Friday, July 26, 2013

Ahly, Zamalek zatoka sare 1-1
KIUNGO Mohamed Aboutrika wa Ahly, Jumatano usiku aliifungia bao timu yake kwa mkwaju wa penalti na kuisaidia kuvuna sare ya bao 1-1 dhidi ya Zamalek katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa mjini hapa.
Ingawa baadhi ya mechi za makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho zilichezwa mwishoni mwa wiki, mechi ya timu hizo mbili ilisogezwa hadi Jumatano kutokana na vurugu zilizoukumba mji wa Cairo na Alexandria.
Aboutreika alifunga bao kwa penalti dakika 27 kabla ya filimbi ya mwisho baada ya Salah Soliman wa Zamalek kumchezea vibaya mshambuliaji Ahmed Abdel-Zaher.
Bao hilo lilirejesha furaha kubwa wapenzi na mashabiki wa Ahly kutokana na timu yao kuwa nyuma tangu dakika ya nane baada ya Ahmed Gaafar kuifungia timu yake bao, akimtungua kipa Sherif Ekramy.
Kwa sare hiyo, timu zote za kundi A, zimelingana kwa pointi moja kwani katika mechi ya mwishoni mwa wiki, timu za Orlando Pirates ya Afrika Kusini na AC Leopards ya DR Congo zilishindwa kufungana.
Mechi hiyo ya Zamalek na Ahly, ilichezwa mjini El Gouna, badala ya Cairo kutokana na sababu za kiusalama baada ya uwepo wa maandamano ya wafuasi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Morsi.
Ingawa awali mechi hiyo ilitakiwa ipigwe bila mashabiki, lakini kutokana na ulinzi mkali wa vyombo vya usalama, mashabiki wapatao 7,000 waliingia kwenye uwanja wenye uwezo wa kubeba watu 12,000.
Matokeo hayo yanaifanya Ahly kuongoza kundi A, ikiwa na pointi moja ikifuatiwa na wapinzani wakubwa katika ligi ya Misri, Zamalek pia wenye poiinti moja kama ilivyo kwa Leopards ya DR Congo na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Libolo FC ya Angola inaongoza kundi B, ikiwa na pointi moja ikifuatiwa na Coton Sport ya Cameroon, Sewe ambazo hazijacheza na Esperance ya Tunisia iliyopoteza mechi ya kwanza mjini Luanda.
CASTLE LAGER yaileta Barcelona Afrika
Makamu wa Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu akimkabidhi Mkurugenzi wa Masoko Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Kashililla Thomas, amletee Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. TBL kupitia bia yake ya Castle jana iliingia mkataba wa ushirikiano wa miaka mitatu na klabu hiyo kwa upande wa Afrika.
BIA ya Castle Lager, jana iliingia makubaliano ya kuidhamini klabu maarufu Duniani, FC Barcelona ya Hispania kwa kipindi cha miaka mitatu udhamini utakaokifanya kinywaji
hicho kuwa bia rasmi ya klabu hiyo Afrika.
Hafla ya ushirikiano huo iliyofanyika kwenye uwanja wa Camp Nou, unaifanya CASTLE Lager kuwa bia rasmi itakayotumika kwa shughuli yoyote ambayo Barcelona itashiriki Afrika.
Aidha, chini ya ushirikiano huo, FC Barcelona itafungua milango kwa mashabiki wake Barcelona Afrika kuwa karibu na wachezaji wa Barcelona, vifaa na kumbukumbu.
Aidha, itapata nafasi ya kusafiri kwenda Hispania kushuhudia kwa karibu timu ya Barcelona.
Mkataba huu utakuwa maalum kwa ajili ya CASTLE Lager kwenye nchi nyingi za Afrika isipokuwa kwa baadhi ya nchi chache zilizochaguliwa ambapo itatumika Castle Milk Stout.
Ni mara ya kwanza kwa timu ya FC Barcelona kusaini mkataba
wa udhamini na kampuni ya bara la Afrika. Kushirikiana na bia bingwa Afrika litaongeza kwa haraka umaarufu wa timu ya FC Barcelona ndani ya bara la Afrika na kufungua milango kwa mashabiki wa klabu hii kupata bidhaa mbalimbali za Barcelona na nafasi za kushinda safari ya kwenda Barcelona kuitembelea klabu hiyo.
