Kocha Cameroon akerwa Eto’o kustaafu
KOCHA wa timu ya taifa ya Cameroon, Volke Finke amekanusha habari kuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Samuel Eto'o ameamua kustaafu soka ya kimataifa.
Kauli ya kocha huyo inatokana na habari kuwa, Eto’o (32), nyota bora mara nne wa Afrika kwamba mechi ya Jumamosi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia dhidi ya Libya, ilikuwa ya mwisho kwake.
Katika mechi hiyo ya kundi I, Cameroon walishinda bao 1-0, hivyo kumaliza kinara wa kundi hilo kwa pointi 13 na kutinga hatua ya 10 bora itakayotoa timu tano za kwenda Brazil kwa fainali za Kombe la Dunia.
Nyingine zilizotinga hatua ya 10 bora ni Ethiopia, Algeria, Senegal, Burkina Faso, Nigeria, Misri, Ghana, Ivory Coast na Cape Verde kucheza hatua hiyo ya kupigania nafasi tano za kwenda Brazil, mwakani.
Baada ya miamba 10 kujulikana, Septemba 16 kutafanyika droo itakayozingatia ubora kwa mujibu wa viwango vipya vya Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa) kwa timu kucheza mechi mbili, nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla kujitwalia tiketi.
"Samuel Eto'o ni mchezaji mahiri, hivyo ingependeza kama kauli hiyo ingetoka kwake. Yeye pekee ndiye wa kufanya maamuzi sahihi," alisema Finke.
"Ameiletea mafanikio makubwa soka na Cameroon, ndio maana nasema yeye ndiye angeweza kulisema hilo sio kusemewa."
Eto'o aliyetua Chelsea hivi karibuni akitokea Anzhi Makhachkala ya Russia, hakutokea kwenye mkutano na waandishi wa habari kuelezea kama kweli amestaafu timu ya taifa au hapana.
Hata hivyo, kuna habari kuwa nyota huyo anakusudia kustaafu soka ya kimataifa akitaka kujielekeza zaidi katika kuendeleza kituo chake cha soka ya vijana.
Aidha, Eto'o amekuwa na jukumu la kumtibia aliyekuwa kocha wa Cameroon, Jean Paul Akono, aliyepatwa na maradhi ya kupooza mapema mwaka huu.
Baaada ya Cameroon kuifunga Libya katika mechi ya jana usiku, Finke alimpongeza Akono, aliyemrithi kwenye nafasi hiyo ya Indomitable Lions.
"Nampongeza Jean Paul Akono, aliyeshinda mechi tatu za kwanza katika kampeni hii, hivyo ni sehermu ya mafanikio ya leo," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.
Baada ya kutinga hatua ya 10 bora, kazi kubwa iliyobaki kwa Cameroon ni kusubiri kuona inapangwa kucheza na nani katika mtoano kwenye droo itakayofanyika Septemba 16, itakayofanyika Cairo, Misri.
No comments:
Post a Comment