Saturday, July 27, 2013

Bolt hashikiki London
BINGWA mara sita wa michuano ya Olimpiki, Usain Bolt, ameendeleza msimu kwa ushindi katika mbio za mita 100, wakati aliporejea kwa kishindo kwenye Uwanja wa Olimpiki jijini hapa katika maadhimisho ya mwaka mmoja baada ya michuano hiyo.
Juzi, katika sherehe za mwaka mmoja tangu ufunguzi wa michuano ya Olimpiki ya Kiangazi mwaka jana 2012 jijini hapa, Bolt alilipa fadhila ya ushindi wake wa dhahabu ya michuano hiyo kwenye dimba la Olimpiki kwa kukimbia akitumia sekunde 9.85.
Mwingereza James Dasaolu alijitoa kabla ya kuchuana na Bolt katika umbali huo kutokana na majeruhi yanayomkabili.
Mmarekani Michael Rodgers alikamata nafasi, huku Mjamaica mwenzake Nesta Carter akikamata nafasi ya tatu akitumia sekunde 9.99, wakati Mwingereza pekee katika mbio hizo Dwain Chambers, akimaliza wa tano kwa sekunde 10.10.
Bolt, ambaye anatarajiwa kuutetea ubingwa wa dunia wa mita 100 mwezi ujao jijini Moscow, Russia, alionekana mwenye furaha kuu kushinda mbio hizo mbele ya mashabiki 60,000.
“Ni jambo zuri la kuvutia kushiriki mashindano jijini London, ni uzoefu wa aina yake kwa mimi kuwa hapa kwa mara nyingine," alisema Bolt kwa furaha, huku akiongeza kuwa yampasa kufanya kazi kwa bidii kuelekea kutetea ubingwa wa dunia.
"Uanzaji wangu wa mbio ulikuwa mbovu na nahitaji kulifanyia kazi hilo. Ili kuwa na mbio nzuri, nahitaji kuanza vema na kumaliza kwa ushindi. Ninatumaini kuwa nitakuwa na kipindi kizuri jijini Moscow na kuendelea kufanya vema mchezoni,” alisisitiza Bolt.

No comments:

Post a Comment