PAMOJA na ukweli kuwa Gareth Bale kwa sasa ndie mwanasoka ghali duniani baada ya kujiunga na Real Madrid kwa kitita cha euro mil 100 akitokea Tottenham ya England, Rais Florentino Perez amesema ni fedha kiduchu.
Perez, kiongozi anayefahamika kwa sera yake ya kununua nyota wa bei kubwa, amesema japo kiasi hicho kinaonekana kikubwa, lakini fedha hiyo hailingani na thamani yake halisi kwa maana ya uwezo wake dimbani.
Alisema kiasi cha fedha walizotoa kumpata nyota huyo kwenda Santiago, ni kutokana na ukweli kuwa wasingeweza kwenda mbali zaidi ya hapo japo uwezo na thamani halisi ya mchezaji huyo ni zaidi ya kiasi hicho.
"Ukiangalia uwezo wake halisi dimbani na fedha tuliyomnunulia, naweza kusema Bale ametua Madrid kwa bei chee," alisema kiongozi huyo alipozungumza na Cadena SER na kuongeza:
"Kusajili mchezaji kwa kiwango kikubwa ni filosofia ya klabu hii kwa sababu tunaamini ndiye bora kwa msimu huu. Tumekuwa tukimfuatilia kwa miaka miwili.
"Awali, Tottenham hawakutana kumuuza, lakini tuliposikia Manchester United wanamtaka, tukaketi nao kujadili. Hata hivyo kiu yake ya siku moja kucheza Real Madrid tangu akiwa mtoto, ikawa siraha kwetu," alisema.
Tangu Bale atue Real Madrid, amecheza mechi moja dhidi ya Villarreal na kufunga bao, lakini akikosa mechi ya wikiendi iliyopira dhidi ya Getafe kutokana na maumivu ya paja.
Maumivu hayo ya paja yamemzuia Bale kucheza mechi ya leo ya La Liga dhidi ya Elche, lakini huenda akwa fiti kuelekea mechi itakayofuata dhidi ya watani wao wa jadi, Atletico Madrid.
No comments:
Post a Comment