Uchaguzi Mkuu TFF utata mtupu
UWEZEKANO wa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), kufanyika ndani ya kipindi kilichotakiwa na Shirikisho la soka Tanzania
(Fifa), ni mdogo, Tanzania Daima imebaini.
Wakati Fifa wakiagiza uchaguzi huo uwe umefanyika ifikapo
Oktoba 30, lakini marekebisho ya katiba yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa Dharura
Julai 13, yamekwama katika
Ofisi ya Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo.
Japo TFF imepanga uchaguzi huo ufanyika Septemba 29, lakini
suala la Katiba hiyo kukwama kwa Msajili, kunatia shaka kama uchaguzi huo
utafanyika kwa ulitakiwa na Fifa
Wakati kukiwa na ukimya huo, habari zilizoifikia Tanzania
Daima, zinasema kukwama kwa Katiba hiyo katika ofisi ya Msajili, ni kutokana na
dosari mbili kubwa zilizofanywa.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa, dosari ya kwanza ambayo
imeifanya ofisi ya Msajili kusita kupitisha marekebisho hayo, ni staili
iliyotumiwa na Mkutano Mkuu kuipitisha Katiba hiyo.
Kwamba, wakati Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Shirikisho hilo
ikitaka marekebisho yapigiwe kura, kuna habari kuwa jambo hilo halikufanywa na
wajumbe wa mkutano Mkuu.
Kwa mujibu wa kipengere hicho, ili marekebisho yawe halali,
yapaswa kupata baraka ya zaidi ya asilimia 50 ya idadi ya Wajumbe katika
mkutano huo.
“Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya TFF inatamka wazi ili
marekebisho yaweze kuwa halali, yanapaswa kupata baraka ya asilimia 50 + 1 ya
wajumbe walipo ukumbini. Katika uchaguzi ule wa Julai 13, hili halikufanyika,
ilipitishwa kijumla tu,” kilidokeza chanzo chetu.
Habari zinasema, kwa vile jambo hilo halikufanyika katika
upitishaji wa marekebisho hayo, Ofisi ya Msajili imejikuta kwenye wakati mgumu
kuipitisha hadi kufikia jana, akihoji ilipitishwa kwa staili ipi kwani
utaratibu ni wajumbe kupiga kura.
“Ili marekebisho yaweze kuwa halali, yanapaswa kuuungwa
mkono na asilimia 50+ 1 ya idadi ya wajumbe waliohudhuria mkutano husika,”
kinasomeka kifungu hicho cha tatu cha Ibara ya 30 ya Katiba ya shirikishi hilo.
Habari zinasema, japo Ofisi ya Msajili ingependa kuona
mchakato wa uchaguzi huo unafanyika ndani ya kipindi kinachotakiwa na Fifa,
lakini dosari hiyo imeifanya isite kuipitisha katiba hiyo haraka kama
ilivyokuwa imetarajiwa.
Kinachotishia zaidi uchaguzi huo kufanyika kwa wakati, ni
mchakato mzima kuhitaji muda wa siku zisizopungua 60 kabla ya kufanyika kwa
uchaguzi huo, hivyo kama si rasimu hiyo kukwama kwa Msajili, mchakato huo
ungepaswa uwe umeanza walau kuanzia leo.
Aidha, kitendo cha Kamati ya Utendaji kufanya uteuzi wa
Kamati mbalimbali kwa mujibu wa marekebisho yaliyomo kwenye rasimu inayosubiri
baraka za Msajili, ni dosari nyingine ambayo
pia imehojiwa na Ofisi ya Msajili.
“Ofisi ya Msajili imehoji pia uundwaji wa Kamati za Maadili
umefanywa kwa katiba ipi? Inajiuliza hivi kwa sababu marekebisho yaliyofanywa
bado hayajapata baraka kisheria,” kilisema chanzo hicho.
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Msajili, Mercy
Rwezaura kupata kauli yake
juu ya madai hayo, alisema hawezi kusema lolote kwa vile
ofisi yake bado inaendelea kuipitia.
“Kwa sasa siwezi kusema lolote kwa vile bado tunaendelea
kuipitia,” alisema Msajili huyo.
Alipoulizwa juu ya madai kwamba dosari ndizo zimeifanya
ofisi yake ishindwe kupitisha rasimu hiyo kwa wakati, alisema hana taarifa
yoyote na kusisitiza wanaendelea
kuipitia rasimu ya katiba hiyo.
Tanzania Daima lilimtafuta Katibu Mkuu wa TFF, Angetile
Osiah kujua mustakabali mzima wa katiba na mchakato wa uchaguzi huo kwa ujumla,
alisema bado wanasubiri majibu kutoka kwa msajili kabla ya mengine kuendelea.
Kuhusu madai ya dosari ya akidi, Osiah alisema wakati wa
kukabibidhi marekebisho hayo kwa Msajili, waliambatanisha na muhtasari wa
mkutano huo ambao unaonesha kila kitu kilichofanywa na wajumbe wa Mkutano Mkuu.
“Katika katiba tuliyoipeleka kwa Msajili, tuliambatanisha
muhtasari ya wajumbe walioshiriki, sasa sijui idadi ipi inayohojiwa,” alisema
Kuhusu uteuzi wa Kamati mbili mpya za Maadili, Osiah alisema
kwa mujibu wa katiba hiyo hiyo ya TFF, mabadiliko yaliyopitishwa huanza
kutumika mara moja hata kabla ya kupitishwa na Msajili.
Awali, uchaguzi wa Shirikisho hilo ulipangwa kufanyika
Februari 24, mwaka huu, lakini ukaota mbawa baada ya Shirikisho la Soka kutaka
iwe hivyo kutokana na baadhi ya wagombea kulalamika kuchujwa isivyo halali.
Baada ya Fifa kumtuma mjumbe wake, Primo Carvaro kuja nchini
na kupeleka ripoti, ndipo Shirikisho hilo lilipoagiza uundwaji wa Kamati mbili
za Maadili na kutaka uchaguzi uwe umefanyika hadi ifikapo Oktoba 30.
Hata hivyo, habari zinasema pamoja na dosari hizo, Ofisi ya
Msajili yaweza
kuipitisha katiba hiyo kwa sharti la dosari hiyo kifanyiwe kazi
katika Mkutano
Mkuu wa Uchaguzi kama ilivyokuwa uchaguzi wa Desemba 27,
2004.
No comments:
Post a Comment