Yanga TV kuonekana ndani ya Azam Media
HATIMAYE mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga,
wameamua kufuata nyayo za watani wao Simba, baada ya kukubali kuingia mkataba
na Azam Media ili kurusha kipindi chao kitakachojulikana kama Yanga TV.
Awali, Yanga walikataa udhamini wa Azam TV
kurusha mechi zao za Ligi Kuu Bara, kwa madai mbalimbali, ikiwamo kupinga dai
la sh milioni 100, kabla ya juzi kulipeleka suala hilo Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, ambako lilijadiliwa na pande zinazovutana kufikia
mwafaka.
Klabu nyingine za Ligi Kuu ikiwamo Simba,
ziliafiki udhamini, ambapo mbali ya sh milioni 100 hizo za udhamini wa Ligi Kuu,
Wekundu hao wa Msimbazi, awali waliingia mkataba wa sh milioni 300 na Azam
Media kurusha vipindi vyao vikijulikana kama Simba TV.
Habari zilizoifikia zinasema kuwa Yanga na Azam Media, walianza vikao juzi na kuzungumza mambo
mengi likiwamo la kipindi chao cha TV kurushwa Azam TV, ili waweze kuwa tofauti
na timu nyingine, kutokana na ukubwa wa jina na idadi kubwa ya mashabiki.
“Baada ya kukutana na Naibu Waziri, Yanga na
Azam Media walikaa na kuanza mazungumzo na wamefikia pazuri, ambapo na wao
watapewa udhamini kama waliopewa Simba wa sh milioni 300 kuonesha kipindi chao katika
Azam TV,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake, kwa
kuwa bado pande hizo zinaendelea na mazungumzo, japokuwa wamefikia pazuri.
Aidha, chanzo chetu cha habari kiliwasaka viongozi wa
pande hizo, Azam TV, Said Mohamed na Yanga, Clement Sanga, ambao walikuwapo juzi
katika kikao na wizara.
Mohamed alisema bado wanaendelea kuzungumza na
mara baada ya kufikia mwafaka wataweka wazi suala hilo kuanzia leo huku Sanga
simu yake ya kiganjani ikiwa haipatikani.
No comments:
Post a Comment