“Tumefurahi sana kuingia katika ushirikiano na Castle Lager na Castle Milk Stout, chapa zinayofahamika dunia nzima. Tunafanana na Castle kwa kuwa sote tuna historia ya zaidi ya miaka 100 na utamaduni uliotukuka. Na sote tuna mapenzi na mpira wa miguu pamoja na mashabiki wake katika soko muhimu kama Afrika,” alisema Javier Faus, Makamu wa Rais wa FC Barcelona anayeshughulikia masuala ya uchumi.
“Uamuzi wa Barcelona kuingia ushirika na na bia inayoongoza barani Afrika kutaongeza umaarufu wa bia hiyo kwenye bara hili na kuwawezesha wachezaji wa timu hiyo kufika maeneo amabyo hawajawahi kufika barani Afrika,” alisema David  Carruthers Mkurugenzi wa Masoko wa SabMiller Afrika (kampuni mama ya TBL).
CASTLE Lager si bidhaa mpya kwenye udhamini wa mpira wa miguu na vyama, ina miaka mingi ya kujihusisha katika soka barani Afrika kwa kipindi cha miaka 85 kupitia ligi mbalimbali za nchi tofauti kama vile Zimbabwe, Swaziland, Botswana, Lesotho na pia mashindano ya kanda kama COSAFA Kusini mwa Afrika na CECAFA Afrika Mashariki.
Kutokana na soka la Ulaya kupata umaarufu mkubwa na mashabiki wengi barani Afrika, Castle Lager imekuwa ikidhamini urushaji wa matangazo ya ligi hizo kwenye televisheni barani Afrikana kuwapa mashabiki fursa ya kufatilia kila kinachoendelea kwenye ligi hizo maarufu duniani ambazo ni Ligi Kuu ya Ulaya, Ligi Kuu ya Uingereza na La Liga ya Kihispania.
Kufuatia udhamini huu, wanywaji wa Castle Lager na Castle Milk Stout pamoja na mashabiki wa Barcelona barani Afrika sasa watarajie mambo mengi ya kusisimua katika ulimwengu wa soka. 
Stars yaapa kufia Uganda
Wachezaji wa Taifa Stars wakiwa katika mazoezi yao ya mwisho kabla ya mechi na Uganda
WAKATI timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars inashuka dimbani leo kuwakabili Uganda Cranes katika mechi ya kuamua tiketi ya kwenda Afrika Kusini kwa fainali za Afrika kwa nyota wa ndani (CHAN) hapo mwakani, Kocha 
Kim Poulsen amesema kazi kubwa kwa vijana wake ni kupambana mwanzo mwisho kupata mabao ya mapema.
Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya bia kupitia kinywaji chake cha Kilimanajro Premium Lager, inawakabili Uganda ikiwa nyuma kwa bao 1-0 walilofungwa katika mechi ya kwanza baina yao iliyochezwa Julai 13, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Kampala jana kuhusu kikosi chake, Poulsen alisema vijana amejiandaa vizuri na kwamba licha ya kuwa ni mwezi mgumu kisoka kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa kwenye mfungo, wachezaji wamepania kupata matokeo mazuri.
“Tunajua watanzania wengi walikataa tamaa au kupoteza matumanini baada ya sisi kufungwa 1-0, lakini katika mpira haya yanaweza kubadilika…tukifunga bao kesho litabadilisha kila kitu,” alisema Poulsen.
Alikiri kuwa mechi hii ya marudiano ni ngumu kwani Stars itakuwa inacheza na timu bora Afrika Mashariki
lakini lolote linaweza kutokea ndani ya dakika 90 au zaidi za mchezo.
Alisema licha ya kuwakosa wachezaji Shomari Kapombe na Mwinyi Kazimoto, maandalizi ni mazuri na hasa walipokuwa kambini Mwanza wachezaji walionesha bidii sana katika mazoezi.
Alisema katika mechi ya kesho watajitahidi kutengeneza nafasi nyingi na kufunga magoli. “Katika mazoezi yetu tumefanya mazoezi sana katika ushambuliaji, kutengeneza nafasi na kufunga magoli,”alisema huku akiongeza kuwa mabeki watahakikisha washambuliaji wa The Cranes hawapiti kabisa.
Aliwataka watanzania wawe na imani na timu ya Taifa kwa matokeo yoyote yatakayopatikana kesho kwani mpira ni safari na kukubali matokeo ni sehemu ya mchezo.
