SIKU moja baada ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya hapa, kocha wa Chelsea, Jose Mourinho ameibuka na kuapa kwamba ataachana na jukumu lake klabuni Stamford Bridge kama hatoweza kutwaa mataji.
Mourinho, Mreno anayependa kujiita Special One, alitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya Barclays katika kipindi chake cha kwanza kuinoa Blues na sasa amerejea kwa mara ya pili kuwanoa mabilionea hao wa Magharibi mwa jiji hili.
Lakini sasa, Mourinho anaahidi kujiweka kando katika jukumu la kuinoa Chelsea, kama ataendeleza ukame wa mataji ulioanzia Santiago Bernabeu yaliko makazi ya klabu ya Real Madrid, ambako alimaliza msimu uliopita bila kikombe.
"Bila shaka, katika suala la kutwaa mataji. Hakuna mabadiliko katika DNA yangu, sijabadilika chochote pia katika asili yangu," alisema kuwaambia wanahabari wakati wa maandalizi ya mwisho kuelekea mechi yao ya jana.
Mourinho aliongeza: "Mimi si aina ya mtu ninayeweza kukaa katika klabu moja kwa misimu mitatu au minne bila kutwaa taji lolote.
"Katika hilo, mimi sihitaji klabu kuniambia 'hatuna furaha kuwa na wewe, kwaheri'.
"Mimi nitakuwa wa kwanza kusema 'nimejitoa kwa kila nilichoweza, lakini sijapata mafanikio, hivyo acha kila mmoja baina yetu awe kivyake na kujaribu mambo kivingine'," alijinasibu Mourinho.
No comments:
Post a Comment