Gareth Bale apata majeraha
GARETH Bale aliyetua Real Madrid akitokea Tottenham kwa dau kubwa linalomfanya kuwa ghari zaidi, ameumia nyonga kwenye mazoezi kuelekea mechi ya kimataifa kati ya Wales na Macedonia iliyochezwa Ijumaa iliyopita.
Baada ya Bale kukosa mechi hiyo ambayo Wales walifungwa, kocha wake Chris Coleman amesema atafanyiwa vipimo zaidi kuona kama atacheza mechi dhidi ya Serbia, itakayochezwa mjini Cardiff.
"Tunapaswa kufanya kitu kwa Gareth kabla ya mechi kwa sababu ana maumivu ya nyonga," alisema kocha huyo na kuongeza kuwa kipimo hicho ndio kitatoa majibu yote.
Wakati nyota huyo akiwa majeruhi, Klabu yake ya Real Madrid aliyojiunga nayo hivi karibuni kwa kitita cha pauni mil 86, ilipanga kumchezesha katika mechi la La Liga ya Septemba 14 dhidi ya Villarreal.
Bale sasa anaungana na Cristiano Ronaldo ambaye naye anaweza kukosa mechi hiyo kutokana na kukabiliwa na maumivu.
Kuhusu Bale, kuna habari kuwa Real Madrid ndio iliomba asipangwe kwenye mechi ya Ijumaa dhidi ya Macedonia na Serbia itakayochezwa leo.
Pamoja na hayo, Bale mwenyewe anataka kucheza ili kuboresha kiwango chake, pia ni heshima kuichezea nchi yake na kuisaidia katika kampeni ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia.
"Nina maumivu madogo yatakayochukua muda mfupi kupona, lakini mara zote nipo hapa kuiwakilisha Madrid. Naamini nitapangwa katika mechi ya nchi yangu (Wales) ili kuboresha kiwango changu kuelekea mechi ya Real Madrid dhidi ya Villarreal," alisema.
No comments:
Post a Comment