Mgongolwa amemuangushia
NIMESHANGAZWA na uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji juu ya mchezaji Mrisho Ngasa. Kwamba kamati hiyo imemfungia kucheza mechi sita za mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kumuamuru kurejesha fedha za klabu ya Simba Sh. milioni 30 na fidia ya asilimia 50 ya fedha hizo, kufanya jumla ya Sh. 45 milioni anazotakiwa kuilipa Simba.
Mwenyekiti wa kamati hiyo mwanasheria Alex Mgongolwa amesema wametoa adhabu hiyo dhidi ya Ngasa kwa sababu wamebaini mchezaji huyo aliyesajiliwa na Yanga, alikuwa ameingia mkataba mwingine na Simba wakati akiichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea timu ya Azam ambayo alikuwa na mkataba nayo uliomalizika Mei 31, mwaka huu.
Uamuzi huu ni wa kushangaza sana. Ninashindwa kuelewa kama kamati hii ilifikia uamuzi huu kwa kuongozwa na sheria. Kwanza, hicho kinachodaiwa kuwa mkataba kati ya Ngasa na Simba hakina nguvu ya kisheria ya kuitwa mkataba, hivyo hakikuwa na hadhi ya kujadiliwa na kamati hiyo.
Nasema makubaliano kati ya Ngasa na Simba hayakuwa na nguvu ya kisheria kwa sababu ili makubaliano kati ya mchezaji na klabu yakamilike kuwa nyaraka ya kisheria ni lazima makubaliano hayo yasajiliwe na TFF.
Makubaliano kati ya Ngasa na Simba hayakusajiliwa na TFF, hivyo hayawezi kuwa mkataba wa kisheria kwa mujibu wa kanuni za TFF na hivyo hayawezi kujadiliwa na Kamati ya Mgongolwa (Rejea sakata la Mbuyu Twite na Simba).
Pili, makubaliano kati ya Ngasa na Simba hayana nguvu za kisheria kwasababu wakati Ngasa akisaini makubaliano hayo na Simba, tayari alikuwa na mkataba mwingine na Azam ambao ulikuwa katika makabati ya TFF.
Kwahiyo, kisheria mkataba unaotambulika ni ule wa kwanza kati ya Ngasa na Azam. Kwanini leo kamati ya Mgongolwa iseme Ngasa alikuwa ameingia mkataba na Simba ilihali yale yalikuwa makaratasi tu yasiyo na maana yoyote?
Kamati ya Mgongolwa haikupaswa kujadili suala hili na kulitolea maamuzi. Hayo yalikuwa makubaliano ya kihuni yaliyofanyika uchochoroni, hivyo Kamati ya Mgongolwa ingewaambia Simba na Ngasa waende wakamalizane huko huko uchochoroni.
Hata kama makubaliano hayo yanachukuliwa kuwa mkataba halali, basi haliwezi kuwa kosa la Ngasa pekee yake. Wote wawili, mchezaji na klabu ya Simba wana makosa kwa mujibu wa kanuni za Fifa.
Kosa la Simba ni kufanya mazungumzo na kuingia mkataba na mchezaji wa timu nyingine bila klabu inayommiliki kuwa na taarifa. Kwanini leo Ngasa aadhibiwe pekee yake? Wote walipaswa kuadhibiwa. Chelsea na mchezaji Ashley Cole waliwahi kuadhibiwa baada ya kubainika kufanya mazungumzo bila kibali cha timu ya Arsenal iliyokuwa ikimmiliki mchezaji huyo.
Halafu Kamati ya Mgongolwa imemhukumu Ngasa kukosa mechi sita, kwa kosa gani hasa? Ni kanuni ipi ya TFF au Fifa iliyowaongoza kufikia adhabu hiyo? Ngasa na Simba walipaswa kuhukumiwa kulipa faini kwa kosa la kufanya mazungumzo na kuingia mkataba bila kibali cha Azam.
Kitu kingine kinachozusha maswali na kutia shaka uhalali wake ni adhabu aliyopewa Ngasa na Kamati ya Mgongolwa ya kutakiwa kulipa fidia ya asilimia 50 ya fedha alizopewa na Simba Sh. milioni 30. Fidia ya asilimia 50 ipo kisheria? Suala la riba linaongozwa na sheria za fedha za Benki Kuu na siyo suala la kuamua tu unavyotaka.
Isitoshe, adhabu hii inayapa nguvu za kisheria makubaliano ya Simba na Ngasa na kuyafanya kuwa mkataba halali wa kisheria, na hivyo kumfanya Ngasa aonekane amesaini
timu mbili, Simba na Yanga. Kwanini sasa Kamati ya Mgongolwa imuidhinishe kuchezea Yanga wakati alianza kusaini Simba? Huu ni uamuzi wa fedheha kwa kosa letu.
No comments:
Post a Comment