“Wachezaji wana ari ya kupata ushindi ili waende CHAN mwakani kwani hii itawapa nafasi nzuri ya kuonekana na vilabu kubwa duniani na tayari tumeona jinsi watu wengi wametambua kuwa kuna wachezaji wazuri Tanzania….Kapombe ameenda kwenye majaribio Uholanzi, Kyemba naye yuko njiani na nasikia Kazimoto yuko Qatar..nawatakia kila la heri.” Alisema.
Poulsen alisema Jumatatu atazungumza na waandishi wa habari kuhusu mipango ya muda mrefu ya Taifa Stars.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, ambaye Bia yake inadhamini Taifa Stars alisema wao kama wadhamini wanawaomba watanzania wawe na imani na stars na waiombee ifuzu mashindano ya CHAN.
“Sisi kama wadhamini tuna imani na timu yetu na tuna imani watafanya maajabu katika mechi ya kesho ili wawape raha watanzania,” alisema Kavishe.
Kilimanjaro Premium Lager imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa mwaka kuidhamini timu ya Taifa kwa mkataba wa miaka mitano.
Cranes inawakabili Stars leo ikiwa na tatizo la ufungaji kwani katika mechi mbili za kirafiki ilizocheza na vijana wa chini ya miaka 23 na kufungwa zote kwa bao 1-0 ambazo Denis Iguma aliyewafungia bao Julai 13, alichezeshwa sehemu ya kiungo.
Micho atawakosa wachezaji wake wawili wa mbele,  Tony Odur na Patrick Edema. Wakati Odur anauguza nyonga, Edema amekwenda Ureno kwa majaribio.
Katika kuziba pengo, Micho amewaita Simon Okwi (KCC FC), David Kasirye (URA FC) na Henry Oguti anayechezea Kiira Young.
Hata hivyo, Okwi ameitwa licha ya kushindwa kufungia bao KCC msimu uliopita huku kukiwa na shaka juu ya kiwango cha Kasirye.
Mazingira hayo yanamfanya Micho amtegemee Oguti kuongoza safu ya ushambuliaji anayeonekana kuwa na nguvu kuliko wengine ingawa kuna mwingine kama Frank Kalanda.
Barca yaitaabisha Man Utd kwa Fab
NDOTO za Klabu ya Manchester United kupata saini ya kiungo Cesc Fabregas, zimeyeyuka baada ya FC Barcelona kusisitiza kwa mara nyingine kuwa hawamtoi Camp Nou.
Licha ya Manchester United kugonga mwamba mara ya kwanza katika kumwania nyota huyo, bado ilituma ofa kwa mara ya pili ya pauni mil 30 na mchezaji. 
Makamu Rais wa Klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu amewajibu Manchester United, kuwa hawapo tayari kumuuza kiungo huyo kwa bei yoyote.
Japo Alhamisi wiki hii Kocha wa United, David Moyes, alisema wanaendelea na juhudi za kumwania, lakini wameelezwa kuwa waachane na bishara hiyo.
Bartomeu said: "Man United imekuwa ikimtaka Fabregas kwa muda mrefu kwa sababu ni mchezaji mkubwa, lakini hauzwi
Fabregas aliyecheza soka ya utoto katika klabu ya Barcelona kabla ya kutimkia Arsenal mwaka 2003, aliondoka Emirates Agosti 2011 na kurejea Camp Nou kwa kitita cha pauni mil 30.
Akiwa Arsenal, mechi yake ya kwanza ilikuwa ya Kombe la Ligi dhidi ya Rotherham United ya Oktoba, 2003, wakati huo akiwa na umri wa miaka 16 na siku 177.
Tangu arejee Barcelona, Fabregas amekuwa hana raha kutokana na kukosa uhakika wa kikosi cha kwanza hadi kutamani kuondoka, lakini kuondoka kwa Thiago kumeongeza thamani yake Camp Nou.
Ni mara ya kwanza kwa Bartomeu kuonekana hadharani akizungumza akiwa na kocha mpya
Gerardo Martino aliyeziba nafasi ya Tito Vilanova.
Ndoano ya kwanza ya Man United kwa kiungo huyo ilikuwa Julai 15, walipokuwa tayari kucheua kiasi cha pauni mil 25 ambazo zilikataliwa kabla ya kupanda hadi 30 na mchezaji.
