Uchaguzi Mkuu TFF kupigwa Okt. 20
Rais wa TFF, Leodegar Tenga |
Mchakato kuelekea uchaguzi huo umepangwa kuanza kesho kwa wadau kuanza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Hamidu Mbwezeleni, alisema kuwa nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi wa Shirikisho ni Rais, Makamu wake na wajumbe 13 wa Kamati ya Utendaji, watakaowakilisha kanda tofauti, huku uchaguzi wa Bodi ya TPL ikiwa ni nafasi ya Mwenyekiti, Makamu na wajumbe wa bodi hiyo.
Akizungumzia mchakato huo uliosimamishwa awali na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Mbwezeleni alisisitiza kuwa wagombea wanapaswa kuzijua sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi huo, ambazo zinapatikana katika ‘Election Menu’ ya TFF, ili kujua miongozo na taratibu ili kuondoa malalamiko.
“Sababu za kuchelewa kwa uchaguzi huu ziko wazi, ni agizo la Fifa kutaka kuwapo kwa Kamati ya Maadili. Kamati iko tayari, imekuja wakati mwafaka ambao taifa linaugua ugonjwa mbaya wa ukosefu wa uadilifu miongoni mwa viongozi,” alisema Mbwezeleni.
Alisema anaamini kamati yake ikishirikiana na ile ya Maadili, watafanikisha mchakato sahihi, huru na wa haki wa uchaguzi, huku akitoa angalizo kwa watakaojaribu kudanganya kwa kuwasilisha sifa bandia, kuwa wataingia kitanzini.
Alifafanua kuwa fomu kwa wagombea zitatolewa kuanzia kesho saa 3 asubuhi hadi saa 10:00 alasiri kwenye ofisi za TFF na mwisho wa kuchukua na kuzirudisha itakuwa Agosti 20.
Mbwezeleni, alitaja bei za fomu hizo kuwa ni sh 500,000 kwa nafasi ya Rais, sh 300,000 Makamu wa Rais na wajumbe sh 200,000.
Kwa Bodi ya Ligi Kuu, Mbwezeleni alisema Mwenyekiti ni sh 300,000, Makamu wake sh 200,000 na wajumbe sh 100,000, ambapo kwa wale waliolipia fomu za uchaguzi uliofutwa na wanakusudia kugombea nafasi zile zile, hawatalipia tena ada ya fomu husika, bali wataambatanisha stakabadhi za malipo (risiti), wakati wa kuzirejesha.
Mbwezeleni, mwanasheria mkuu wa zamani wa Zanzibar, aliongeza kuwa hakuna kizuizi kwa wagombea waliokuwa wamekataliwa katika mchakato wa awali kujitosa katika uchaguzi huu.
Akielezea suala la pingamizi kwa wagombea, Mbwezeleni alisema kuwa utaratibu wa awali wa yeyote kuweka pingamizi, kwa sasa hautotumika, kwani ulichangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa pingamizi ‘hewa,’ ambapo waliopinga hawakutoa ushahidi kwa kamati.
“Kwa sasa watakaoruhusiwa kuweka pingamizi ni wanachama wa TFF, ambao ni vyama vya soka vya mikoa, vyama vya waamuzi, wachezaji, viongozi wa klabu na viongozi wa kuteuliwa, ili kukwepa usumbufu wa baadhi ya wanaopinga kutotoa ushirikiano unaohitajika,” alisema Mbwezeleni.
Katika mchakato uliofutwa, aliibuka mdau aliyejiita Agape Fue na kumwekea pingamizi mmoja wa wagombea, huku mwenyewe akiwa hajawahi kujitokeza hata siku moja, kitendo kilichoibua malalamiko lukuki.
Aidha, Mbwezeleni alivitaka vyombo vya habari kuzisaidia kamati za Uchaguzi na ile ya Maadili kwa kufanikisha uchaguzi huru na wa haki, usio na malalamiko yatokanayo na upotoshaji wa habari na madai ya kupandikiza kutoka kwa wagombea watakaopingana na uamuzi wa kamati.
“Hii ni ngoma, wachezaji ni kamati husika na wagombea. Wanahabari msigeuke wachezaji, nyie ni watazamaji na mnapaswa kubaki hivyo, ili kujua nani kati ya sisi (kamati) na wao (wagombea) wanacheza vizuri na kwa usahihi,” alisisitiza Mbwezeleni.
Wakati huo huo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokuwa ikutane juzi Agosti 13 na jana Agosti 14 kupitia usajili wa wachezaji kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza, haikufanya hivyo na sasa itakutana kesho saa 4 asubuhi.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Alex Mgongolwa, amepanga kesho, baada ya vikao vya juzi na jana kushindwa kupata akidi.
No comments:
Post a Comment