old Trafford.
Alisema hiyo inatokana na Fabrega kutamka wazi kuwa bado anapenda kubaki Barcelona, hivyo Manchester United wanajisumbua bure kumwania mchezaji huyo.
Alisema kwa mazingira haoni sababu ya kuongeza dau kwa Fabregas kumzuia kwenda Old Trafford kwani anaamini hawezi kuondoka Camp Nou msimu huu.
Kauli hiyo inatokana na Arsenal kukwama kumrejesha Fabregas kwa dau la pauni mil 29, hivyo hofu yake ni kwenda Man Utd iliyo tayari kumsajili kwa pauni mil 30.     
"Fabregas ameamua kubaki Barcelona," alisema Wenger mbele ya waandishi wa Habari juzi na kuongeza:
Vita ya kumwania Fabregas ni kutokana na shauku ya nyota huyo kukosa uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza cha Barcelona tangu arejee akitokea Arsenal miaka miwili iliyopita.
Haya hivyo, kitendo cha kuondoka kwa Thiago aliyetimkia Bayern Munich  ya Ujerumani, kumeongeza uzito wa kubaki kutokana na presha ya namba kupungua katika nafasi ya kiungo chini ya Kocha Tito Vilanova.
Mapema wiki hii, Vilanova alisema nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, angependa kubaki Camp Nou kuboresha kiwango chake zaidi.
"Najua amepata ofa nyingi. Lakini nimezungumza naye amenieleza angependa kubaki.
"Hana mpango wa kwenda kwingine. Anajua kuwa hapa ndipo mahali anapoweza kucheza michuano ya kimataifa. Ndoto yake ni kupata mafanikio hapa."
Luis Suarez
Arsenal yampandia dau Luis Suarez
KLABU ya Arsenal imezidi kuonesha nia yake ya kupata saini ya mshambuliaji mtukutu Luis Suarez, raia wa Uruguay baada ya kuongeza dau hadi pauni mil 40 ili aweze kutua Emirates.   
Kiasi hicho ni nyongeza ya pauni mil 5 ya dau la awali la pauni mil 35 ambalo lilitupwa na Liverpool licha ya nyota huyo kuonesha wazi kutaka kuhama Anfield na kwenda Arsenal.
Habari zinasema, kwa kiasi hicho kipya cha fedha huenda suala la mchezaji huyo likapata ufumbuzi ndani ya saa 48 kuanzia jana kwani tayari Kocha Arsene Wenger anajiandaa kuwasilisha ofa hiyo mpya.
Kuna habari kuwa, Arsenal sasa imeamua kuacha mambo mengine ili kupigania usajili wa nyota aweze kucheza Emirates msimu ujao.
Wakati Arsenal ikipambana kusaka saini ya nyota huyo, Liverpool nayo imekuwa ikijitahidi kumzuia asiondoke kutokana na umuhimu wake dimbani.
Mbali ya Arsenal, Suarez amekuwa akimezewa mate na klabu kadhaa ikiwemo Real Madrid ya Hispania
Pamoja na Arsenal ‘kujikamua’ hadi kiasi cha pauni mil 40, Kocha wa Liverepool,  Brendan Rodgers amekuwa akisema thamani ya nyota huyo ni pauni mil 55 kama ya Edinson Cavani.
Cavani ambaye pia ni nyota wa kimataifa wa Uruguay, amejiunga na Paris Saint-Germain tangu Jumanne wiki hii akitokea Napoli ya Italia.
Pamoja na kauli ya kocha huyo, hatima ya mchezaji huyo atakayekosa mechi sita za awali za Ligi Kkuu, itaamuliwa na mmiliki wa klabu hiyo,
Kampuni ya Fenway Sports Group ya Marekani inayomiliki klabu hiyo.
Kuna uwezekano wa Arsenal kufanikiwa mpango huo kutokana mkataba wake kuonesha kuwa hiyo ndio 
thamani yake ya kuuzwa.
Lakini, Liverpool imedai kuwa suala la thamani hiyo kuandikwa kwenye mkataba, haina maana ndio tahamni halisi ya nyota huyo kuondoka Anfield.
Hata hivyo, Arsenal inaamini kuwa itampata mchezaji huyo ambaye amekuwa na shauku ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati hayo yakiendelea, Suarez anatarajiwa kujiunga na Liverpool hapo kesho kwa safari ya kwenda
Australia kwa ziara ya mechi za kirafiki kwa ajili ya msimu ujao.
Suarez ni chaguo la kwanza la Wenger katika msimu huu kabla ya kuangalia uwezekano wa kuwapata Gonzalo Higuain wa Real Madrid ya Hispania na Wayne Rooney wa Manchester United.
Kuhusu Higuain, nyota wa kimataifa wa Argentina, Real Madrid imeshasema kwamba inataka kiasi cha pauni mil 25.5 ili kumruhusu.
YayaToure