Tangu arejee Barcelona, Fabregas amecheza mechi 96 zikiwemo 60 za La Liga, lakini amekuwa akifunikwa na uwepo wa nyota wengine kama Xavi (33) na Andres Iniesta (29). 
Azam Tv yacheuwa mabilioni Ligi Kuu
Baadhi ya viongozi wa TFF na Azam wakitiliana saini
KAMATI ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana imesaini makubaliano ya kuuza haki za kuonesha mechi za Ligi Kuu kwa Kampuni ya Azam Media Ltd kupitia kituo cha televisheni cha Azam Tv
kwa kipindi cha misimu mitatu, kuanzia  msimu wa 2013/14 utakaoanza Agosti 24.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa TFF, Ilala jijini Dar es Salaam, Azam Media itamwaga kitita cha shilingi bilioni 5.560 ikiwa nji thamani ya mkataba huo ambao utasainiwa ndani ya siku 30 kuanzia jana.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia, alisema kulikuwa na ofa nyingi
za zabuni ya kuonesha mechi za Ligi Kuu - zikiwamo kutoka nje ya nchi, lakini ofa ya Azam ni nono zaidi na kuongeza watatoa asilimia 25 kabla ya kuanza ligi.
Wallace alitumia fursa hiyo kuishukuru Azam kukubali kununua haki hiyo kwa ofa nono iliyozipiku kampuni kadhaa zikiwamo kongwe za kimataifa na kwamba wanajivunia kufanya kazi na kampuni ya kizawa iliyojitoa katika uwekezaji katika soka.
Akinuzngumza kwa niaba ya Rais wa TFF, Makamu wa Pili wa Rais Athumani Nyamlan aliwapongeza Azam Media Ltd kushinda manunuzi ya haki za kuonesha mechi za ligi kupitia kituo cha televisheni cha Azam Tv.
“Udhamini huu wa Azam Media Ltd, unastahili kupongezwa, hasa ukizingatia unakuja kipindi ambacho Tanzania kama taifa limeshaanza kunufaishwa na uwekezaji wa Kampuni SSB, ikiwamo kupitia michuano ya vijana ya Uhai Cup,” alisema Nyamlani.
Aliongeza kwamba Azam imefanya mengi ya kuigwa katika soka la Tanzania, lakini mkataba huu wa kwanza kwa kampuni ya nyumbani, unathibitisha utayari iliyonao SSB katika kusaidia harakati chanya za kunyanyua juu maendeleo ya soka nchini.
Akizungumza baada ya kutiliana saini kwa makubaliano hayo, Meneja wa Azam Media, Mzee Said Mohamed, alisema wamejipanga kufanya vitu vikubwa kupitia makubaliano hayo na kwamba kila Mtanzania atafurahia matangazo bora kupitia Azam Tv itakayozinduliwa Agosti 1.
Alibainisha kuwa, uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 30 wa kuanzishwa kwa Azam Tv chini ya Azam Media, unawapa uhakika wa matangazo bora ya televisheni, ili kushinda vita ya pili ambayo ni ya ubora wa huduma zake kwa wateja hususani wapenzi wa soka.
“Nia ya makubaliano haya na mkataba baina ya Azam Media na Kamati ya Ligi wa haki za kuonesha mechi za Ligi Kuu, ni kunyanyua maendeleo ya soka letu kwa mchezaji mmoja mmoja, klabu na hatimaye taifa kwa ujumla,” alisema Mzee Said.
Alisema kuwa, Azam Tv itahakikisha katika msimu huu wa kwanza, angalau kila klabu inaoneshwa mechi zake mara nne na kwamba kituo hicho kitarusha moja kwa moja (live) jumla ya mechi 60, huku zingine 82 zikioneshwa baada ya kurekodiwa (Recorded).
Aliongeza kuwa, licha ya msimu huu kutarajia kutoa shilingi milioni 25 za maandalizi kwa kila klabu shiriki kama makubaliano hayo yanavyowaongoza, matarajio yao ni kuwa baada ya kumalizika kwa mkataba wa sasa, kila klabu kupata milioni 100 za maandalizi.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Azam Media Ltd inamiliki haki ya kufanya maelewano na kituo chochote cha televisheni ndani na nje ya nchi, ili kuweza kuonesha ‘live’ au marudio ya mechi za ligi kuanzia msimu huu wa 2013/14 unaoanza Agosti 24.
