Everton yakataa fedha za Man Utd
KLABU ya Everton imeripotiwa kuikataa ofa ya pauni milioni 28 kutoka kwa Manchester United kwa ajili ya kuwasajili beki wa kushoto Leighton Baines na kiungo-mchezeshaji Marouane Fellaini.
Man United walituma ofa ya pauni milioni 16 kuomba ridhaa ya kumsajili Fellaini - wiki mbili baada ya kumalizika kwa muda wa kutengua kipengele chake cha kumuuza kwa ada ya pauni milioni 23.5, huku wakiongeza pauni 12 kwa ajili ya Baines.
Lakini katika namna ambayo haikutarajiwa, Everton haraka waliikataa ofa hiyo kutoka kwa kocha wao wa zamani David Moyes, ambaye kwa sasa anainoa Man United akirithi mikoba iliyoachwa wazi na Sir Alex Ferguson.
Inaaminika Everton watakuwa tayari kuwauza wachezaji hao kwa angalau kuanzia dau la pauni milioni 38 na sasa inasubiriwa kama Man United watakuwa tayari kuongeza paundi millioni 10 ili kufanikisha dili hilo kabla ya siku ya mwisho ya uhamisho wa kiangazi.
Harakati za Man United kumnasa Fellaini zinatokana na kukata tamaa ya kumpata Cesc Fabregas, huku Baines akija kuchukua mikoba ya Patrice Evra. Nyota wote wawili walikuwa kikosini katika mechi ya ufunguzi wa ligi ya sare ya 2-2 dhidi ya Norwich.
Moyes ni mfuasi mzuri wa soka la wakali hao, ambao wote aliwasajili akiwa Everton, Baines akimtoa Wigan kwa dau la pauni milioni 6 Agosti 2007, huku Fellaini akimng’oa Standard Liege ya Ubelgiji kwa dau rekodi ya klabu la pauni milioni 15, Septemba 2008.
No comments:
Post a Comment