Wednesday, August 21, 2013

AC Milan yabanwa, Zenit yaua Ulaya

AC Milan yabanwa, Zenit yaua Ulaya
 Stephan El Shaarawy kushoto akishangilia bao lake pamoja na Abate
MABINGWA mara saba wa Ulaya, AC Milan ya Italia, jana ilivuna sare ya ugenini ya bao 1-1 dhidi ya PSV Eindhoven ya Uholanzi katika mechi ya kwanza ya mtoano kuwania tiketi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakicheza ugenini, Milan walitangulia kupata bao kabla ya wenyeji kusawazisha kutokana na makosa ya kipa Christian Abbiati, hivyo kutanguliza mguu mmoja hatua ya makundi kama itaulinda ushindi huo hadi marudiano.
Milan walipata bao kupitia kwa nyota mwenye asili ya Misri, Stephan El Shaarawy aliyefunga kwa kichwa kabla ya Tim Matavz kuisawazishia PSV.
Katika mechi nyingine za kuwania tiketi ya 32, Real Sociedad, Zenit St Petersburg na Plzen ya Czech, zilianza kwa ushindi hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kujitwalia tiketi kama zikilinda ushindi hadi katika mechi za marudiano.
Real Sociedad wakicheza ugenini, walishinda mabao 2-0 dhidi ya Lyon ya Ufaransa; Plzen nayo ikicheza nyumbani ilishinda 3-1 dhidi ya Maribor huku Pacos Ferreira ya Ureno ikilipuliwa 4-1 na Zenit St Petersburg ya Uswisi.
Kwa kipigo cha 2-0, Lyon inakabiliwa na kibarua kigumu cha kupindua matokeo katika mechi ya marudiano dhidi ya Real Sociedad ya Hispania.
Aidha, Celtic ya Scotland ikicheza ugenini, imeshindwa kufurukuta kwa kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya FC Shakhter Karagandy.
Hata hivyo, timu zilizovuna matokeo mabaya katika mechi za kwanza za juzi na jana, bila kujali zitakuwa ugenini au nyumbani, zitapaswa kubadili matokeo katika mechi za marudiano za usiku wa Agosti 27 na 28.
Timu 10 zitakazoibuka na ushindi wa jumla katika mechi mbili (nyumbani na ugenini) zitaungana na nyingine kutinga kwenye kapu la timu 32 tayari kwa hatua ya makundi kuanza safari ya kupigania ubingwa wa Ulaya.
MATOKEO
Shakhter 2-0 Celtic
Lyon 0-2 Real Sociedad
Paços Ferreira 1-4 Zenit
PSV 1-1 Milan
Plzeň 3-1 Maribor

No comments:

Post a Comment