Tito Vilanova |
Guardiola amhurumia Vilanova
KOCHA wa Bayern Munich ya hapa, Pep Guardiola, ameelezea
masikitiko aliyonayo, kutokana na changamoto ngumu itokanayo na maradhi ya
kansa ya tezi iliyomlazimisha swahiba wake Tito Vilanova kubwaga manyanga
kuinoa FC Barcelona.
Akizungumza baada ya taarifa ya Vilanova kujiuzulu,
Guardiola alikiri kuumia moyo kiasi cha kushindwa kuzungumza lolote akiwa nje
ya Hispania; jambo linalomhusu nduguye huyo aliyekuwa akimsaidia kabla ya kurithi mikoba yake.
“Ni vigumu mno kwangu kuzungumzia suala hili kwa hapa Ujerumani.
Vilanova ni zaidi ya rafiki yangu wa karibu na niseme ukweli kuwa nampenda
sana,” alisema Guardiola alipokuwa akihojiwa na vyombo vya habari vya Hispania.
Guardiola aliongeza: “Naweza tu kusema kwamba namtakia kila
la heri yeye na familia yake katika kukabiliana na kipindi hiki kigumu. Hili ni
jambo gumu sana kwangu.”
Alionekana kukwepa kuzama zaidi kuhusu Vilanova.
Wawili hao hawakuwa na mawasiliano mazuri katika siku za
karibuni, baada ya kuzaliwa kwa vita ya maneno iliyoibuliwa na Guardiola,
akiilalamikia bodi ya Barca kuyatumia maradhi ya Vilanova kumchafua.
Katika madai yake, Guardiola alikuwa akikana madai ya
viongozi wake hao wa zamani kuwa licha ya Vilanova kufanyiwa upasuaji,
Guardiola hakuwa na muda wa kumtembelea wodini alikolazwa licha ya kuishi New
York alikokuwa anaugulia.
“Sitokuja kusahau kuwa wao walitumia maradhi ya Vilanova
kuniathiri mimi na kunichafua, kwa sababu ilikuwa ni uongo wa dhahiri kwamba
mimi sikuwahi kumtembelea hospitalini jijini New York,” alisema Guardiola.
Vita ya maneno baina ya wawili hao ikaibuka hivi karibuni,
baada ya Vilanova kuwatetea mabosi wake hao kwa kusema hakuna hata mtu mmoja
miongoni mwa bodi ya klabu hiyo aliyetumia maradhi yake ya kansa kumshambulia
Guardiola.
Vilanova alikaririwa akisema: “Pep amefanya vibaya na
kimsingi imenishangaza sana kutokana na maelezo yake. Hakuna yeyote katika bodi
klabu aliyetumia maradhi yangu kumshambulia yeye kama alivyodai.
Na Vilanova akaongeza: “Guardiola alinitembelea mara moja tu
toka nilipowasili jijini New York, lakini baada ya operesheni nikawa naugulia
huko kwa miezi miwili na sikuwahi kumuona akinitembelea tena.
“Guardiola ni rafiki na ningali namhitaji sana, lakini
kusema ukweli hakuwa kule kwa ajili yangu. Ningependa kufanya mambo tofauti.
Sitaki kusema lolote zaidi kuhusu hili,” alimaliza Vilanova kuungana na
ukosoaji kuwa Guardiola hakumjali.
No comments:
Post a Comment