Tuesday, July 23, 2013

Fabregas aitesa Man Utd

KAMA kuna kipindi ambacho Manchester United imewahi kuteseka katika usajili, basi ni sasa katika juhudi za kupata sahihi ya kiungo wa kimataifa wa Hispania, Cesc Fabregas ambapo kutokana na ugumu, imepanda hadi pauni mil 41.
United imepanda haki kiasi hicho baada ya ofa zake mbili ikiwemo ya hivi karibuni ya pauni milioni 35 kutupwa na Barcelona ikisema haina mpango wa kumuuza na Fabregas anapenda kubaki Camp Nou.
Mbali ya kiasi hicho, United pia ilikuwa tayari kumtoa mchezaji katika mpango huo ili kumpata Fabregas, lakini bado Barcelona wakatupa ofa hiyo hivyo kuikata maini Arsenal iliyokuwa ikimtaka kwa pauni mil 29.   
Ugumu wa Barcelona kumtoa Fabregas kwa United umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuondokewa na Thiago Alcantara aliyetimkia Bayern Munich ya Ujerumani akimfuata Kocha Pep Guardiola. 
Kuondoka kwa Thiago, kunatoa nafasi kubwa kwa Fabregas kupata namba kwenye kikosi cha kwanza kusaidiana na Xavi chini ya kocha mpya Gerardo 'Tata' Martino.
Hata hivyo, kutokana na United kutokuwa na uhakika wa ofa hiyo ya tatu kukubaliwa na Barcelona, wamepanga kumshawishi Fabregas kwa mshahara wa euro 233, 000 kwa wiki.
Moyes alisema juzi kuwa wameongeza dau hilo kutokana na mazingira magumu ya kumshawishi kiungo huyo kwenda Old Trafford ikiwemo shauku ya Barcelona kutaka abaki Camp Nou baada ya Thiago kuondoka huku kukiwepo presha kutoka klabu nyingine kama Arsenal.
Moyes alisema hilo ni jaribia la mwisho kwao katika kumwania nyota huyo anayewindwa vikali ikiwemo Arsenal aliyowahi kuichezea kwa mafanikio makubwa hadi kuwa nahadha wake, lakini mwaka 2011 akaondoka kurejea Barcelona alikocheza soka yake ya utoto.
"Hii ni ofa ya mwisho kwetu katika kushawishi Fabregas ajiunge nasi japo klabu yake Barcelona imekuwa ikiweka ngumu, lakini ofa yetu ya pili tuliituma siku ambayo Tito Vilanova alitangaza kuachia ngazi kutokana na sababu za kiafya,” alisema Moyes.
Nje ya Fabregas, United imekuwa ikisaka saini za nyota wengine kama Luka Modric, Yohan Cabaye na Marouane Fellaini kwa lengo la kuimarisha safu ya ushambuliaji na kiungo.
Kiasi cha pauni mil 41, ni dau la tatu kwa United katika harakati za kumpata Fabregas kwani ofa ya kwanza ilikuwa ni pauni mil 29 kama Arsenal kabla ya kupanda hadi 35. 
Fabregas alirejea Barcelona mwaka 2011 baada ya kucheza Arsenal kwa miaka nane, lakini amekuwa hana uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza Camp Nou, akicheza mara 32 na kufunga mabao 11 na kuchangia 11.

No comments:

Post a Comment