Wednesday, August 21, 2013

Eto’o atabiriwa kutimkia Chelsea

Eto’o atabiriwa kutimkia Chelsea

KOCHA wa zamani wa Anzhi Makhachkala, Rene Meulensteen, amesema hatashangazwa kusikia nyota wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o, anajiunga na Chelsea ya England inayonolewa na Jose Mourinho, raia wa Ureno.
Rene aliyewahi pia kuinoa Manchester United ya England, amesema kwa mazingira ya sasa ya Chelsea, hatashangazwa kuona Eto’o akiihama Anzhi na kujiunga na timu hiyo.
Uwezekano wa Eto’o kuondoka ni mkubwa kutokana na wengi kutamani kufanya hivyo wakihofia mwelekeo wao hasa baada ya mmiliki wa Anzhi, Suleyman Kerimov kuamua kupunguza matumizi ya uendeshaji wa timu.
Kitisho hicho ndicho pia kimemfanya mchezaji nyota wa kimataifa wa Brazil, Willian Borges da Silva kuwa kwenye mchakato wa kujiunga na Tottenham ya England kwa kitita cha pauni mil 30.
Chini ya mazingira hayo, haitashangaza kusikia Eto’o akithibitisha ambacho kimekuwa kikizungumzwa kwa muda mrefu kuwa anatamani kumfuata Mourinho kutokana na kuwahi kupata naye mafanikio makubwa akiwa Inter Milan ya Italia.
Meulensteen, mwenye rekodi ya kuinoa Anzhi kwa siku 16 kabla ya kutimuliwa, amesema Eto’o hawezi kubaki kwenye klabu hiyo na ligi pekee ambayo angependa kuicheza ni Ligi Kuu ya England hasa katika klabu ya Chelsea.
Kauli ya kocha huyo inakuja huku Mourinho akisema bado anasaka mshambuliaji katika kikosi chake na kuongeza kuwa hesabu zake hazipo kwa Wayne Rooney wa Manchester United, hivyo anaweza kusajili popote.

AC Milan yabanwa, Zenit yaua Ulaya

AC Milan yabanwa, Zenit yaua Ulaya
 Stephan El Shaarawy kushoto akishangilia bao lake pamoja na Abate
MABINGWA mara saba wa Ulaya, AC Milan ya Italia, jana ilivuna sare ya ugenini ya bao 1-1 dhidi ya PSV Eindhoven ya Uholanzi katika mechi ya kwanza ya mtoano kuwania tiketi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakicheza ugenini, Milan walitangulia kupata bao kabla ya wenyeji kusawazisha kutokana na makosa ya kipa Christian Abbiati, hivyo kutanguliza mguu mmoja hatua ya makundi kama itaulinda ushindi huo hadi marudiano.
Milan walipata bao kupitia kwa nyota mwenye asili ya Misri, Stephan El Shaarawy aliyefunga kwa kichwa kabla ya Tim Matavz kuisawazishia PSV.
Katika mechi nyingine za kuwania tiketi ya 32, Real Sociedad, Zenit St Petersburg na Plzen ya Czech, zilianza kwa ushindi hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kujitwalia tiketi kama zikilinda ushindi hadi katika mechi za marudiano.
Real Sociedad wakicheza ugenini, walishinda mabao 2-0 dhidi ya Lyon ya Ufaransa; Plzen nayo ikicheza nyumbani ilishinda 3-1 dhidi ya Maribor huku Pacos Ferreira ya Ureno ikilipuliwa 4-1 na Zenit St Petersburg ya Uswisi.
Kwa kipigo cha 2-0, Lyon inakabiliwa na kibarua kigumu cha kupindua matokeo katika mechi ya marudiano dhidi ya Real Sociedad ya Hispania.
Aidha, Celtic ya Scotland ikicheza ugenini, imeshindwa kufurukuta kwa kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya FC Shakhter Karagandy.
Hata hivyo, timu zilizovuna matokeo mabaya katika mechi za kwanza za juzi na jana, bila kujali zitakuwa ugenini au nyumbani, zitapaswa kubadili matokeo katika mechi za marudiano za usiku wa Agosti 27 na 28.
Timu 10 zitakazoibuka na ushindi wa jumla katika mechi mbili (nyumbani na ugenini) zitaungana na nyingine kutinga kwenye kapu la timu 32 tayari kwa hatua ya makundi kuanza safari ya kupigania ubingwa wa Ulaya.
MATOKEO
Shakhter 2-0 Celtic
Lyon 0-2 Real Sociedad
Paços Ferreira 1-4 Zenit
PSV 1-1 Milan
Plzeň 3-1 Maribor

