MSHAMBULIAJI wa FC Barcelona, Lionel Messi amekanusha dhana iliyoshamiri miongoni mwa mashabiki wa soka duniani kuwa yeye na nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo wana chuki na uhasama.
Wakali hao wamekuwa katika vita ya kuwania tuzo za soka duniani, ambapo Messi, alikiri kuvutiwa na soka la mpinzani wake huyo, huku akifafanua kuwa anafanya kazi yake kwa faida ya klabu na si kumthibitishia Ronaldo kuwa yeye ni zaidi.
"Hakuna chuki binafsi (na Ronaldo) kwa namna yoyote," alisema Messi Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Fifa mwenye miaka 26 kuliambia gazeti la Maxim.
"Ronaldo ni mtu mzuri na anaweza kubadili mchezo wowote. Yeye anafanya vitu kivyake na mimi najitoa kadiri niwezavyo kuipa mafanikio Barcelona," alisisitiza Messi nyota wa kimataifa wa Argentina.
Messi alikuwa akisisitiza nia yake ya kufikia malengo binafsi, lakini muhimu zaidi ni kufanikisha mipango ya klabu yake, hasa katika kipindi hiki ambacho inajaribu kuzika jinamizi la kujiondoa kazini kwa kocha wao Tito Vilanova.
"Tunataka kutwaa ubingwa wa Hispania na Ulaya msimu huu," alifichua na kuongeza: "Ilikuwa ni huzuni kwa namna Vilanova alivyoondoka, lakini kwa sasa sote tuko chini ya kocha mpya (Tata Martino).
"Na sio suala la bahati mbaya kwamba wachezaji wa Barcelona tumekuwa tukifanya masuala ya kimaisha chini na kutupa mafanikio.
"Tunajitambua kwamba sisi ni wachezaji, sio nyota wa filamu. Wakati tusipokuwa na mazoezi au mechi, tunakuwa nyumbani na familia zetu," alisema Messi.
No comments:
Post a Comment