Toure amwagia sifa Tata Madiba 

KIUNGO mahiri wa timu ya Manchester City, Yaya Toure amesema ni heshima na historia ya aina yake kwake na wachezaji wengine kucheza mechi rasmi ya kuadhimisha miaka 95 ya Rais 
wa zamani wa nchini hapa, Mzee Nelson Mandela.
Toure ambaye pia ni nyota bora wa Afrika, aliyasema hayo juzi saa chache kabla ya timu yake ya Manchester City iliyopo nchini kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya England  kucheza mechi ya kirafiki kwa heshima ya Mandela dhidi ya AmaZulu ikiwa ya mwisho katika ziara yao.
Mechi hiyo iliyochezwa juzi jioni katika Uwanja wa Moses Mabhida ilikwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 95 ya kuzaliwa kwa Mzee Mandela ambayo iliadhimishwa katika nchi mbalimbali za ndani na nje ya Afrika kwa kufanya shughuli za kijamii kwa dakika 67.
Walitumia dakika hizo kama ishara ya miaka 67 ya harakati za Mzee Mandela katika masuala ya kisiasa kwa kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini ambaye aliongoza kwa miaka mitano kabla ya kumpisha Thabo Mbeki na sasa Jacob Zuma.
"Ni birthday ya mzee wa Africa. Nafurahi sana na kujisikia fahari kubwa kucheza mechi hii maalumu ya kuadhimisha miaka 95. Naamini atapata nafuu haraka," alisema Toure alipozungumza na Footba ll411. 
Yaya aliyekuwemo kwenye kikosi kilichofungwa mabao 2-0 na SuperSport United wiki iliyopita, alisema wakiwa nchini hapa wamenufaika kwa kiasi kikubwa na ziara ya nchini hapa ndio maana walionesha kiwango bora walipocheza dhidi ya Usuthu. 
"Tumekuwa tikicheza kwa juhudi kubwa kujiweka fiti kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya England," alisema Toure na kuongeza: 
"Kwetu ni mechi muhimu sana. Nimekuwa nikifarijika kucheza na timu za Afrika kwani tunapata fursa ya kujifunza mengi." 
Toure, aliyetoa mchango mkubwa kwa Man City kutwaa ubingwa wa England msimu wa 2011/12, alisema kurejea kwa Jose Mourinho katika timu ya Chelsea na David Moyes kuino Manchester United na usajili wa nyota mbalimbali wapya, kutaongeza ugumu wa ligi hiyo msimu ujao.  
"Kurejea kwa Mourinho katika Ligi Kuu ya England na usajili wa nyota wapya huku Chelsea na Arsenal zikipambana kurejesha heshima yao, nadhani itakuwa ni ligi ya ushindani zaidi, lakini naamini tutabeba ubingwa kwa sababu tuna kikosi bora." 
Kwa mujibu wa Toure, City inajipanga kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwezekana kutwaa uningwa baada ya kuishia hatua ya makundi katika misimu miwili iliyopita.

