HATIMAYE mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez, jana alifanya mazoezi na wenzake wa kikosi cha kwanza Cha Liverpool baada ya kufanya majadiliano na kocha wake, Brendan Rodgers.
Suarez, 26, aliyekuwa akitaka kuhama Anfield bila mafanikiuo, alirejea katika kikosi cha Liverpool tangu Alhamisi baada ya kuichezea Uruguay katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Japan na kushindwa mabao 4-2, mjini Miyagi.
Awali, nyota huyo aliyekuwa akifanya mazoezi kivyake baada ya kutaka kulazimisha kuondoka Anfield kwa njia ya kisheria hadi pale atakapoomba radhi kwa kocha wake na klabu ya Liverpool.
Licha ya Suarez kuwindwa vikali na klabu kadhaa hasa Arsenal ambayo hata mchezaji mwenyewe alisema alitaka kujiunga nayo akitaka kucheza Ligi ya Mabingwa, mpango huo umekwama na nyota huyo amekubali matokeo.
"Ninataka kuelekeza nguvu na akili zangu katika kucheza soka," alisema Suarez atakayekosa mechi sita za Ligi Kuu inayoanza leo kwa kosa la kumng’ata sikio beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic tangu Aprili mwaka huu.
Suarez, aliyetua Liverpool tangu Januari 2011, akitokea Ajax ya Ufaransa kwa kitita cha pauni mil 22.7, amecheza jumla ya mechi 44 na kufunga mabao 30.
No comments:
Post a Comment