Simba yamtoa bure Shomari Kapombe
UONGOZI wa Simba, umemtoa bila ada beki wake mahiri Shomari Kapombe kwa klabu ya AS Cannes ya Ufaransa inayoshiriki Ligi Daraja la Nne kwa lengo la kumtafu timu kubwa ndani ya miaka miwili.
Usajili huo, haujawahi kutokea wala kufanywa na klabu yoyote ya Tanzania, ambako kwa makubaliano waliyoingia, Simba itakuja kupata gawio endapo tu atauzwa timu nyingine.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, ‘Mr Liverpool’ AS Cannes itamgharamia Kapombe kwa kila kitu wakati akiwa Ufaransa na lengo la mchezaji huyo kubaki huko ni kumfanya awe bora zaidi kuliko Asasa.
“Kwenye makubaliano hayo, Simba haitapata chochote kwa sasa. Isipokuwa endapo Kapombe atapata timu, Simba itapata mgawo wake kutoka katika mauzo hayo, makocha wa Ulaya wamebaini kwamba, Kapombe ni mchezaji mzuri lakini anahitaji kuboreshewa vitu vichache kabla hajawa mchezaji mkubwa wa kutumainiwa na klabu kubwa,” alisema Kamwaga.
Alisema, katika mkataba huo mpya, Simba imeangalia zaidi maslahi ya Taifa na ya mchezaji kuliko ya klabu, kwa vile kama mchezaji huyo atapata nafasi Ulaya, hilo litafungua milango kwa wachezaji wengi wa Kitanzania, ambao kwa sasa hawapati fursa.
Wakala wa Kapombe, Denis Kadito, alisema, ingawa Kapombe ameonekana kuwa mchezaji mzuri, kutofahamika kwa jina la Tanzania kumekuwa kikwazo kikubwa kupata nafasi ya moja kwa moja na ndiyo maana imebidi aanzie kwenye hatua ya chini.
“Ofa hii ya Cannes ni nzuri, kwa sababu timu hiyo huwa inacheza na timu za akiba za klabu zote zinavyoshiriki katika Ligi Kuu ya Ufaransa na hivyo atakuwa anaonwa na mawakala wa timu kubwa kila wiki, hii itamsaidia kupata timu kubwa mapema ndani ya msimu mmoja kutoka sasa,” alisema Kadito.
Alisema, kutokana na mkataba huo wa Kapombe na Cannes, Simba sasa imeongeza mkataba wake na mchezaji huyo kwa miaka mitatu zaidi, kwa vile mkataba wake wa sasa unamalizika Aprili mwakani.
Aliongeza kuwa, Kapombe hatafanikiwa kupata timu katika kipindi cha miaka miwili kutoka sasa, atarejea klabu yake ya Simba kuendelea na majukumu yake.