Saturday, July 27, 2013

Bale aipigia magoti Spurs 
WINGA wa kimataifa wa Wales, Gareth Bale, amewaomba maofisa wa klabu yake ya Tottenham kumruhusu ajiunge na klabu ya Real Madrid ya Hispania.
Tamko la Bale limekuja saa chache baada ya miamba hiyo ya soka ya Hispania kupandisha dau la ofa yake na kufikia ada rekodi ya dunia ya pauni milioni 81, ambalo pia limeonekana kupuuzwa na Spurs.
Gazeti la Marca la nchini Hispania, ambalo liko karibu mno na vyanzo vya ndani klabuni Santiago Bernabeu, limedai kuwa Bale aligeuka mbogo kwa maofisa wa klabu yake kwa kuonesha dharau kwa donge nono.
Hasira za Bale zinatokana na Madrid kuonesha nia ya dhati ya kupata saini yake, kwa dau linalovunja rekodi iliyowekwa na Cristiano Ronaldo alipoihama Manchester United kujiunga na Madrid, Julai 2009.
Bale, 24, anaamini kuwa kunahitajika kukosa uelewa kwa Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy na klabu yake kukataa dau kubwa kama hilo kwa ajili yake.
Gazeti la Marca limedai kuwa, Bale amevunja ukimya na kumwambia Mwenyekiti wake Levy: “Kumbuka ulichoniahidi. Uliniahidi kuwa kama Spurs haitofuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kisha kukaja ofa nzuri utakuwa tayari kuisikiliza.
“Naam, hatimaye ofa rekodi ya dunia imewasili na kimsingi nataka kuichezea Real Madrid. Hivyo unapaswa kutoa ridhaa na kuingia katika mazungumzo ya makubaliano,” amekaririwa Bale akimwambia mwenyekiti huyo wa Spurs.
Bale alikutana na Levy na kuweka wazi kutoona mwanga katika matarajio yake klabuni hapo na imetabiriwa kuwa dau nono zaidi ya hapo linaweza kuvunjika mahusiano ya winga huyo na Bodi ya Spurs kama wataendelea kumbania.

No comments:

Post a Comment