Lewandowski ajazwa manoti Dortmund

Lewandowski ajazwa manoti Dortmund
KLABU ya Borussia Dortmund imeamua kumaliza mvutano kati yake na mshambuliaji kimataifa wa Poland, Robert Lewandowski, aliyekuwa akitaka kuhama kwa kutoridhishwa na mshahara wake.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na uongozi wa klabu hiyo, nyota huyo aliyetoa mchango mkubwa kwa timu hiyo kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, atalipwa mara tatu ya mshahara aliokuwa akilipwa.
Baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa iliyochezwa Mei 25 kwenye  Uwanja wa Wembley, mjini London ambayo walifungwa na Bayern Munich, Lewandowski akawa lulu lakini akiwekewa ngumu kuhama.
Klabu yake iligoma kumruhusu kwa hoja kuwa ingefanya hivyo mwakani, hivyo nyota huyo kuamua kubaki kwa shingo upande.
Kuhusu maslahi, jarida la michezo la Bild, limedokeza kuwa klabu hiyo imemalizana na nyota huyo kwa kuyafanyia kazi madai yake yote ambayo awali yalikuwa vigumu kutekelezwa.
Licha ya klabu hiyo kukiri kufanyia kazi madai ya mchezaji huyo, ikiwemo kumwongezea mshahara, haijaweza wazi ni kwa kiwango gani.
Hata hivyo, kuna habari kuwa nyota huyo sasa atakuwa akilipwa mshahara wa euro mil 5, badala ya ule wa awali wa euro mil 1.5 kwa mwaka.

58 waomba uongozi TFF

58 waomba uongozi TFF
JUMLA ya wadau wamichezo 58 wamerudisha fomu kuomba kuteuliwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na ule wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Kwa upande wa TFF waliorejesha fomu kwa upande wa urais ni Athuman Jumanne Nyamlani,Jamal Emil Malinzi, Omari Mussa Nkwarulo na Richard Rukambura. Nafasi ya Makamu wa Rais wamejitokeza Imani Omari Madega, Nasib Ramadhan na Walace Karia. 
Walioomba nafasi za ujumbe kuwakilisha kanda mbalimbali ni Abdallah Hussein Mussa, Kaliro Samson, Jumbe Odessa Magati, Mugisha Mujwahuzi Galibona, Vedastus Kalwizira Lufano, Samwel Nyalla, Epaphra Amana Swai, Mbasha Matutu Mong’ateko, Stanslaus Haroon Nyongo, Ally Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omari Walii.
Ahmed Msafiri Mgoyi, Yusuf Hamisi Kitumbo, Ayoub Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja, Ayoub Shaib Nyenzi, Cyprian Charles Kuyava, David Lugenge, Elias Mwanjala, Eliud Peter Mvela, John Mwachendang’ombe Kiteve, James Patrick Mhagama, Kamwanga Rajabu Tambwe na Stanley William Lugenge. 
Athuman Kambi, Francis Kumba Ndulane, Zafarani Damoder, Charles Komba, Hussein Mwamba, Stewart Ernest Masima, Farid Salum Nahdi, Geoffrey Nyange, Riziki Majala, Twahil Twaha Njoki, Davis Elisa Mosha na Khalid Abdallah Mohamed. 
Wengine ni Alex Chrispine Kamuzelya, Juma Abbas Pinto, Muhsin Balhabou, Omar Isack Abdulkadir, Shaffih Dauda Kajuna na Wilfred Mzigama Kidao.
Kwa upande wa uchaguzi wa TFF mwombaji ambaye hakurudisha fomu ni Venance Mwamoto pekee. 
Kwa upande wa TPL Board waliojitokeza kuwania uongozi wa juu ni wawili tu; Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti) na Said Muhamad Said (Makamu Mwenyekiti).
Walioomba nafasi za ujumbe wa TPL Board ni Kazimoto Miraji Muzo, Michael Njunwensi Kaijage, Omari Khatibu Mwindadi, Salum Seif Rupia na Silas Masui Magunguma.