Azam Tv yacheuwa mabilioni Ligi Kuu
Baadhi ya viongozi wa TFF na Azam wakitiliana saini |
KAMATI ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana imesaini
makubaliano ya kuuza haki za kuonesha mechi za Ligi Kuu kwa Kampuni ya Azam
Media Ltd kupitia kituo cha televisheni cha Azam Tv
kwa kipindi cha misimu mitatu, kuanzia msimu wa 2013/14 utakaoanza Agosti 24.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa
TFF, Ilala jijini Dar es Salaam, Azam Media itamwaga kitita cha shilingi
bilioni 5.560 ikiwa nji thamani ya mkataba huo ambao utasainiwa ndani ya siku 30 kuanzia jana.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi,
Wallace Karia, alisema kulikuwa na ofa nyingi
za zabuni ya kuonesha mechi za Ligi Kuu - zikiwamo kutoka
nje ya nchi, lakini ofa ya Azam ni nono zaidi na kuongeza watatoa asilimia 25
kabla ya kuanza ligi.
Wallace alitumia fursa hiyo kuishukuru Azam kukubali kununua
haki hiyo kwa ofa nono iliyozipiku kampuni kadhaa zikiwamo kongwe za kimataifa
na kwamba wanajivunia kufanya kazi na kampuni ya kizawa iliyojitoa katika
uwekezaji katika soka.
Akinuzngumza kwa niaba ya Rais wa TFF, Makamu wa Pili wa
Rais Athumani Nyamlan aliwapongeza Azam Media Ltd kushinda manunuzi ya haki za
kuonesha mechi za ligi kupitia kituo cha televisheni cha Azam Tv.
“Udhamini huu wa Azam Media Ltd, unastahili kupongezwa, hasa
ukizingatia unakuja kipindi ambacho Tanzania
kama taifa limeshaanza kunufaishwa na
uwekezaji wa Kampuni SSB, ikiwamo kupitia michuano ya vijana ya Uhai Cup,”
alisema Nyamlani.
Aliongeza kwamba Azam imefanya mengi ya kuigwa katika soka
la Tanzania ,
lakini mkataba huu wa kwanza kwa kampuni ya nyumbani, unathibitisha utayari
iliyonao SSB katika kusaidia harakati chanya za kunyanyua juu maendeleo ya soka
nchini.
Akizungumza baada ya kutiliana saini kwa makubaliano hayo,
Meneja wa Azam Media, Mzee Said Mohamed, alisema wamejipanga kufanya vitu
vikubwa kupitia makubaliano hayo na kwamba kila Mtanzania atafurahia matangazo
bora kupitia Azam Tv itakayozinduliwa Agosti 1.
Alibainisha kuwa, uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 30 wa
kuanzishwa kwa Azam Tv chini ya Azam Media, unawapa uhakika wa matangazo bora
ya televisheni, ili kushinda vita ya pili ambayo ni ya ubora wa huduma zake kwa
wateja hususani wapenzi wa soka.
“Nia ya makubaliano haya na mkataba baina ya Azam Media na
Kamati ya Ligi wa haki za kuonesha mechi za Ligi Kuu, ni kunyanyua maendeleo ya
soka letu kwa mchezaji mmoja mmoja, klabu na hatimaye taifa kwa ujumla,”
alisema Mzee Said.
Alisema kuwa, Azam Tv itahakikisha katika msimu huu wa
kwanza, angalau kila klabu inaoneshwa mechi zake mara nne na kwamba kituo hicho
kitarusha moja kwa moja (live) jumla ya mechi 60, huku zingine 82 zikioneshwa
baada ya kurekodiwa (Recorded).
Aliongeza kuwa, licha ya msimu huu kutarajia kutoa shilingi
milioni 25 za maandalizi kwa kila klabu shiriki kama makubaliano hayo
yanavyowaongoza, matarajio yao
ni kuwa baada ya kumalizika kwa mkataba wa sasa, kila klabu kupata milioni 100
za maandalizi.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Azam Media Ltd inamiliki
haki ya kufanya maelewano na kituo chochote cha televisheni ndani na nje ya
nchi, ili kuweza kuonesha ‘live’ au marudio ya mechi za ligi kuanzia msimu huu
wa 2013/14 unaoanza Agosti 24.
Mzee Saidi alibainisha kuwa, Azam Media Ltd itatoa asilimia
25 ya thamani ya mkataba kabla ya kuanza msimu huu, huku akifichua kuwa
wamefurahishwa kushinda zabuni ya haki ya kuonesha Ligi Kuu na kuzipiku kampuni
kubwa ambazo hata hivyo hazikutajwa.
Kusainiwa kwa makubaliano hayo, kumefuatia mazungumzo kati
ya Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu za Ligi Kuu, ambapo mkataba huo utazipunguzia
mzigo klabu ambazo zimekuwa zikisumbuliwa na ukata kwa kutegemea udhamini wa
Vodacom peke yake, ambao hautoshi.
No comments:
Post a Comment