Sunday, July 21, 2013

Fabregas, Ronaldo na Rooney
Fab, Rooney, Ronaldo wamtesa Moyes
MRITHI wa Sir Alex Ferguson, David Moyes, anapitia kipindi kigumu katika timu ya Manchester United kutokana na kukabiliwa na vita ya kumbakisha Wayne Rooney huku akiwatamani Cesc Fabregas wa Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid.
Kocha huyo yuko katikati ya shinikizo kutoka kwa Chelsea, Barcelona na Real Madrid kuwahusu nyota hao watatu.
Chelsea wameongeza presha kwa Moyes baada ya kusema wapo tayari kumtwaa Rooney
kwa dau la pauni milioni 24 huku yeye akiboresha ofa ya kumpata Fabregas hadi pauni milioni 30.
Wakati hajajua majaaliwa ya Rooney na ujio wa Fabregas Old Trafford ukiota mbawa kutokana na kung’ang’aniwa na Barcelona na yeye kusema yu tayari kubaki, Moyes amechanganyikiwa kwani hata Madrid wamesema hawana mpango wa kumtoa Ronaldo.
Carlo Ancelotti wa Real Madrid, amemwaga dharau kwa Man United juu ya mpango wao wa kumrejesha winga huyo wa Kireno Old Trafford, akisema anawaza kusaini mkataba mpya Bernabeu.
Bosi wa Chelsea, Jose Mourinho amevuta kasi ya aina yake katika jaribio la kumng’oa Rooney na kupandisha dau lake kutoka pauni milioni 20 mapema wiki jana hadi kufikia pauni milioni 24 licha ya Moyes kukana kumuuza.
Kubwaga manyanga kuinoa Barca kulikofanywa na kocha Vilanova, kunailazimisha miamba hiyo ya Nou Camp kuachana na wazo la kumuzaa Fabregas, mshindi wa Kombe la Dunia, hadi itakapojua kocha mpya na mahitaji yake kikosini.
Kutokana na kuyumba kwa jaribio la kumnasa Fabregas na kumbakisha Rooney, maelezo ya Ancelotti kuhusu Ronaldo si habari nzuri kusomwa au kusikiwa Moyes, ambaye alikuwa na matumaini makubwa akishirikiana na Fergie kupata saini ya Mreno huyo.
Ancelotti aliyerithi mikoba ya Jose Mourinho aliyetimkia Chelsea, alimmwagia sifa nyota wake huyo aliyedai kuwa anaweza kuwa msukumo kwa nyota vijana  klabuni Bernabeu.
Mtaliano huyo alisema: “Cristiano ni nyota wa daraja la juu. Ni mchezaji mkubwa. Kwa klabu hii, jambo muhimu ni kuhesabu wachezaji wakali wa kulipwa waliopo. Wachezaji vijana humuangalia bingwa katika kuhakikisha wanafanya kama yeye.
“Sio jukumu langu linapokuja suala la kumpa mkataba mpya kubaki hapa, lakini sidhani kama kunaweza kuwa na tatizo lolote katika hilo,” alimaliza kocha huyo aliyeipa ubingwa wa Ligue 1 klabu ya PSG na kutimkia Bernabeu.

No comments:

Post a Comment