Stars yaapa kufia
Uganda
Wachezaji wa Taifa Stars wakiwa katika mazoezi yao ya mwisho kabla ya mechi na Uganda |
WAKATI timu ya soka ya Tanzania ,
Taifa Stars inashuka dimbani leo kuwakabili Uganda Cranes katika mechi ya
kuamua tiketi ya kwenda Afrika Kusini kwa fainali za Afrika kwa nyota wa ndani
(CHAN) hapo mwakani, Kocha
Kim Poulsen amesema kazi kubwa kwa vijana wake ni kupambana
mwanzo mwisho kupata mabao ya mapema.
Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya bia kupitia kinywaji
chake cha Kilimanajro Premium Lager, inawakabili Uganda
ikiwa nyuma kwa bao 1-0 walilofungwa katika mechi ya kwanza baina yao iliyochezwa Julai 13, jijini Dar es Salaam .
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Kampala jana kuhusu kikosi chake, Poulsen
alisema vijana amejiandaa vizuri na kwamba licha ya kuwa ni mwezi mgumu kisoka
kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa kwenye mfungo, wachezaji wamepania kupata
matokeo mazuri.
“Tunajua watanzania wengi walikataa tamaa au kupoteza
matumanini baada ya sisi kufungwa 1-0, lakini katika mpira haya yanaweza
kubadilika…tukifunga bao kesho litabadilisha kila kitu,” alisema Poulsen.
Alikiri kuwa mechi hii ya marudiano ni ngumu kwani Stars
itakuwa inacheza na timu bora Afrika Mashariki
lakini lolote linaweza kutokea ndani ya dakika 90 au zaidi
za mchezo.
Alisema licha ya kuwakosa wachezaji Shomari Kapombe na
Mwinyi Kazimoto, maandalizi ni mazuri na hasa walipokuwa kambini Mwanza
wachezaji walionesha bidii sana
katika mazoezi.
Alisema katika mechi ya kesho watajitahidi kutengeneza
nafasi nyingi na kufunga magoli. “Katika mazoezi yetu tumefanya mazoezi sana katika ushambuliaji,
kutengeneza nafasi na kufunga magoli,”alisema huku akiongeza kuwa mabeki
watahakikisha washambuliaji wa The Cranes hawapiti kabisa.
Aliwataka watanzania wawe na imani na timu ya Taifa kwa
matokeo yoyote yatakayopatikana kesho kwani mpira ni safari na kukubali matokeo
ni sehemu ya mchezo.
“Wachezaji wana ari ya kupata ushindi ili waende CHAN
mwakani kwani hii itawapa nafasi nzuri ya kuonekana na vilabu kubwa duniani na
tayari tumeona jinsi watu wengi wametambua kuwa kuna wachezaji wazuri Tanzania ….Kapombe ameenda kwenye majaribio
Uholanzi, Kyemba naye yuko njiani na nasikia Kazimoto yuko Qatar ..nawatakia kila la heri.”
Alisema.
Poulsen alisema Jumatatu atazungumza na waandishi wa habari
kuhusu mipango ya muda mrefu ya Taifa Stars.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya
Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, ambaye Bia yake inadhamini Taifa
Stars alisema wao kama wadhamini wanawaomba
watanzania wawe na imani na stars na waiombee ifuzu mashindano ya CHAN.
“Sisi kama wadhamini tuna imani na timu yetu na tuna imani
watafanya maajabu katika mechi ya kesho ili wawape raha watanzania,” alisema
Kavishe.
Kilimanjaro Premium Lager imewekeza zaidi ya shilingi
bilioni 2 kwa mwaka kuidhamini timu ya Taifa kwa mkataba wa miaka mitano.
Cranes inawakabili Stars leo ikiwa
na tatizo la ufungaji kwani katika mechi mbili za kirafiki ilizocheza na vijana
wa chini ya miaka 23 na kufungwa zote kwa bao 1-0 ambazo Denis Iguma
aliyewafungia bao Julai 13, alichezeshwa sehemu ya kiungo.
Micho atawakosa wachezaji
wake wawili wa mbele, Tony Odur na
Patrick Edema. Wakati Odur anauguza nyonga, Edema amekwenda Ureno kwa
majaribio.
Katika kuziba pengo, Micho
amewaita Simon Okwi (KCC FC), David Kasirye (URA FC) na Henry Oguti anayechezea
Kiira Young.
Hata hivyo, Okwi ameitwa
licha ya kushindwa kufungia bao KCC msimu uliopita huku kukiwa na shaka juu ya
kiwango cha Kasirye.
Mazingira hayo yanamfanya Micho amtegemee Oguti
kuongoza safu ya ushambuliaji anayeonekana kuwa na nguvu kuliko wengine ingawa
kuna mwingine kama Frank Kalanda.
No comments:
Post a Comment