Friday, August 16, 2013

Ushabiki wamponza Mrisho Ngasa

Ushabiki wamponza Mrisho Ngasa
KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imepitia usajili wa Ligi Kuu na kumuidhinisha mshambuliaji Mrisho Ngasa kuchezea timu ya Yanga, huku ikimfungia mechi sita na kumtaka kurejesha sh milioni 30 na fidia ya asilimia 50 kwa klabu ya Simba.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa, imebaini kuwa ni kweli Ngasa alisaini mkataba mwingine Simba katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam, ambako alipewa kiasi hicho cha fedha.
Kutokana na kubainika kwa hayo, Ngasa anatakiwa kurejesha fedha alizopokea, sh milioni 30, pamoja na fidia ya asilimia 50 (ambayo ni sh milioni 15), hivyo kulipa jumla ya sh milioni 45, kwa Wekundu wa Msimbazi, ambao walimtoa Azam FC kwa mkopo.
Kamati ya Mgongolwa, pia imemfungia Ngasa kucheza mechi sita za mashindano zilizo chini ya TFF, kuanzia Ngao ya Jamii kesho, baina ya Yanga na Azam FC, na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi cha kukosa mechi hizo.
Endapo Ngasa atashindwa kulipa fedha hizo kwa wakati huo, hatoruhusiwa kucheza hadi atakapokamilisha hilo.
Aidha, kamati imepitia pingamizi zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi Agosti 22.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata hati za uhamisho wa kimataifa (ITC), pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini.
Kamati hiyo itakutana tena Agosti 23 ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 na kutoa uamuzi kwa pande ambazo hazikuafikiana.
Wakati huo huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa kuzingatia mamlaka iliyonayo katika kifungu cha 10(6), cha Kanuni za Uchaguzi, imesogeza mbele tarehe ya uchaguzi mkuu kutoka Oktoba 20 hadi 27, ukitanguliwa na mkutano mkuu siku moja kabla, huku ule wa Bodi ya Ligi Kuu ukibaki kuwa Oktoba 18.
Sababu za kusogeza mbele uchaguzi huo ni kutokana na kuwa Oktoba 20 uongozi wa TFF utakuwa na shughuli nyingi za maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga na hivyo haitawezekana kusimamia shughuli za mkutano mkuu wa uchaguzi kwa wakati mmoja na mchezo huo.
Kutokana na mabadiliko hayo, siku ya mwisho ya kampeni itakuwa Oktoba 25, badala ya Oktoba 17 ya awali na ukiondoa mabadiliko hayo, ratiba ya mchakato wa uchaguzi itabaki kama ilivyotangazwa na kamati hiyo Agosti 24 mwaka huu.
Wambura alibainisha kuwa kamati inaamini wahusika wote watapokea vema mabadiliko yaliyotokana na Sekretarieti ya TFF kumwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, kumuomba kupishanisha mechi na uchaguzi, kwa vile yeye na kamati yake ndio wenye mamlaka.

No comments:

Post a Comment