Bongani Ndulula (kulia) wa AmaZulu akifunga bao la kwanza kwa
timu yake dhidi ya Manchester City, juzi
Man City yamaliza ziara kwa kichapo
MANCHESTER City ya England, juzi ilikumbana na kichapo kingine cha mabao 2-1 kutoka kwa AmaZulu katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mosea Mabida, mjini hapa.
Katika mechi hiyo iliyokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 95 ya Mzee Nelson Mandela, Manchester City walicheza bila kocha wake Manuel Pellegrini aliyeondoka ghafla na kwenda Chile kwa matatizo ya kifamilia.
Licha ya mechi hiyo kupambwa na furaha ya timu hiyo kufanikiwa kuwasajili wachezaji Alvaro Negredo Stevan Jovetic, walishindwa kuhimili kishindo cha AmaZulu hivyo kupata kichapo kingine kama ilivyokuwa Jumapili walipofungwa mabao 2-0 na SuperSport, mjini Pretoria.
Katika mechi ya juzi, AmaZulu walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 20, likifungwa na Bongani Ndulula kabla ya Manchester City kusawazisha dakika ya 26, likifungwa na James Milner, hivyo timu hizo kwenda mapumziko zilkiwa sare ya bao 1-1.
Zikisalia dakika tatu kabla ya filimbi ya wmisho, Van Heerden aliifungia AmaZulu bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti.
AmaZulu: Kapini; Macala, Teyise, Msekeli, Hlanti; Madondo, Madubanya, Manqana, Zondi, Dlamini; Ndulula. 
Man City: Hart/Pantilimon; Richards/Zabaleta, Kompany/Garcia, Nastasic/Lescott, Kolarov/Boyata, Milner/Razak, Toure/Rodwell, Fernandinho/Barry, Sinclair; Dzeko/Nimely, Nasri/ Suarez. 
Kuhusu kutokuwepo kwa Pellegrini, Msaidizi wake Brian Kidd alisema aliondoka ghafla kwa matatizo ya kifamilia akiwa tayari amerpanga kikosi cha kwanza katika mechi hiyo ya kirafiki ya juzi, akiwapanga  myota mpya Fernandinho aliyesajiliwa kwa pauni mil 30 na Yaya Toure katika kiungo.

Misri, Cameroon zafumua ratiba Caf 
KAMPENI ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoendelea mwishoni kwa wiki hii, imeingia dosari kutokana na mechi moja kuahirishwa na nyingine zikiwa kwenye hatihati kuchezwa kutokana na sababu kadha wa kadha.  
Mechi mojawapo iliyoindia doa ni kati ya Coton Sport ya Cameroon na Sewe Sports ya Ivory Coast za kundi B ambayo imesitishwa kwa wiki moja kupisha maridhiano kati ya Shirikisho 
la soka la Cameroon (Fecafoot) na Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa).
Hivi karibuni, Fecafoot ilisimamishwa uanachama na Fifa kutokana na Waziri wa Michezo 
kuingilia kati uendeshaji wa shughuli za soka, hivyo mechi hiyo haiwezi kuchezwa hadi 
pande hizo mbili zitakapopata suluhu ya mvutano uliopo.    
Mechi nyingine iliyopo kizani ni kati ya Zamalek na Al Ahli za Misri ambazo zilikuwa 
zicheze leo mjini Cairo katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ambayo sasa 
itachezwa kesho.  
Shirikisho la soka Afrika (Caf), lilisema kuwa hadi kufikia jana, walikuwa wakijadiliana 
na Chama cha soka cha Misri (EFA) huku kukiwa na habari kuwa, viongozi wa EFA 
wanahofia athari ya mapato kutokana na mabadiliko hayo.
Hata hivyo, kumekuwa na mkanganyiko kuhusu lini mechi hiyo itachezwa kwani Ahly 
Kupitia mtandao wao wanasema mechi hiyo itachezwa kati ya Jumanne au Jumatano 
huku taarifa ya Zamalek ikisema mechi hiyo ni Jumatatu au Jumatano.
Kauli hizo mbili tofauti juu ya lini hasa mechi hiyo itachezwa, imeleta mkanganyiko 
mkubwa japo inajulikana wazi sasa itachezwa mjini  El Gouna huku mashabiki wengi 
wakiwa na hofu ya kuzuka vurugu.
Aidhga, kutokana na uwanja huo kutokuwa na taa za kutosha, mechi hiyo imepangwa kuanza mapema. 
Kwa upande wa mechi ya Coton Sport na Sewe Sports iliyokuwa ichezwe leo, imesogezwa hadi Julai 27 kutoa nafasi kwa Fecafoot na Fifa kumaliza mgogoro uliopo.  
Julai 4, Fifa iliifungia Cameroon kutokana na serikali kuingilia utendaji wa Fecafoot ikitaka kuundwe Kakati ya mpito kuendesha shughuli za soka kuelekea uchaguzi mkuu.

