Saturday, July 27, 2013

Brandts wa Yanga achota ujuzi Uefa 
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts
KOCHA Mkuu wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, Ernie Brandts, kesho Jumatatu anatarajia kuwa mmoja wa makocha watakaohudhuria kozi ya mafunzo ya na kuongeza muda wa leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) itakayofanyika nchini Ujerumani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye tovuti ya klabu hiyo jana, Brandts atakuwa mmoja wa washiriki wa kozi hiyo kwa ngazi ya Daraja la Kwanza, itakayofanyika kwa siku tatu kuanzia Jumatatu Julai 29 hadi Julai 31.
Taarifa hiyo imeongeza, baada ya kozi hiyo Brandts anatarajia kurejea nchini Agosti 1, kuendelea na maandilizi
ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom na michuano ya klabu barani Afrika, ambako Yanga inacheza Ligi ya Mabingwa.
Brandts amekwenda kuhudhuria kozi hiyo ya Uefa, ambayo hutolewa kila baada ya miaka miwili kwa makocha wenye leseni zinazotambuliwa na shirikisho hilo kwa ajili ya kuongeza muda (uhai) wa leseni hizo.
Uongozi wa klabu ya Yanga umebariki safari ya mafunzo kwa kocha Brandts, ukiamini itamuongezea ujuzi atakoutumia kuijenga timu, ikiwamo kuipa uwezo wa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kung’ara katika mashindano ya klabu Afrika.
Brandts alijiunga na Yanga mwaka jana akitokea kuinoa APR ya Rwanda, ambapo katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom ameiwezesha kutwaa ubingwa uliokuwa ukishikiliwa na watani wao wa jadi, Simba.
Yanga inatarajia kucheza mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Makamu Bingwa, Azam FC hapo Agosti 17 kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kurejea tena dimbani hapo Agosti 24 kucheza mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Ashanti United ya Ilala iliyorejea msimu huu kutoka Lifi Daraja la Kwanza.

No comments:

Post a Comment