Neymar atabiriwa makubwa Barcelona
SIKU moja baada ya Neymar kuanza kwa sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kirafiki na Lechia Gdansk, kiungo wa FC Barcelona, Xavi Hernandez, amemtabiria neema, ustawi na mafanikio dimbani kwa Mbrazil huyo aliyesajiliwa kwa dau la dola milioni 75.
Xavi amesema ana imani kuwa nyota huyo aliyetua hapo akitokea Santos ya nyumbani kwao Brazil, atapata mafanikio akiwa Blaugrana, anakotarajiwa kubebwa na ushirikiano wake na Lionel Messi na nyota wengine Camp Nou.
“Neymar atafanya vitu tofauti akiwa Barca,” alisema Xavi, 33 na kuongeza: “Ana kasi ya ajabu na anafunga mabao. Kuwa na Messi, Neymar na wachezaji wengine wote ni uhakika wa kutusaidia kila mmoja kufanya kilicho bora mchezoni.
“Wachezaji bora na wakubwa hutoa ubora wao kwa wengine mchezoni. Naamini Neymar atakuwa bora zaidi akiwa pamoja na Messi na Messi atakuwa bora zaidi kwa kuwa tu pamoja na Neymar kikosini.
“Tutajaribu kadri tuwezavyo kumsaidia Neymar kukabiliana na changamoto mpya Camp Nou, kumfanya awe na furaha na kufikia ubora wake kama aliokuwa nao akiwa anacheza Brazil.”
Aidha, ingawa Real Madrid imeripotiwa kutenga kitita cha euro milioni 115 kufanikisha uhamisho wa Gareth Bale kutoka Tottenham kwenda Bernabeu, Xavi amedai kuwa yeye binafsi anajua mambo machache kumhusu winga huyo wa kimataifa wa Wales.
“Sijui kabisa kama Bale ana thamani hiyo wanayosema Madrid,” alibainisha Xavi na kuongeza: “Kusema ukweli ni kuwa sijawahi kumuona Bale akicheza angalau kwa dakika 90.”
No comments:
Post a Comment