Zambia, Zimbabwe fainali Cosafa
ZAMBIA ambao ni wenyeji wa Kombe la Cosafa wametinga fainali ya michuano hiyo baada ya kuwafunga Afrika Kusini katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa Jumatano, hivyo watacheza 
na mabingwa watetezi Zimbabwe wikiendi hii. 
Wenyeji hao walitinga fainali kwa ushindi wa mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare katika muda wa kawaida ambapo Zambia walipata mikwaju yote huku shuti ya Lerato Chabangu wa Afrika ikipanguliwa na Danny Munyau. 
Zambia sasa itakutana na Zimbwabwe ambapo timu hizo zitakuwa na kumbukumbu ya fainali ya michuano hiyo ya mwaka 2009, baada ya Zimbwabwe kuifunga Lesotho mabao 2-1.

Keshi amwita Ameobi kuivaa Bafana Bafana

KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Stephen Keshi amemwita mshambuliaji wa kimataifa Shola Ameobi anayekipiga Newcastle United ya England kwa ajili ya mechi maalumu dhidi ya Bafana Bafana kwa heshima ya Mzee Nelson Mandela ambaye juzi alitimiza umri wa miaka 95. 
Keshi amemwita Ameobi kwa mechi hiyo itakayofanyika Agosti 14, mjini Durbun ambapo kutapigwa michuano maalumu ya Nelson Mandela Challenge.
Kuitwa kwa nyota huyo ni baada ya kumalizana na klabu yake ya Newcastle United kuhusu hatima ya mkataba wake ambao awali ulikuwa ukimzuia kuichezea timu hiyo ya taifa katika michuano ya Kombe la Afrika iliyochezwa mapema mwaka huu nchini hapa ambapo walitwaa ubingwa kwa kuwafunga Burkina Faso.
Kocha huyo aliamua kumpigania mchezaji huyo alitaka kuimarisha kikosi chake baada ya kuyumba katika mechi kadhaa kutokana na pengo la Emmanuel Emenike na Victor Moses ambao walikuwa majeruhi.
Baada ya kupona, Emenike na Moses watakuwemo kwenye kikosi hicho cha nyota 20 huku kipa waa muda mrefu Vincent Enyeama akiachwa baada ya nafasi yake kuzibwa na Obinna Nsofor na Uche Nwofor aliyeitwa kwa mara ya kwanza.
Naye Ogenyi Onazi anayecheza katika klabu ya Lazio ya Italia, amerejeshwa kwenye kikosi cha timu hiyo baada ya kushindwa kwenda nchini Brazil kwa michuano ya Kombe la Mabara kutokana na kuwa majeruhi.
Wachezaji hao na timu zao kwenye mabano ni:-
Makipa: Austin Ejide (Hapoel Be’er Sheva, Israel); Chigozie Agbim (Enugu Rangers, Nigeria)
Mabeki: Kenneth Omeruo (Chelsea FC, England); Efe Ambrose (Celtic FC, Scotland); Godfrey Oboabona (Sunshine Stars, Nigeria); Azubuike Egwuekwe (Warri Wolves, Nigeria); Elderson Echiejile (Sporting Braga, Ureno)
Viungo: Mikel Obi (Chelsea FC, England); Fegor Ogude (Valerenga FC, Norway); Victor Moses (Chelsea FC, England); John Ogu (Academica de Coimbra, Ureno); Ogenyi Onazi (SS Lazio, Italy); Nnamdi Oduamadi (AC Milan, Italia); Sunday Mba (Enugu Rangers, Nigeria).

Washambuliaji: Ahmed Musa (CSKA Moscow, Russia); Brown Ideye (Dynamo Kyiv, Ukraine); Shola Ameobi (Newcastle United, England); Emmanuel Emenike (Spartak Moscow, Russia); Obinna Nsofor (Lokomotiv Moscow, Russia); Uche Nwofor (VVV Venlo, Uholanzi)