Kim ahofia saumu Stars
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya
Tanzani, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema vijana wake wameiva kuwakabili Uganda
kwenye mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la
Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayochezwa Jumamosi, jijini Kampala.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Mwanza jana, Kim amesema tangu kikosi chake kimeingia kambini
Julai 14, wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mazoezi na wako tayari kwa
mechi hiyo.
“Uganda ni timu bora kwa
ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Mechi itakuwa ngumu, tunaamini
tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo mikakati kwa ajili ya mechi hiyo,
tunakwenda kuikamilisha Kampala,” alisema Kim.
Hata hivyo, Kim amesema licha
ya mwitikio mzuri wa wachezaji kwenye mazoez, lakini wanakabiliwa na changamoto ya wengi wao
kuwa wamefunga wakati wachezaji wanapokuwa kambini wanatakiwa kula, kunywa na
kupumzika.
“Hiki ni kipindi kigumu
kisoka, suala la kufunga ni la kiimani ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji
kufunga. Karibu nusu ya wachezaji wanafunga, hii ni changamoto ambayo
tunaiheshimu,” amesema Kim na kuongeza ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa
na mabadiliko baada ya beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini
Uholanzi.
Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager inaondoka Mwanza leo saa 7.25 mchana kwa ndege ya
PrecisionAir na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15
mchana.
Nyota waliomo kwenye msafara
huo ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris,
David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
Viungo ni Amri Kiemba,
Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum
Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho
Ngasa.
Stars inakwenda Uganda ikiwa nyuma
kwa bao 1-0 walilofungwa katika mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 13, kwenye
Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Julai 13; huku mshindi wa jumla baina yao
atajitwalia tiketi ya kwenda Afrika Kusini kwa fainali za mwakani.
No comments:
Post a Comment