Safari ya Azam ‘Sauzi’ yaiva
SHIRIKISHO la soka Tanzania
(TFF) limebariki ziara ya Azam FC (pichani) nchini Afrika Kusini kujifua kwa wiki mbili
kabla ya kurejea tayari kwa msimu mpya wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 24.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa
Klabu hiyo, Idrisa Nassoro, Azam itakayoondoka Agosti 2, itacheza mechi tatu za
kirafiki ambapo baada ya kurejea itacheza mechi ya Ngao ya Hisani Agosti 17,
ikiwa ni ufunguzi wa msimu mpya.
Nassoro alisema, maandalizi
ya safari hiyo yamekamilika kwani wachezaji wote wapo tayari isipokuwa
wachezaji wawili Brian Umonyi na Anfrey Mieno ambao watabaki kutokana na kuwa majeruhi.
“Kila kitu kimekamilika
tumebakia kuondoka tu, TFF wana taarifa juu ya safari yetu. Umonyi anasumbuliwa
na maumivu ya msuli huku Mieno akiwa na maumivu ya kifundo cha mguu,” alisema
Nassoro.
Alisema kukawia kwa safari
yao ilikuwa ni kusubiri uhakika wa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu pia baadhi ya
nyota wao kuwemo kwenye kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars
inayokabiliwa na mechi dhidi ya Uganda itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii mjini
Kampala.
Akizungumzia ziara hiyo, Katibu
Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikiri kupata barua ya ziara ya Azam na kuwatakia
kila la kheri katika ziara hiyo kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu.
Mbali ya Ligi Kuu ya Bara,
Azam chini ya Kocha wake Stewart Hall, inakabiliwa na michuano ya Kombe la
Shirikisho kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo licha ya kucheza mara ya
kwanza, ilifika hadi raundi ya pili iking’olewa na FAR Rabat ya Morocco.
No comments:
Post a Comment