KOCHA wa zamani wa Anzhi Makhachkala, Rene Meulensteen, amesema hatashangazwa kusikia nyota wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o, anajiunga na Chelsea ya England inayonolewa na Jose Mourinho, raia wa Ureno.
Rene aliyewahi pia kuinoa Manchester United ya England, amesema kwa mazingira ya sasa ya Chelsea, hatashangazwa kuona Eto’o akiihama Anzhi na kujiunga na timu hiyo.
Uwezekano wa Eto’o kuondoka ni mkubwa kutokana na wengi kutamani kufanya hivyo wakihofia mwelekeo wao hasa baada ya mmiliki wa Anzhi, Suleyman Kerimov kuamua kupunguza matumizi ya uendeshaji wa timu.
Kitisho hicho ndicho pia kimemfanya mchezaji nyota wa kimataifa wa Brazil, Willian Borges da Silva kuwa kwenye mchakato wa kujiunga na Tottenham ya England kwa kitita cha pauni mil 30.
Chini ya mazingira hayo, haitashangaza kusikia Eto’o akithibitisha ambacho kimekuwa kikizungumzwa kwa muda mrefu kuwa anatamani kumfuata Mourinho kutokana na kuwahi kupata naye mafanikio makubwa akiwa Inter Milan ya Italia.
Meulensteen, mwenye rekodi ya kuinoa Anzhi kwa siku 16 kabla ya kutimuliwa, amesema Eto’o hawezi kubaki kwenye klabu hiyo na ligi pekee ambayo angependa kuicheza ni Ligi Kuu ya England hasa katika klabu ya Chelsea.
Kauli ya kocha huyo inakuja huku Mourinho akisema bado anasaka mshambuliaji katika kikosi chake na kuongeza kuwa hesabu zake hazipo kwa Wayne Rooney wa Manchester United, hivyo anaweza kusajili popote.
No comments:
Post a Comment