Mzee Saidi alibainisha kuwa, Azam Media Ltd itatoa asilimia 25 ya thamani ya mkataba kabla ya kuanza msimu huu, huku akifichua kuwa wamefurahishwa kushinda zabuni ya haki ya kuonesha Ligi Kuu na kuzipiku kampuni kubwa ambazo hata hivyo hazikutajwa.
Kusainiwa kwa makubaliano hayo, kumefuatia mazungumzo kati ya Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu za Ligi Kuu, ambapo mkataba huo utazipunguzia mzigo klabu ambazo zimekuwa zikisumbuliwa na ukata kwa kutegemea udhamini wa Vodacom peke yake, ambao hautoshi.
Kashfa ya dawa inakera - Usain Bolt
BINGWA mara sita wa Olimpiki, Usain Bolt wa Jamaica, amesema anakabiliwa na jukumu zito la kuurejeshea heshima mchezo huo kitaifa na kimataifa baada ya nyota wenzake kuingia kwenye tuhuma za kutumia dawa za kusisimua misuli miezi miwili iliyopita.
Kauli hiyo imekuja huku wachezaji mahiri wa mbio fupi,
Asafa Powell wa Jamaica na Tyson Gay ambao wameangukia kwenye tuhuma hizo wakiungana na Sherone Simpson ndani ya mwaka huu.
Bolt (26), aliyeshiriki mbio za hisani wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Olympic, alisema ni jukumu lake na wachezaji wengine kufanya kweli ili kufukia kashfa hiyo katika riadha.  
"Nina kazi kubwa ya kufanya kufukia kashfa hii katika nchi yangu," alisema Bolt na kuongeza:
"Kwa sasa nimeelekeza nguvu katika hilo na kuwadhihirishia watu kuwa mafanikio na ushindi vyote vinawezekana katika mchezo huu."
Bolt aliyesisitiza kuwa yeye ni mtu safi kutokana na kutowahi kupatwa na kashfa ya kutumia dawa, lakini akasema yahitaji mtu kuwa mwangalivu sana asiangukie kwenye mkasa huo.
Bolt, bingwa wa mbio fupi katika mita 100 na 200, alisema kufanya kwake vizuri tangu akiwa kijana mdogo, ni uthibitiosho kuwa yeye ni mtu safi asiyetumia dawa za kuongeza nguvu.
"Nimewahi kuvunja rekodi nikiwa kijana mdogo ambayo hadi sasa haijavunjwa," alisema Bolt alipozungumza na BBC.
Nyota huyo alitumia nafasi hiyo kuueleza ulimwengu kuwa, amekuwa akipata mafanikio kutokana na kipaji kutoka kwa Mungu na juhudi katika mazoezi. 
Kocha mpya awahofia Messi, Neymar
Gerardo Martino
KOCHA mpya wa Barcelona, Gerardo Martino ametua rasmi Camp Nou na
kusema utakuwa mtihani mgumu kwake kama Lionel Messi na Neymar hawatang’ara katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Akizungumza kwa mara ya kwanza jana baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili, Gerardo alisema wazi ana kazi kubwa ya kuwamudu nyota hao wawili.
Alisema kutokana na umahiri wao, anajiona mwenye kazi ya ziada ya kuhakikisha nyota hao wawili wanacheza kwa ufanisi katika kikosi cha kwanza.
Lakini, akajifariji kwa kusema Neymar, aliyetua hivi karibuni kwa mkataba wa miaka mitano na Messi, nyota bora wa Dunia mara nne, hawatamwangusha.
"Kama Messi na Neymar watashindwa kucheza pamoja kwa ufanisi, itakuwa ni pigo kwangu kama kocha," alisema na kuongeza kuwa, jukumu kubwa kwake kuhakikisha wanaisaidia timu kushinda.
"Naamini Barca kwa kuwa na wachezaji hawa, itapata mafanikio makubwa. Kazi yangu ni kuwafanya wachezaji wanifahamu na kuniamini ili kuboresha kiwango,” alisema.
Kocha huyo ambaye ni mara ya kwanza kufundisha Ulaya, amepewa juhumu la timu hiyo kuchukua nafasi ya Tito Vilanova aliyepumzikoa kutokana na matatizo ya kiafya.